Saturday, 6 May 2017

Baada ya kutemwa kwa kughushi: Mlevi kuvamia siasa


Japo ni jambo la aibu, sina budi kulieleza. Mwenzenu nilipokuwa nikiwakoga na maulaji yangu kwenye ofisi ya umma, sikuwaambia ukweli. Ukweli ni kwamba nilikuwa natumia cheti cha kughushi nikichanganya na vile halali nilivyopata baada ya kupata nafasi chuo kikuu kwa kutumia vyeti vya jamaa zangu. Hivyo, hii ndiyo siri ya kuwa na majina mengi na tata.
Baada ya waziri wa Utumikishaji kuanzisha nchakato ulionibaini, nimeamua kuachana na ajira. Badala yake napiga mahesabu kuingia siasa. Kwa vile ninataka kuendelea na kanywaji na ulaji,  sitajiunga na wapingaji. Hawa hawana sirikali wala ulaji ninaoutaka.
Baada ya kugundua kuwa kumbe katiba yetu ya viraka inawakingia kifua vihiyo waliojiunga na siasa na wakateuliwa kwenye ulaji, ifuatayo ni mikakati yangu katika mishemishe yangu ya kuendelea kuula na kuukata baada ya zoezi la uhakiki wa vyeti kunivua nguo:
Mosi, kwa vile bado mimi ni kijana, nitakata kadi ya chama twawala kama kianzio.
Pili, nitajiunga na umoja wa vijana ili nianze kujijengea jina. Hapa, kwa vile nimejaliwa kipaji cha kuchonga, nitaanza kujipendekeza kwa wakubwa ili wanione na kuniibua ghafla bin vuu.
Tatu, nitafanya urafiki kwa gharama yoyote na wale waliobainika kuwa mabingwa wa kughushi na kuteuliwa kwenye nafasi kubwa kubwa zenye ulaji mkubwa. Hapa jamaa yangu mmoja toka Koromija lazima awe mshirika wangu kwa gharama yoyote.
Nne, nitaanza kuwaponda wapingaji hata kujitoa mhanga kupigwa risasi kwa kuwashughulikia. Katika kufanikisha hili, nitajitahidi kuunga mkono kila anachosema dingi. Nitatumia usanii wangu wote. Nitakuwa kiongozi wa dini ambaye hawezi kuongea bila kuwataka walevi wamuombee dingi kutokana na mema anayofanya.
Tano, nitatumia dhana ya kimbelembele (presumptous  theory) kuhakikisha dingi ananiona na kunipa ulaji chapchap. Katika dhana hii, mhusika huvunja kila kanuni ili mradi atakalo liwe. Huwa mhusika haogopi lawama toka kwa anaowakwaza iwapo kufanya hivyo kutafanya anaolenga kuwaingiza mkenge wamwamini na kumteua watafurahi na kuridhika naye.  Mifano mizuri ya wasanii waliowahi kutumia dhana hii na kufanikiwa ni Isaac Maliyamungu, msanii aliyemtumia dikteta Idi Amini kuukwaa ulaji akatenda uovu usiosameheka kwa waganda. Wengine ni Hermann Goering, Joseph Goebbels na Heinrich Himmler waliopata ushawishi mkubwa enzi za manazi wa kule Ujerumani chini ya muuaji Adolf Hitler. Mwingine wa hivi karibuni ni Abdullah Sennusi aliyemtumia marehemu Muamar Gaddafi wa Libya kama alivyotaka baada ya kumzidi kete hadi akamzimia. Hivyo, wanaodhani hizi ni ndoto za bangi na kanywaji, wafikiri upya. Ukiitumia vizuri dhana ya kimbelembele, unawapumbaza hata wasiotegemewa. Dhana hii imeonyesha kufanikiwa sana kuwanasa watu maarufu wanaojiamini sana na wanaoogopewa. Anayebisha, akamuulize dogo Bashsit pale Bongo kama mnadhani nazua.
Hapa lazima nije na mbinu kali ya kuhakikisha navaa nguo zinazofanana na za dingi huku nikirudia maneno yote yawe ya kufurahisha au kuudhi anayosema dingi. Kwa lugha rahisi ni kwamba nitajigeuza kasuku mtu wa kukariri na kubwabwaja kila asemacho dingi.
Chini ya dhana ya kimbelembele au presumptous theory kwa kinyasa, unapoaminiwa ulaji, hufanyi lolote bali kumfurahisha, kumpumbaza na kumridhisha aliyekupa ulaji. Hapa lazima uingilie na kufanya kila kitu ilmradi muungu wako ufurahi.
Kwa vile mimi ni bonge la msanii na kimbelembele nisiye na mfano, lazima nitatoboa piga ua. Hapa lazima nianze kusoma hotuba za dingi ili niweze kuzinukuu kwa kila ninachosema. Lazima nijue nani ni marafiki na maadui zake ili niwatumie maadui kujijenga huku nikijiweka karibu na marafiki zake ili kujua siri za dingi. Naona yule anacheka akidhani hizi ni bangi zinazonibangua na kuwazia yasiyowaziwa. Ngoja mtanisikia naibu ghafla kwenye nafasi nyeti hadi wabaya wangu wajinyonge kabla sijawasakizia jinai mbali mbali. Unafanya nchezo na usanii katika kaya hii ya Danganyika aka Bongolalaland? Sina PhD ya kweli wala Masters zaidi ya shahada yangu niliyopata kwa kutumia majina ya marafiki zangu. Lakini aminini. Nina uwezo wa kuwafanya wenye PhD tena kali kunitumikia kwa kuwatumia bila wao kustuka.
Nimalizie kwa kuwataka washikaji zangu tuliokuwa tukisota wote pale Uwanja wa Hyena kwa Mfuga Dog. Mtakaponikuta meza kuu nikiwa na ukuu utokanao na usanii wangu, msinifichue wala kushangaa. Rafiki yangu mmoja toka Nigeria aliyesifika kwa kuandika vitabu vilivyokwenda shule aitwaye Chinua Achebe aliwahi kuandika “mtoto akinawa mikono yake, anaweza kula na wafalme.
Tuonane wiki ijayo nitakapotongoa ni kwanini njaa ikipanda kichwani PhD hugeuka Bullshit aka Bashiit.
Kwaheri kutoka Koromija.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: