Saturday, 13 May 2017

Njaa Inapopanda Kichwani PhD Hugeuka Bullshit

Image result for photos of profesa paramagamba kabudi
          Juzi wakati waheshimiwa wa mjengoni wakijadili bajeti, pamoja na ulevi wangu, niligundua kitu ambacho wengi hawajaona. Kama si jamaa yangu mmoja, tena aliyekuwa akionekana msomi wa kweli mwenye PhD ya sharia kama mimi kuonyesha ukihiyo wake tena hadhani kwenye njengo, nisingeandika haya. Jamaa ambaye ana bahati ya kuteuliwa kwenye kabineti kupitia viti vya dezo si ukafika wakati wa kuchangia bajeti ya wizara yake. Badala ya ongelee yaliyomo kwenye bajeti yake, akapaaza sauti tena kwa hasira baada ya dogo mmoja kumzodoa. Badala ya kuelezea wizara yake itakavyotenda haki kwa walevi hasa wanaosumbuliwa na kesi za kubambikiwa na ndata ukiachia  mbali kuchukua miaka kibao kuhukumiwa, jamaa alianza kumsifia malkia wa utashani utadhani kaya yetu bado ni koloni. Aliniacha hoi pale alipodai malkia ni taswira ya kaya ya utashani; hivyo na rahis wetu ni hivyo. Sidhani kama tunapaswa kuendelea na hekma za kikoloni kama hizi. Taswira ya kaya ni wana kaya wenyewe hata kama ni ombaomba na walevi. Sijui kama rahis mwenye kuvaa suti za bei kali huku akisafiria midude ya bei mbaya anaweza kuwa taswira ya kweli ya walevi waliopigika. Hapa lazima wasomi wetu wajifunze kuwa critical na siyo ku-bloviate na ku-pontificate mambo na kukariri kama kasuku.
            Hakuna jamaa aliponiacha hoi kama kulalia kwenye kitumbua chake kiasi cha kujigongagonga kwa waliompa ulaji akasahau kuwa wahishimiwa walikuwa wakijadili bajeti ya walevi wote. Hata hivyo, anamwakilisha nani zaidi ya aliyempa ulaji na tumbo lake? Ajabu nyingine ni pale jamaa alipotoa mpya kuwa anajivunia kuwa mteuliwa dezo. Wale waliohenyekea ulaji walimshangaa wakabaki kutikisa vichwa kuonyesha namna gani alikuwa amechemsha.
            Badala ya kuongelea sera aliendelea kujigonga kwa waliompa ulaji kiasi cha kutia kinyaa ukiachia mbali kuwaacha wengi vinywa wazi wakihoji ubobezi na usomi wake. Walevi waliokuwa wakiangalia video hii ya dezo walibaki kushangaa. Mmoja alisema “kumbe ndiyo maana wamezuia kuonyesha haya maigizo laivu siyo!”
            Jamaa ambaya huitwa profwedheha sawa na Annae Kajuamlo, alipandisha mizuka kiasi cha kugeuza mjengo kuwa chumba cha lecture. Ajabu ya maajabu, kidhabi huyu aliyekuwa akitetea ulaji wake kwa kumtukuza muungu uliomteua, alianza kufundisha kimakonde badala ya sharia jambo amblao lilizidi kuwaudhi na kuwachanganya walevi. Jamaa kuonyesha elimu yake ilivyo na shaka, si akaanza kuwatukuza wakoloni kuwa ni wastaarabu na hawawezi kumwambia mlevi kuwa ni bunga au zoba pale anapoonyesha kutoelewa.  Ajabu ya maajabu, mwalimu wangu huyu hakuelewa hata somo lake kiasi cha kuanza kurusha matusi akiwaita waishiwa wenzake wapumbavu badala ya kuiga ustaarabu wa mabwana zake aliowasifia kupita kiasi.
            Mwalimu huyu wa ukoloni aliwaacha walevi hoi pale alipowambia wahishimiwa kuwa wanaongea kimakonde kikavu wakati yeye akiongea kilichoungua.  Ni kwanini jamaa huyu anayonekana kapiga buku alisahau kujua kitu kimoja kidogo kuwa wahishimiwa hawakwenda kwenye mashindano ya kuongea kimakonde bali kuwawakilisha walevi. Sijui kama jamaa alikuwa na chembe ya kumbukumbu. Kwani, kati ya wanaoongea kimakonde kikavu ni ule muungu uliompa huo ulaji uliomchetua kiasi cha kujikanganya na kuchanganyikiwa ukiachia mbali kuwachanganya walevi.
            Hivi inasaidia nini mlevi tena anayeheshimika kama msomi kwenda mjengoni kufundisha kimakonde au historia ya sharia kwa wahishimiwa badala ya kuelezea sera zake? Hapa ndipo namkumbuka mhishimiwa mmoja aliyesema kuwa ukiona mlevi mwenye PhD anajigonga kwa wenye ulaji, ujue hajaelimika hata kama alipata A+ kwenye masomo yote. Hamkumuona yule mwingine anayepoteza muda kibao bila kutoa maelezo juu ya uchunguzi wa jinai ya Kalauds ambao umemfanya aendelee kunywea kwa kuogopa kijitu chenye division zero? Hivi huyu naye ni msomi wa kweli kweli?
            Kwa vile naona kipenga cha kwenda kupata kimelia, leo nitaachia hapa kwa kuwataka wasomaji na walevi waanza kubadili tabia ya kuamini kila anayesema ana PhD. Lazima tupime matendo na mawazo yao. Kwani, wengi walikariri tu. Ukitaka kujua ninaomaanisha, angalia wale wote wanaoogopa au kutumiwa hata vihiyo walioghushi kama Bashit. Sijui kati yao na huyu jamaa nani anayeweza kuitwa msomi. Sijui maana ya usomi kama usomi wenyewe ni ukasuku, ukuku na upwakiaji wa madude bila kupitisha kwenye bongo la yule anayefanya hivyo. Ama kweli, njaa inapopanda upstairs, PhD yaweza kugeuka Bashit kama siyo bullshit.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: