HiVI
karibuni kuliripotiwa habari kuwa msafara wa Naibu Waziri wa Maji, Binilith
Mahenge ulipata ajali baada ya gari mojawapo katika msafara ule kumgonga mtoto
Adam Ramadhani huko Muheza. Waziri alikuwa wilayani humo kukagua miradi ya
maendeleo.
Japo ni kazi ya waziri kukagua miradi ya maendeleo,
ukiangalia kwa undani, mazoezi kama haya yanalitia taifa hasara. Si uzushi. Siku
hizi karibu kila mwenye kacheo kake ni mkubwa kiasi cha kuhitaji msafara wa
magari.
Kwa kiasi fulani tumegeuka nchi ya wapenda sifa na
misafara vitu ambavyo vinasababisha matumizi mabaya ya pesa za walipa kodi wetu
maskini.
Inashangaza kuona nchi maskini kama zetu zinakuwa na
matumizi ya ajabu na kijinga wakati nchi tajiri hazifanyi hivyo.
Nitoe mfano. Katika nchi tajiri, waziri au mbunge
hapewi dereva wala mlinzi au wabeba mikoba (wasaidizi).
Anaendesha gari lake mwenyewe na sifa mojawapo
katika kugombea ubunge lazima ajue kuendesha.
Hii inalenga kuokoa pesa za walipa
kodi.
Inakuwaje tunafuja pesa ya umma, mfano, kwa kutoa
walinzi ofisini na nyumbani, madereva, makatibu muhtasi na vikorombwezo
vinginevyo vingi wakati bajeti yetu inategemea kuomba?
Hata wabunge na mawaziri wa nchi tajiri, licha ya
kuendesha magari yao wenyewe, hawatumii magari ya bei mbaya kama ya wabunge wa
nchi maskini kama yetu.
Ukiangalia Tanzania, unashangaa mantiki na busara ya
kufuja mali ya umma namna hii.
Mkuu wa wilaya, mkoa, idara, wizara, mbunge na
waziri wote wana misafara kila waendeko. Na watembeleapo eneo fulani basi
wakubwa wa eneo husika wataacha kazi zao na kushiriki misafara hii ya hasara na
ya kizamani.
Wanatumia magari mengi bila sababu huku wakifuja
mafuta na kuchafua mazingira na kusababisha umaskini kwa walipa kodi bila
sababu.
Kimsingi, nchi yetu inaendeshwa kisiasa badala ya
kiuchumi. Wanasiasa wana sauti kuliko wachumi na mambo ya kisiasa yanapewa
kipaumbele zaidi yale ya kiuchumi. Namna hii hatuwezi kuendelea.
Ukiachia ugonjwa wa kupenda misafara na sifa, kuna
tatizo jingine la wanasiasa kuwatumia wananchi katika mambo yasiyo na tija kwa
taifa hata kusababisha kusimamisha uzalishaji.
Mfano, unapowatoa watu maofisini na watoto mashuleni
kwenda kumpokea mkubwa unategemea nini kama siyo kusimamisha uzalishaji na
kuathiri uchumi?
Unapopoteza muda mwingi kwa kufunga barabara kwa
vile wakubwa watapita wakitoka au kwenda uwanja wa ndege unategemea
nini?
Ni ajabu kuwa bado tuna utapiamlo na hang over ya
kikoloni ambapo akija kutembea kiongozi wa taifa jingine tunapoteza muda mwingi
kwenda kumlaki kwa ngoma na makando kando mengine yasiyo na umuhimu. Zama za
kuchezeana ngoma na ngojera zilishapita.
Kwa wenzetu, tena wenye nguvu ya kiuchumi, hata
akija kiongozi wa nchi nyingine anamalizana na mwenyeji wake bila kupoteza muda
na kusababisha hasara kwa uzalishaji na uchumi wa nchi. Ili nieleweke, jirejeshe
kwenye mapokezi mengi yanayofanywa na rais wa Marekani kwa viongozi wa mataifa
makubwa.
Huwa wanafika uwanja wa ndege na kupokelewa na
kikundi kidogo cha watu huku wakikagua gwaride la kikosi kidogo kimoja na mambo
yanaishia pale.
Huwezi kuona maelfu ya watu wa Washington eti
wakijipanga kando ya barabara kumpokea kiongozi wa taifa jingine.
Hata rais anapokuwa akisafiri au kurejea nyumbani,
huwezi kuona baraza lote la mawaziri uwanja wa ndege likienda kumpokea. Kwa lipi
iwapo anachofanya ni kazi aliyoomba?
Inashangaza kuona viongozi wetu wanaosifika kusafiri
sana hawajifunzi vitu kama hivi.
Badala yake wanaendelea na tabia za kikoloni kama
zile zilizokuwa zikionyeshwa na gavana wa kikoloni.
Kwa taarifa yenu, gavana alikuwa akifanya aliyofanya
ili kutudhalilisha na kutupotezea muda ili atunyonye vizuri.
Ni bahati mbaya kuwa watawala wetu wanaabudia mambo
haya ya kihasara kuliko kubadilika.
Hebu jiulize, mfano, misafara, makongamano na hafla
za kujipongeza zinakula kiasi gani kwa mwaka katika bajeti ya
taifa?
Je ni fedha kiasi gani inatumika kununulia mafuta ya
magari yanayotumika kwenye misafara isiyo na ulazima kama vile kumsindikiza na
kumpokea mkubwa uwanja wa ndege?
Kuna haja ya kuiga na kufanya mambo ya maana badala
ya kuendelea kuwa maskini tena kwa kujitakia huku tukidhalilika kwa kuombaomba
na kukopakopa.
Ajabu, wakati tukifanya hii israfu, tunawashauri
watu wetu wafunge mikanda na kuwaaminisha kuwa hali ya uchumi ni
mbaya.
Hakuna hali mbaya zaidi ya ubaya wa akili na
matumizi yetu kimfumo.
Kuna haja ya kufumua huu mfumo tuliourithi toka kwa
wakoloni na kufanya mambo kama taifa na watu walio huru kiakili na kisiasa.
Vinginevyo tutaendelea kutawaliwa kwa ujinga wetu.
Huwezi kutumia zaidi ya unavyopata ukawa huru.
Huwezi kutumia kama mfalme wakati wewe ni kapuku ukaheshimika hata ukijiridhisha
kuwa unaheshimika.
Heshima ya mtu ipo katika uhuru wake si wa kisiasa
tu hata wa kiuchumi.
Hili unaweza kuliona wakati marais wa nchi maskini
wanapotembelea mataifa makubwa.
Hawapokelewi uwanja wa ndege na wenyeji wao kama wao
wanavyowapokea na hata wakiwapokea huwa tofauti na wanavyowapokea. Maisha mazuri
ni nipe nikupe. Unakwenda kutembelea nchi tajiri unaingizwa ikulu kupitia mlango
wa nyuma. Kwanini mhusika akija kukutembelea ukamtendea hivyo badala ya
kujidhalilisha?
Wenzetu wanavyowapokea watawala wetu wanawaonyesha
kiwango cha hadhi yao kwao.
Obama akimpokea rais wa Urusi au Ufaransa inakuwa
issue kwenye vyombo vya habari nchi nzima. Lazima hafla ya kitaifa ifanyike na
kuonyeshwa. Lakini kwa ombaomba wa kiafrika hilo sahau.
Kuna haja ya kuanza kuwaainisha maadui wa maendeleo
yetu
Ingawa tumekuwa tukiwalaumu wakoloni na nchi
mabeberu, kimsingi chanzo cha umaskini wetu ni mabeberu wetu wenyewe yaani
watawala wanaopenda ukubwa, sifa na matanuzi.
Chanzo: Dira Machi, 2013.
1 comment:
MSEMA KWELI HUTUNZWA
Post a Comment