Saturday, 30 March 2013

Mhadhara, mkesha…mhadhara, mkesha!


Wapendwa wasomaji wa safu hii, napenda kuwaleteeni habari njema ambayo bila shaka itakonga nyoyo zenu.
Ninaamini mtakapomaliza kusoma, mtakuwa mmejaa ‘roho mtakakitu’ na kitu chenyewe ni imani na furaha katika maisha yenu.
Ingawa mimi ninafikiri kilevi, ninaamini huduma yangu inawaburudisha na kuwafikirisha wengi. Na hakika, hii ndio dhamira yangu pamoja na safu hii.
Najua ninao wapenzi wengi na maadui kadhalika, kuhusu ninayoyaweka kwenye safu hii. Kwani juzi mtaani kwetu, baada ya kushuka kwenye daladala, kuna `njemba’ ilinitisha.
Ilisema hivi, “we mlevi unayejifanya kuishi Canada nakujua. Hakuna cha kuishi Canada wala nini. Punguza mashambulizi yako vinginevyo tutakunyotoa roho.”
Ingawa sina tabia ya kuogopa vitisho na maneno `mbofu mbofu’, moyoni nilistuka. Kwani, kama wasemavyo Waingereza, my cover was blown out.
Kutaka kuepusha shari, maana mimi kwa `makaratee’ na kung-fu sina mfano, `niliminya’ tu.
Niliwahi kuzipiga na Bruce Lee zama zile na `akaramba’ majani. Yule bwana nilimuonea huruma nikamwambia kuwa alikuwa amenifananisha.
Alisisitiza kuwa mimi ndiye na anamjua hata bibi wa bibi yangu. Aliongeza vitisho kuwa kama nitaendelea, basi anaweza kutoa fedha pale kilabuni ninapokamata `ulabu’ niwekewe sumu.
Mie kwa upole na kujua ambacho kingempata, nilizidi kumwambia kuwa, mimi siye na wala sijawahi kusema ninaishi Canada.
‘Mijitu’ mingine bwana haitaki watu wafaidi `ujiko’. Hivi alitaka niseme ukweli kuwa naishi Kigogo au kwa Mfuga Mbwa, Manzese? Hayo tuyaache.
Leo nimedhamiria kutangaza dini yangu mpya. Nafanya hivyo kutokana na kuona wengine wakifanya hivyo na kufaidi, huku wengine wakiwaumiza wenzao.
Silengi kumfaidi mtu, ingawa kwenye mhadhara na mkesha tutapokea michango kidogo ya kuwezesha jenereta na kuwalipa wahadhiri.
Najua viherehere wataanza kuuliza, “tuwalipe wahadhiri kwani tumewaajiri?” Mbona mnawalipa wale tena wahubiri maafa? Nasi acha tuwale japo kidogo `tugange njaa’ yetu.
Tofauti na wale, sisi tunaohubiri dini hii mpya tumeisomea. Wanaonijua wanajua ni kiasi gani nimesoma hadi nikafika kwenye sehemu chuoni iitwayo ‘No more class for you go and teach others.For you are above all levels of learning on earth.
Kwa lugha rahisi ni kwamba, nilisoma hadi nikafika kwenye ubao ulioandikwa: ‘hakuna darasa linaloweza kukufaa kwa vile una elimu juu ya viwango vyote duniani’.
Naona yule anatikisa kichwa akidhani ninadanganya. Unataka niape kuwa nisemayo ni ukweli? Umenoa. Mimi si mtu wa ‘mjengoni’ au mwanasiasa anayeweza kuapia lolote. Hayo tuyaache.
Naomba nichukue fursa hii kuwapa ithibati ya mihadhara na mikesha yetu. Kwanza, imehalalishwa kwa vile hatushambulii ‘lisirikali’. Pili, tunahubiri bangi ulevi na gongo na si siasa wala uduni.
Hata tukigusia siasa tunazungumzia mazuri tu ya utawala hata kwa kuyaita mabaya mazuri. Ukila na kipofu ‘don’t shika him’ mkono mwanangu.
Tatu, ufalme wa mbinguni uko hapa hapa duniani. Hii ndiyo tofauti na wale wanaohubiri ufalme wa ndotoni ambao wanaotaka kuufikia, lazima wafanye hivyo hata kwa kunyotoana roho.
Sisi hatutoi roho wala hatuna uroho wala roho mtakachafu. Tuna roho mtakakitu--- yaani peace on earth.
Nne, tunachohubiri ni dini mpya ambayo ilisahaulika. Ni dini ambayo ilikuwapo kabla ya kuja kwa ukoloni na unyemelezi.
Ni dini ambayo iliwafanya babu zetu waishi kwa kupendana na kuheshimiana, huku udugu na ujamaa vikitamalaki. Ni dini iliyofanya watu watembee usiku bila kuogopa binadamu, bali wanyama mwitu.
Ni dini iliyozuia watu kujineemesha wao peke yao huku majirani na ndugu zao wakiangamia kwa umaskini.
Ni dini iliyokana utajiri utokanao na uchafu kama vile ufisadi, ushirikina wa kuua zeruzeru, wanyama wetu, miti yetu na rasilimali nyingine. Ni dini inayoabudia utu badala ya vitu kama utajiri na mamlaka.
Ni dini ya kweli hata kama inahubiriwa na walevi na wavuta bangi. Inayoonyesha upendo kwa matendo na si maneno.
Tano, maandiko yetu yanaitwa uhalisia na lugha ya kuhubiria ni kiswahili. Bahati mbaya hayakuandikwa kwenye karatasi bali mioyoni.
Hayahitaji kukariri wala kupigiana kelele.
Sita, hatubadili majina ya mtu isipokuwa kuongeza neno moja tu, mlevi. Pia hatutukani imani za watu wengine. Maana, kufanya hivyo ni kuwachokoza.
Saba, ingawa sikulipia tangazo hili, nalitoa kuwapa watu wote moyo waje kwenye dini yetu mpya. Ninaamini na serikali itatuvumilia kama ilivyowavumilia wanaohubiri shari na mauaji.
Hatuna ugomvi na mavazi ya mtu hasa akina mama. Ukivaa `kimini’ we njoo tu. Hatuna haja ya kuchana nguo ya mtu wala kumwambia anatembea uchi, wakati wasemao hivyo nyoyo zao ziko uchi kuliko yeye.
Hatuangalii kibanzi kwenye jicho la mwenzetu huku tukisahau boriti kwenye macho yetu. Hatuhukumu wala kudanganya. Hatutendi miujiza zaidi ya kukumbusha.
Maana kwetu miujiza ni utapeli wa kawaida. Ni uganga wa kienyeji ambapo mhusika anakuza kuwa anaweza kukutengenezea utajiri wakati yeye ni `kapuku’ huku nao kama vipofu wanauvaa `mkenge’.
Njoo, kwetu uone visivyoonekana na uelewe visivyoeleweka. Pia ifahamike, tunajihubiria bangi na ulevi tu. Hatuhubiri uzinzi wala chuki.
Tunajivutia bangi, mikesha yetu ni ya wote na si watu fulani wenye kutia shaka. Tunapenda sana bangi na gongo kwa vile havifichi unafiki, kama wale wavutao vitu hivi kwa vificho.
Sisi si kama wale wote wanywao kilevi chini ya kivuli cha kiza. Sisi hatunywi kilevi kiitwacho kasumba cha kujiona ni bora kuliko wengine.
Hatuuzi `bwimbwi’ kama wauzaji walioshindikana, wala hatufanyi magendo wala kutorosha wanyama kama wale.
Pia dini yetu haibagui watu kwa rangi wala imani zao. Kwetu walevi wote ni sawa na Mungu wao ni mmoja. Hatuna vigenge wala vishirika vya siri vyenye kulenga kutuneemesha kwa kisingizio cha dini.
Wala hatutoi misaada ya unafiki kwa maskini ambao kimsingi ni matokeo ya hujuma yetu kama wale.
Mwisho, kwenye mihadhara na mikesha yetu tunapiga kelele kidogo na hatuwasumbui watu usiku wala hatukeshi wala kuamshana kwa kelele.
Sisi ni wavuta bangi. Kama nawe ni mvuta bangi na mlevi basi amini niliyoandika hapa. Kama siyo, yadharau.
Blessed be.
Ni mimi Mtakatifu, Nabii, Profwesa, Daktari, Mtukufu, Man and a Half, Nkwazi Mhango, Kwa mfuga Mbwa, Manzese Kanada.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Machi 30, 2013.

No comments: