The Chant of Savant

Wednesday 6 March 2013

Serikali ya Kikwete na 'genocide'


Ingawa natumia neno genocide kwa kusitasita, kama likifafanuliwa vizuri kuwa ni kutekeleza mauaji dhidi ya kundi moja la watu, kinachoendelea Tanzania ni genocide hata kama ni ndogo.
Kwa kumbukumbu ni kwamba tangu rais Jakaya Kikwete aingie madarakani kwa mgongo wa baadhi ya waandishi wa habari nyemelezi, serikali yake imesifika kwa kufumbia au kuwa nyuma ya mauaji ya baadhi ya wanajamii. Rejea mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Mpaka tunaandika watu wapatao 72 wameishapoteza maisha na serikali bado haina jibu juu ya jinsi ya kukomesha genocide hii.
Rejea kuuawa na kuteswa kwa waandishi wa habari. Alianza Daudi Mwangosi (Channel Ten) akafuatia Shaban Matutu (Tanzania Daima). Kabla hata Matutu hajapona wala Mwangosi kuoza amefuatia Absalom Kibanda mhariri mtendaji wa New Habari (2006) Ltd.
Ukiachia watajwa hapo juu, waandishi wa habari wengine wameishapokea vitisho dhidi ya maisha yao. Hawa ni Mbaraka Islam (Raia Mwema), Evarist Chahali (Kulikoni Ughaibuni) na Ansebert Ngurumo (Tanzania Daima).
Mie mwenyewe nimekuwa napokea ujumbe wa vitisho ila kwa vile niko mbali na nimejihami sibabaiki wala kutishika. Nshazoea.
Ukiachia mbali waandishi wa habari ambao walimsaidia Kikwete kuingia madarakani na akawalipa 'fadhila' ya genocide, wengine walioonja joto ya jiwe ya utawala habithi wa Kikwete ni madaktari, walimu hata wananchi wa kawaida. Matukio ya polisi kuuawa raia wema yamekithiri tangu Kikwete aingie madarakani. Ni ajabu kuwa watanzania hawajajua tabia hii chafu na ya kigeugeu ya Kikwete. Ingawa ni mapema kusema ni nani wako nyuma ya mateso na utekaji wa Kibanda, serikali haiwezi kukwepa lawama hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya wahusika wanatajwa kuwa usalama wa taifa ambao umegeuka uhasama wa taifa. Rejea kutajwa kwa Ramadhan Igondhu wa usalama wa taifa  kwenye utekaji na utesaji wa Dk Steven Ulimboka. Je Igondhu na wenzake wamechukuliwa hatua gani zaidi ya kufungia vyombo vya habari vilivyoshupalia jinai hii? Kama hamjui kisa cha kufungiwa gazeti la Mwanahalisi basi jueni ni kufichua cover ya Igondhu na usalama wa taifa wenzake. Kwani siri?
Je Kikwete ataua na kutesa wangapi kabla ya kuondoka madarakani?
Kwa habari zaidi kuhusu kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda BONYEZA HAPA.

No comments: