Japo jamii inatuona kama ‘hamnazo’, tulioishiwa, nasi tuna mawazo. Juzi tulipokuwa tukikamata ‘ulabu’ kwenye baa yetu ya mataptap, mlevi mmoja alituacha vinywa wazi.
Kwa vile nilishawadokeza walevi wenzangu kuwa nimeanzisha chama, na kwamba lazima nigombee ukuu na kuupata, wanapendekeza Bi. Mkubwa wangu, yaani mama kidume wa kidumke, aitwe ‘Raisa’ badala ya ‘first lady’.
Kwanza, wanakataa mke wangu kuitwa first lady wakati siyo. Waliuliza eti wale watoto wangu wakubwa niliwazaa na nani kama yeye ni first lady?
Wakati nikijiandaa kuwaweka sawa, luninga ilinisaidia. Tukiwa ndio tunaanza kukolea si luninga ya ITview, ikaonyesha picha ya Bi Mkubwa.
Yaani mke wa ‘mkulu’, akikagua miradi ya maendeleo kwenye mkoa mmoja wa pembezoni mwa maendeleo unaosifika kwa mambo mengine.
Bila hili wala lile, nilisikia baadhi ya walevi wakisonya, wengine kulalamika kuwa hii kali ya mwaka.
Bi Mkubwa akiwa ametuna kwenye kochi huku wazito wa mkoa ‘wakijimogola’ na kushindana kuonyesha unyenyekevu, ili kulinda ulaji wao.Alionekana kuuhimili ‘uraisa’ bila wasi wasi.
Tukio hilo la kihistoria lilichochea akili za walevi, kiasi cha kuonyesha kuwa kumbe nasi walevi ni `jiniasi’ hata kama jamii haitaki kuliona hili.
Ndiposa mlevi mmoja akatoa wazo, kuwa kwenye Katiba Mpya, tubadili jina la mke wa mkulu. Badala ya kuitwa first lady aitwe ‘raisa’, ili awe na mamlaka kamili kwa vile yupo karibu sana na Rais. Wachina wanaiita hii yin yang.
Wamarekani wanasema kuwa Makamu wa Rais yupo pigo moja la moyo kutoka kwa Rais, wasijue Bi Mkubwa yuko nusu pigo!
Hivyo kwa mantiki hiyo, walevi wanadhani Bi Mkubwa aitwe ‘raisa’ ili kufaidi ‘maulaji’ ya Rais. Je, ninyi wasomaji mwasemaje?
Ndiyo mzee, ndiyo mzee, ndiyo mzee na Bi Mkubwa atukuzwe na kukwezwa!
Tuache utani. Japo mwaweza kudhani walevi ni wachochezi, zingatieni wanaotenda kuliko wanaotafsiri matendo ya watendaji.
Kimsingi, ni ukweli usiopingika kuwa kaya yetu imekuwa kidemokrasia kiasi cha kuanza kuzalisha usawa kati ya `walume’ na wanawake.
Rejea yule mama kipaza sauti (a.k.a) speaker, alivyopewa ukuu wa ‘mjengo’ kwa sifa moja kuu tu yaani kuwa ‘ke. Kama ni hivyo, kwanini na Bi Mkubwa naye asipewe ujiko wake?
Kusema ukweli nilipoanzisha mjadala huu, kila mmoja alichangamka na kuchangamkia mjadala. Walevi walitadhani walikuwa wakiwatetea wake zao wasijue ni wangu na mkulu tu!
Kwa vile walevi nao ni wanakaya tena waheshimiwa kutokana na uwezo wao wa kufikiri zaidi ya wengine na kutoogopa kuelezea wanachoamini, tunaamini pia kuwa wazo letu, litaungwa mkono na wengi kayani.
Ili kuondoa utata na aibu ya bi wakubwa wa wakubwa kuonekana wanadandia ‘maulaji’.
Sababu za kupendekeza Bi Mkubwa wa mkulu aitwe ‘raisa’ ni rahisi. Iwapo mke wa mlevi anaweza kuitwa Mrs Mlevi au Bi Mlevi, kwanini mke wa Rais asiitwe ‘raisa’, mbunge akaitwa ‘mbunga’? Ila iishie hapa. Siyo kesho tusikie mke wa hakimu akiitwa ‘hakima’ au wa jaji, `jaja’. No. ni kwa mkuu mimi na wahishimiwa tu. Timeelewana?
Walevi wanapendekeza Ikulu igawanywe sehemu mbili, yaani ile ya Rais na ya ‘raisa’. Hata kwenye ‘pesamadafu’ kuwe na vichwa viwili yaani cha Rais na cha ‘raisa’. Yatanoga au siyo?
Pia NGO ya Bi Mkubwa isiitwe NGO au kampuni bali chama nambari mbili. Chama cha Rais kiwe nambari wani na cha ‘raisa’ kiitwe nambari mbili.
Wazo hili liliibua mjadala wa hali ya juu. Baadhi ya walevi walionekana kuliunga mkono kwa wingi.
Sababu ya kufanya hivyo, kwa mujibu wa walevi, wangependa Bi Mkubwa wao awe huru kukusanya fedha kutoka kwa wanachama wa chama chake na kwenda nje kihalali, kuomba misaada kama anavyofanya mumewe.
Walevi waliongeza kuwa itaongeza hadhi yake tofauti na sasa ambapo wenye wivu wanampiga mdongo wakihoji anakusanya pesa kama nani?
Mmoja alitoa mpya aliposema kuwa kama hawatabadili mfumo na kumwita Bi Mkubwa, `raisa’ atajinyotoa roho kupinga udhalilishaji anaofanyiwa Bi Mkubwa.
Mwingine alisema kuwa kama hawatabadilisha Katiba na kumpa cheo cha ‘raisa’ kwa Bi Mkubwa, basi wanaomtuhumu kukusanya fedha kwa wafadhili bila mamlaka wakidai anatumia atakavyo kwa mambo ya binafsi wahukumiwe kunyongwa.
Kwa maana, wanachofanya ni uasi ambao kisheria adhabu yake ni moja, mnaijua.
Wakati mwingine, walevi huwa wana vituko. Unaweza kuamini kuwa wakati walevi wote wakipigania ulaji wa Bi Mkubwa wetu, yupo mmoja aliyeonyesha kuathiriwa na ‘mibangi’ aliyokuwa amevuta siku hiyo.
Yeye, tena bila aibu, alisema eti hakuna haja ya Bi Mkubwa kupewa `ulaji’ kisheria iwapo `ulaji’ huo unaweza kupatikana kinyume cha sheria.
Kigezo alichotumia ni kuwa hata sisi walevi, tunafaidi gongo, mataputapu na bangi kinyume cha sheria. Alisema eti kama kuna wafadhili wanaotaka maendeleo kwa watu wetu basi watoe michango yao kwa mawaziri husika.
Aliposema hivyo, kila mmoja alisonya. Mmoja wetu alimtolea uvivu kwa kumwambia kuwa, mawaziri watafuja ile fedha kama ambayo taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali amekuwa akifichua.
Kabla ya kuendelea, si mlevi mwingine akatoa mpya eti ni heri kwa wizara hata kama zinaiba, zinakaguliwa na mkaguzi ingawa hazidhibiti.
Je, Bi Mkubwa yeye anakaguliwa na nani zaidi ya kuhomola? Hili swali lilituacha hoi. Kwani lilitusuta na kutustua. Je nyinyi mwasemaje?
Kwa vile sijachaguliwa kuwa Rais, haya mawazo ya kilevi hayana sababu ya kukuhangaisha. Hata kama yana ujumbe mzito na maana kwa wengine, mambo ya Ngwose muachie mwenyewe.
Muhimu ni kutafakari na kujifunza. Je, mnakubaliana nami kumuita mke wangu ‘raisa’ au mtanirushia `mimawe’ kwa vile mnadhani ninazidi kuwazidi akili?
Kalagabaho! Acha nikitoe kabla ya walevi na wavuta bangi kuanza kunirushia `michupa’ na vipisi.
Naona yule njiwa jike naye anajishaua, eti kwa vile dume lake ni kuu la njiwa nyumbani kwangu.
Anasahau kuwa yeye ni mfugo! Ukome na ukomae!
Chanzo: Nipashe Jumamosi 9, 2013.
No comments:
Post a Comment