How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 23 March 2013

Tubinafsishe `geshi’ la ‘polish’ FBI

Juzi tulikunywa ‘gongo’ kwa wasi wasi sana. Si alikuja ‘fyatu’ mmoja akatwambia eti Federal Burea of Intelligence (FBI) walikuwa mtaani wakitafuta wanaoua mashehe, mapadre na walevi.

Si hatukujua kuwa, kumbe alimaanisha walevi wa dini na si gongo! Aliongeza eti walikuwa wamemiminwa ile mbaya!

Tukiwa tunatafakari tukidhani ni utani, si akapita `mtasha’ akifukuzia `vichangu’ pale mtaani.

Bwani we! Muuza gongo alijikuta ameachwa na walevi tena bila kulipa. Kusema ukweli wengi hawakukimbia kumuogopa FBI, bali kulipa `njuluku’. Si unajua waswahili wakipata kisingizio.
Baada ya `zali’ kumalizika, nilianza kutafakari kutoa pendekezo kwa kituo cha uwekezaji na uchukuaji kayani kiitwacho Tanzia Investment Centre.

Sababu ambazo zimenisukuma kutaka `geshi’ la `polish’ libinafsishwe ni kama ifuatavyo:

Kwanza, `geshi’ lenyewe halina `polish’, wala gesi vya kutosha kufanya kazi. Haling’ali tena wala kufaa. Limeishiwa `polish’ na gesi ya kukimbizana na wahalifu wadogo wadogo, huku likiwagwaya wakubwa.

Limeharibika na kuchafuka sina mfano. Ukiondoa wingi wa `mabobish’, `kash kash’ na `mishemishe’ za kusaka kitu kidogo na kitu kikubwa, `geshi’ letu halina hata heshi…. malizia.

Kama lina lolote la maana si jingine bali `ufyosi’ na force. Mara utasikia ‘rire jamaa razima niriaresti.’

Ajabu jamaa `hiro hiro rikirikatia kiu’, sorry, kitu kidogo, linalegea na kuliachia! Hatutaki maneno bali vitendo. Amkeni mpambane na mabaya badala ya kuyashiriki.

Pili, limeshindwa kuwashughulikia `mafwisadi’. Huwa wanawakatia kitu kidogo au woga na kujigonga tu?

Mbona huko nyuma hamkuwa hivyo? Naona yule `ndata’ anasonya na kukamia. Hunipati.

Foka, sonya, hata ujinyotoe roho ili ufe na uroho na roho mbaya vyako hunipati aku! Huo ndiyo ukweli.

Badala wamkamate, wao wawalinda. Kama hawawalindi wamekamata nani? Hebu fikiria akina `kagodamn’ na majambazi wengine wanavyoendelea `kupeta’.

Tungekuwa na `geshi’ la `polish’ lenye akili lingeshindwa angalau kuwanyima raha?

Tatu, limeshindwa kuwanyaka wanaonyotoa roho za mazeruzeru hadi kulazimika kuita FBI. Watu wanaitwa `dili’ wakiuawa huku nao `polish’ wakihangaikia `madili’ kama si kufanya hilo kuwa `dili’ la kuingizia uchache.

Hayo kweli ndiyo maisha bora kwa wote? Hawa wanauawa wengine wanafaidi! Kuna jamaa aliniacha hoi aliposikia kuwa FBI wapo kayani kuchunguza mauaji ya kasisi na shehe kule Zenj.

Aliuliza mbona wanapouawa mazeruzeru tena kwa makumi, hao FBI hawaletwi? Je, akiuawa mheshimiwa au waziri si wataletwa NASA?

Kwa vile juzi rafiki yangu Absally Kibanda alicharangwa mapanga, kung’olewa kucha na kuharibwa jicho, nangoja kusikia kama wataleta hao KGB.
Hakuna sehemu ‘geshi’ limeonyesha umahiri kama kubambikizia watu kesi na kuwamiminia risasi akina Mwangoshi.

Kwenye mchezo wa kutumia bunduki kizembe lol! Hapa mwao japo si wote. Wengi wanashangaa, kwanini huyo `dingi’ wake bado analipwa wakati `geshi’ lake limeishiwa gesi na `polish’ ya kufanya watakavyo walevi!

Kuna jamaa aliniibia siri kuwa jamaa na mkulu wana uhusiano wa kindoa. Don’t quote me please hata kama kuna ukweli.

Sita, kukamatwa kwa baadhi ya `ndata’ wakishirikiana na `majambi wazi’. Litamkamata nani iwapo baadhi ya `majambi wazi’ ni `polishi’ wenyewe?

Litamkamata nani iwapo nalo linapaswa kukamatwa? Litamshitaki nani wakati nalo linapaswa kushitakiwa kwa kuishiwa gesi?
Nakumbuka jinsi walivyoingilia kwenye zoezi la kuzuia wizi mitaa ya Kariakoo wakaishia kuondoka na `uchache’. Bado hapa hatujagusia ule wizi wa mishahara kule Msimbazi `polishi steisheni.’

Kwa vile chini ya dhana ya uwekezaji na ubinafsishaji, kampuni au taasisi inayoleta hasara inapigwa mnada, basi na `geshi’ letu tulipige mnada.

Mwekezaji awe FBI. Hakuna kitu nina usongo nacho kama `viribatumbo’ vya `ndata’. Nataka niwaone watakavyoanza kupwaya baada ya kubinafsishwa.

Nataka niwaone wakilipa nauli kwenye ngwala ngwala wanazopanda `dezo’ utadhani wanafanya kazi dezo.

Laiti `viribatumbo’ vingekuwa vinabinafsishwa, hata kama ni hasara tupu, ningewania lau nami nionekane nimeula na nina `njuluku’, hivyo ni kizito mwenye kuweza kuvutia `totoz’ na `dili’.

Ningenunua `kiribatumbo’ hata kama ni ugonjwa ili niwatishie watu kwa kuwauliza ‘unajua mimi ni nani?’

Wee si nyani tu. Najua walevi wengi wangejibu. Au vipi? Ukisoma hii kitu soma kimya kimya. Maana Bi Mkubwa akiinyaka jua nitaaibika.

Mezea mshirika basi. Siyo utoke hapa uende kunichoma. Nitatoa pendekezo kwa FBI kama itakubali kulinunua iwapeleke `ndata’ wetu Kandahari ili wakawanyotoea roho watalebani vizuri.

Maana wao kwa kupiga watu risasi hawana mfano. Pia wanafaa kwenda kule ili wapate mshiko wa kutosha kutokana na ukweli kuwa watu wengi huko ni matajiri kutokana na kuuza `bwimbwi’.

Badala ya kuhangaika kutukamata sisi wanywa gongo, waende huko wakamalizane. Kama kweli wao ni `walume’, kwanini watunyake sisi `wabwia bwimbwi’ wakati wakila na wauzaji?

Kama mnadhani nazusha, jiulize ni kwanini biashara ya `bwimbwi’ inazidi kushamiri? Kwani hatujui kuwa kuna watu tena pale `eyapoti’ ya International ya Mwalimu Mchonga, wanaopewa chao na kuruhusu `mibwimbwi’ ipite na kuingia kayani ili itumalize na wao watajirike?

Tena nasikia kuna na madingi wakubwa tu nao wanaingiza `mibwimbwi’. Ukiachia mbali `geshi’ la `polish’, napendekeza hata Takokuru iwekezwe kwa Wachina ili wanyonge mafisadi, uhasama wa taifa tuwape warusi.

Tume ya uchakachuaji na uchafuzi uitwao uchaguzi wapewe Wakenya. Hata baadhi ya wakubwa wa `geshi’ wabinafsishwe haraka.
Ingawa juzi Bwana Nchimvi alijitutumua kwa kuwasimamisha kazi baadhi ya `ndata’ wanaoshirikiana na majambazi, kuiba nyara za umma hata kuwatoza kitu kidogo na kikubwa makuruta, ukweli ni kwamba bila kufumua `geshi’ lote au kulibinafsisha mchezo utakuwa ule ule.

Ufwisadi na ujambazi wa kimfumo. You know what. If I were to advise Mr Prezzo, I’d strongly recommend that we jail all of our current dudes and recruit new ones after grilling them.

Loo! Bangi na gongo vikichanganyika hatari. Huwa vinanifanya niongee Kikameruni kama sina akili nzuri.

Hata hivyo acha nijisifu japo kidogo. Mwenzenu nimepiga shule bwana. Naongea `ung’eng’e’ ambao hata `kamuzi’ za dictionary hazina!

Hayo tuyaache. Naona yule anasonya. Kwani kujisifu vibaya? Mbona wakubwa zenu wanajisifu kwa kila upuuzi na hamsonyi wala kuwakamatisha adabu?

Niache nijisifu kwa vile hamtaki kunisifu zaidi ya kunitumia watu waninyotoe roho kwa kuwapa vipande vyenu. Hata mkituua mjue nanyi kuna siku mtakufa tena vifo vibaya.

Chanzo: Nipashe Jumamosi Machi 23, 2013. 

No comments: