Taifa letu, kwa sasa, ni maarufu dunia kutokana na tabia mbaya.
Hakuna ubishi kuwa kwa sasa Tanzania inasomeka sana kwenye vyombo vya habari vya
kimataifa kutokana na uchafu wake. Hivi karibuni kulikuwa na umaarufu wenye
harufu mbaya utokanao na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Baada ya kadhia ya mauaji ya kishenzi, kinyama na kishirikiana na
watu wenye ulemavu wa ngozi yanayofanywa na watu wenye imani chafu na tamaa
utajiri, wanaofuatia ni waandishi wa habari.
Mwaka jana mwandishi Daudi Mwangosi alipigwa risasi na kuuawa na
polisi jambo ambalo lilifanya taifa letu kujulikana kwa tabia hii chafu kwenye
vyombo vya kimataifa vya habari na vya kutetea haki za binadamu.
Hata
kabla ya vumbi kutua, mwandishi mwingine wa habari Shaban Matutu wa Tanzania
Daima alipigwa risasi na polisi akiwa nyumbani kwake. Hadi sasa haijulikani
wahusika ambao wanafahamika walichukuliwa hatua gani.
Hivi
karibuni mwandishi mwanadamizi Absalom Kibanda, mhariri mtendaji wa New Habari
(2006) alitekwa akiwa anashuka nyumbani kwake. Kibanda alipigwa
sana, kung’olewa meno na kucha kiasi cha kukimbizwa nchini Afrika Kusini kwa
matibabu.
Kwa
wanofatilia matukio haya kwa undani, watakubaliana nasi kuwa kinachojibainisha
ni dalili za mfumo fisadi na wa kimafia unaoanza kujengeka nchini. Si uvumi,
waandishi wa habari wanalengwa na makundi ya watu hata taasisi yanayowaona kama
tishio la maslahi yao ya kijinai. Waandishi mahiri wanaofichua uchafu unaotendwa
na wakubwa wamekuwa wakaitishiwa maisha na hata kuumizwa na hakuna
kinachofanyika. Je namna hii tunalipeleka taifa wapi kama si kuligeuza kaburi la
waandishi wa habari? Je nchi na serikali vinaweza kuwapo na kuendesha shughuli
zake bila waandishi wa habari?
Nchi
zilizoendelea zinajua umuhimu wa waandishi wa habari. Ndiyo maana tasnia ya
habari huitwa fourth estate yaani mhimili wa nne wa dola baada ya Utawala, Bunge
na Mahakama. Inashangaza kuona watumishi wa mihimili mingine wakilindwa na
kuheshimiwa huku waandishi wa habari wakiendelea kuishi kwa wasi wasi.
Inasikitisha kuona hata mamlaka zinazojigamba kuwapo kwa ajili yakulinda raia na
mali zake hazichukui hatua.
Umefika wakati wa waandishi wa habari kuanza kumsaka mbaya wao na
kumfichua bila woga wala ajizi. Inasikitisha kuona waandishi wa habari
wakitolewa kafara na manyang’au wanaolihujumu na kuliibia taifa kwa kutumia
madaraka waliyopewa na umma.
Ifikie mahali waandish tukatae udhalili na utumwa huu.
Japo wanandishi wa habari nchini hawezi kuwa kitu kimoja kutokana na
kuzuka aina fulani la waandishi nyemelezi ambao hutumiwa kama nepi na wakubwa
kuficha uchafu wao, waandishi makini na safi tushikamane tupamane
na mfumo huu zandiki. Tusiendelee kugeuzwa mabunga kwa kuhadaiwa na tume za
uongo na ukweli zinazoundwa pale wenzetu wanapouawa au kuumizwa kama iliyotokea
kwa Kibanda. Pia tusiridhike na salamu na pole za wakubwa yanapotupata. Salamu
si muhimu kama kutafuta suluhu na kujenga mazingira ya uwajibikaji haki na
usawa.
Tunafahamu fika kuwa adui mkubwa wa waandishi wa habari ni waandishi
wa habari wanaotumia matumbo yao kufikiri badala ya vichwa. Ni waandishi
waliojigeuza nepi za wakubwa ambao wako tayari kuficha na kufumbia macho uoza
ilmradi wanakatiwa kitu kidogo au kupewa vyeo vya uongo na ukweli kwa wale
wanaotumikia taasisi au watu wachafu. Je waandishi wote wa habari tutajiruhusu
kusaliti taaluma na maadili yake ili kupewa makombo na kuyafakamia kama
wafanyavyo waandishi nyemelezi au makanjanja?
Umefika wakati wa waandishi wa kweli kusimama kidete na kuibana
serikali ili ituhakikishie usalama na kufanya kazi bila vitisho wala bughudha
sawa na wanajamii wengine.
Ninapoandika makala hii nafahamu waandishi wa habari tena nguli
wanaoishi kwa shinikizo na hofu baada ya kupokea vitisho toka kwa mafisadi
wanaowaona kama tishio la shughuli zao haramu za kulihujumu na kulizamisha
taifa.
Nimewahi kupokea malalamiko toka kwa waandishi Ansbert Ngurumo,
Mbaraka Islam, George Maziku na Evarist Chahali ambao wamekuwa wakipokea vitisho
na wakati mwingine kuvipuuzia. Kwa lililomfika Kibanda, nawashauri waandishi
ambao wamekuwa wakitishiwa maisha wachukue hatua hata kama itabidi kuondoka
Tanzania kwa wale walioko huko. Maana inavyoonekana, serikali na taasisi zake
hawako tayari kuwahakikishia usalama.
Ingawa magenge yanayoendesha hujuma dhidi ya waandishi yanaweza
kushinda kwa kipindi fulani, hayatashinda milele. Je wataua wangapi? Nadhani
dawa si kuua waandishi bali kuacha kutenda jinai dhidi ya taifa. Waandishi wengi
hasa niliowataja hapo juu wanachukiwa si kwa sababu ya kumuonea wala kumhujumu
mtu. Wanachukiwa, ima kwa kukataa kuwekwa mifukoni mwa mafisadi, au kuandika
vitu vinavyowaudhi watawala na mafisadi. Tanzania ni nchi yetu kwa sawa. Ni mali
yetu sote kuanzia rais hadi msukuma mkokoteni. Hivyo, hakuna mtu mwenye mamlaka
wala haki kumtoa roho mwenzie kwa kulinda uchafu wake. Kwangu mimi
kinachoendelea ni kichocheo cha kuwa mkali zaidi bila kujali matokeo.
Kinachonisaidia tofauti na wengine ni kwamba niko mbali na makundi haya ya
kiharamia.
Kwa
wale walioko ndani ya nchi, hakikisheni mnapiga kelele na kusikika ingawa
kuna gharama ya kufanya hivyo. Tanzania imefanikiwa kuwa na genge
la wahalifu lisiloguswa na vyombo vya habari kwa sababu ya kutokuwa na Gutter
Press. Magazeti haya fichi husaidia kufichua kashfa zenye kuwa
tishio kwa waandishi wa habari kwa vile hayataji majina ya waandishi wala hayana
ofisi maalumu na anayeyamilki huwa hajulikani. Kwa waliosoma chuo kikuu cha Dar
es salaam watanakumbuka Punch. Mr Punch alikuwa anaogopewa na kila fisadi chuoni
kwa kujua kuwa atamfichua na kutoa uoza wake bila ya mtoa taarifa kujulikana.
Wenzetu Kenya wanayo Gutter Press ambayo hufichua maovu mengi ambayo magazeti ya
kawaida huogopa kuandika kwa sababu za kisheria na kiusalama. Hufikia mahali
vyombo vya habari vikapata fununu hata stori kama hizo na kuzirusha kwa Gutter
Press ambayo huuzwa kwa bei nafuu kwenye vituo vya mabasi hata baa bila
kubughudhiwa. Serikali zinazowajibika na kuchukia uoza huacha Gutter Presses
zifanye kazi bila kuziingilia. Sasa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwa na
nyenzo hii ili kuendeleza mapambano dhidi ya ufisadi.
Chonde chonde, tusiigeuze Tanzania kaburi la waandishi wa habari.
Hawa ni wajumbe tu wasiopaswa kutishwa kudhiriwa wala kuuawa. Wao ni sauti ya
wasio na sauti na sauti ya umma isiyopaswa kuchukiwa wala
kunyamazishwa.
Chanzo: Dira Machi, 2013.
No comments:
Post a Comment