Juzi nilicheka hadi nikapaliwa na ulabu. Kama sio kuwahishiwa maji, huenda
ningelazwa.
Kwa vile si mtu wa kuibiwa mchana, sikwenda hospitali
kuishia kulipa ‘fweza’ za kumuona daktari ambaye angeniandikia dawa na kuniagiza
nikanunue kwenye ‘famasi’ yake.
Wajua nini? Hakuna kitu kilichonivunja
mbavu kama majibu ya baadhi ya watahiniwa wa form fail.
Nasikia badala
ya watahiniwa kujibu maswali ya mtihani, waliamua kuonyesha vimbwanga vyao hasa
chuki kwa waheshimiwa na usongo wao katika mapenzi.
Japo wengi waliona
hili kama jambo la ajabu, walishindwa kuelewa kuwa haya yote yanasababishwa na
kaya yetu kuwa ya siasa na mapenzi.
Ukisikiliza miziki inayochezwa
kwenye radio zinazoendeshwa na watangazaji mabambataa, utagundua kuwa hupenda
kucheza nyimbo za mapenzi tena X ndicho chanzo.
Sasa mnategemea nini?
Sababu nyingine ni ile hali ya `wadanganyika’ kuabudia `ustaa uchwara’ na
usanii.
Baada ya mkulu `kuwashobokea mastaa’ hasa alipokwenda kumzika
mwenzao mmoja, kila kitu kilibadilika, wasijue jamaa alikuwa akikwepa joto la
migomo. Hayo tuyaache.
Kimsingi, mambo yasiporekebishwa hasa kumtimua
kazi waziri mhusika aitwaye Doc Thanks Kawambwa, mambo yatazidi kuharibika.
Natabiri kuwa kwenye majibu ya mwaka ujao, watahiniwa wanaweza kuonyesha
hata video za ngono kama majibu.
Wakati vitegemezi vyenu vinavyosoma
`uswekeni’ vinaotea bongofleva na mapenzi, vigegemezi vyetu vinavyosoma ‘majuu’
vinaota kurithi ukubwa wetu.
Usishangae ya Ndalichako kusema eti
vitegemezi vya wachovu viliandika mistari ya love.
Kitegemezi changu
kilichosoma huko kwa Mama kiliandika kwenye mtihani, once I am done hither, I
become a ruler like my dad and mam. Waulize akina Jan Makamba au Hossein Mwinyi
watakwambia.
Watoto wa wakubwa hawali ‘bwimbwi’ wala kuiba kuku, bali
‘midola’.
Ila wachovu wakitaka watoto wao wawe wanasiasa, hawana haja ya
kuwapeleka nje hata Uganda au Kenya.
Hebu, mfano, angalia hiki
kitegemezi kilivyowashukia jamaa wa ‘mjengoni’.
“Unakuta mwanafunzi
anaeleza anavyolishangaa Bunge… mtu anaandika… nawashangaa wabunge, wamekaa kama
wapo kijiweni…”
“Wabunge wamekosa ustaarabu, badala kujadili kero za
wananchi waliowachagua, wanapokea timu zilizoshinda makombe… timu ikishinda
Kombe la Kagame inapokelewa bungeni…”
“Bunge limekuwa kama kijiwe,
bungeni siyo ukumbi wa starehe, kama mnataka kupokea timu hizo nendeni katika
ofisi zao au viwanjani.”
Je, unaweza kusema kuwa hicho ‘kitoto’
hakina elimu? Sema, hakina cheti ila kina elimu kuliko waheshimiwa.
Hiki
kitegemezi ‘noma’ kweli kweli. Kumbe kinajua kuwa sheria mbovu wanazopitisha
wahishimiwa ‘mjengoni’ ndizo chanzo cha maangamizi yake! Good kid, good job!
Japo wengi wasiojua falsafa ya elimu watawalaumu vitegemezi vyao kwa
kuandika vitu vya ajabu.
Mlitaka waandike nini iwapo kila uchao
mnawahubiria maloveydovey? Nadhani vitegemezi vyenu vimeonyesha umahili wa
kusoma magazeti ya uchafu na kuangalia luninga kwa sana.
Mnapopanda
ngono na ufisadi mnategemea mvune elimu? Mnapopanda ‘mitusi’ tena ‘mjengoni’
mnategemea nini?
Waulize akina Jobless Nduguy. Aliposema kuwa mwenzake
kazoea kuchamba sana au Nahoda aliyemwambia mwenzake kuwa hatumii akili, ana
tofauti gani na yule aliyesema kuwa waheshimiwa wanatumia masaburi kufikiri
badala ya vichwa?
Nadhani wakati muafaka umetimu kuwashauri waheshimiwa
wakae ‘mjengoni’ na kutunga sheria itayolazimisha kila mzazi kupeleka kitegemezi
chake kusoma nje.
Kama wakubwa wanatibiwa India, kwa nini vitegemezi
vitibiwe ujinga wao nje? Mie napendekeza vipelekwe Syria ili vijifunze kupambana
na kukomboa kaya yao.
Vingine vipelekwe Afghanistan ili vijifunze jinsi
ya kupambana na ugaidi wa kidini kama ule uliotokea Zenj ambapo kasisi mmoja
alinyotolewa roho.
Watahini wanalalamika kuwa wamepewa majibu ya urongo.
Hivi walitegemea nini kama waheshimiwa wanapewa majibu ya uongo na mawaziri na
hakuna kinachofanyika?
Walitegemea nini iwapo ujambazi unaoitwa twisheni
umehalalishwa? Hivi mlitegemea waogope kutoa majibu ya uongo kwa vile wanaogopa
kufeli?
Siku hizi hakuna anayeogopa kufeli. Unafeli darasani na kwenda
mtaani na kununua cheti na shahada na kuendelea kupeta. Anayedhani namdanganya
akawaulize wale mawaziri waliotuhumiwa kughushi shahada.
Si wanaendelea
kupeta na kupetuka tena kwa pesa ya mlipa kodi kapuku. Sasa Mungu awape nini
zaidi ya ulaji huu wa ‘dezo’ na laini?
Ukifeli darasani huna haja ya
kuhofu. Kama hutaki kununua shahada basi unaanzisha mradi wako wa kuuza bwimbwi
kama si kuimba mistari na kuukata.
Ukiona haya huyapendi, unaanzisha
kampuni ya kushindanisha ma-miss vichochoroni na kupata ‘mshiko.’
Juzi
mlevi mwenzangu alituacha hoi. Alisema mwanae alilalamikia maswali ya mitihani.
Alisema kuwa mwanae alipoulizwa swali la: Define the law of floatation
alijibu simpo kuwa you sniff cocaine and start floating.
Hii maana
yake ni kwamba tubadili mitaala. Badala ya kuwauliza vitu kama Newton’s laws of
motion waulize Adam’s and Eve’s secrets and the fruit they ate.
Tupige
marufuku ma-novels kama Things Fall Apart, The River Between, No longer at ease
na mengineyo ili yasiwaumize vichwa watoto wetu.
Tufundishe elimu yetu
kwa Kiswahili kwa sababu soon kitakuwa lugha ya dunia. Mambo sonic subsonic and
supersonic tuwaachie wenyewe tuwe watazamaji au vipi?
Badala ya
kuwasumbua na kukariri `matabu’ kama history of the time- Stephen Hawking
waulize maswali toka kwenye magazeti ya udaku muone watakavyotoka na flying
colours kama siyo cum laude.
Ningekuwa mwalimu ningeuliza maswali kama:
What do people do in short-time guest houses? What are the effects of barning
marijuana and the effects of legalizing impunity?
Mlevi mwingine
alituacha hoi aliposema kitegemezi chake kilipoulizwa kuelezea maana ya siasa
kilijibu kuwa:
Siasa ni mfumo wa uongo na usanii unaomwezesha mtu
kuukata haraka na kuitwa mheshimiwa hata kama anayofanya hayastahili heshima.
Nasikia eti mwenzie alipotakiwa afafanue maana ya uhuru, alisema eti
uhuru ni hali ya kila mtu kufanya ufisadi na usanii atakavyo bila kuvunja
sheria.
Tumalizie kwa kuwapongeza vitegemezi vyetu kwa kutufungua
macho. Ingawa wengi wanavilaani, kimsingi majibu yake yanatoa jibu la tatizo
kuwa tusomeshe watoto nje au tubadili mitaala.
Badala ya kuwekeza sana
kwenye grossaries, short-time guest houses na siasa za kibabaishaji, tuwekeze
katika elimu. Simpo. Anyways, napita tu.
Chanzo: Nipashe Jumamosi Machi 2, 2013.
No comments:
Post a Comment