Friday, 16 January 2015

IPTL "kupunguza" bei ya umeme huruma hadaa?


Baada ya kampuni ya kuzalisha umeme yenye utata ya International Power Tanzania Limited (IPTL) kukumbwa na kashfa ya kuiba mabilioni ya fedha za wananchi kwenye fuko la escrow, imekuja na mbinu nyingine ambayo yaweza kuwa ya kitoto kama tutakuwa makini. Imetoa taarifa kuwa itapunguza bei ya umeme kwa 20% tokana na kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la kimtaifa. Hii hatua imefikiwa baada ya IPTL kusababisha ulanguzi na mgao wa umeme kwa miaka mingi tu. Wengi wanajiuliza; Kwanini sasa ambapo maji yako shingoni? Je huyu anayejigamba kufanya hivyo ni mmilki halali wa IPTL? Je kuna wakubwa nyuma ya kampeni hii chafu?
Hatua hii, japo yaweza kuonekana njema, inazua maswali mengi. Kwanini sasa ambapo kampuni inakabiliwa na kashfa nyingi miongoni ikiwa ni kutaka kuongezewa muda tofauti na makubaliano ya awali, kudanganya kiasi cha fedha ya mtaji wake ambapo tunaambiwa waliwekeza shs. 50,000 badala ya Dola za Marekani 36 milioni wakawa wanalipwa capacity charges kwa mabilioni ya shilingi na kuliibia taifa? Rejea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha za serikali iliyosema, “Mgogoro uliopo hivi sasa kati ya Tanesco na IPTL unahusu kiwango cha malipo ya uwekezaji yaani capacity charges ambacho IPTL walikuwa wanalipwa na Tanesco. Kwa mujibu wa mkataba huo, capacity charge inapaswa kukokotolewa kwa kuzingatia mtaji wa asilimia 30 na mkopo wa asilimia 22.31.” Kama kanuni hii ingefuatwa, IPTL walipaswa kulipwa si zaidi ya shs 7,000.  Walichofanya IPTL licha ya kuwa jinai ni utapeli, wizi na uongo wa kutupwa. Je unategemea huruma na ukweli toka kwa watu kama hawa? Hata hiyo aslimia 20 wanayodai kutaka kupunguza walishajilipa kwa wizi wa miaka 20. Hakuna siku hata moja chui atamwonea huruma mbuzi hata ashibe kiasi gani. Sana sana atakachofanya ni kumuua na kumweka ima kiporo hata kumuharibu ili mradi lake litimie.
Je bei ya mafuta kwenye soko la dunia imeshuka kwa asilimia 20 tu au zaidi. Kwa mujibu wa kampuni ya New York Mercantile Exchange (NYMEX) inayoshughulika na biashara ya mafuta, mafuta ghafi (crude oil) hadi terehe mwezi Januari ilikuwa imeporomoka kutoka takriban $90 kwa pipa hadi $46. Hii ni zaidi ni sawa na aslimia 54. Kwanini sasa IPTL ipunguze bei ya umeme kwa asilimia 20 na si 40 na ushei? Mbona IPTL ilituibia matrilioni kwa miaka mingi kwa kudanganya capacity charge na leo ijifanye inawajali watanzania kama siyo kutaka kuwazuga waione inawajali wakati imekuwa ikiwaibia kwa muda mrefu? Je watanzania watakuwa wajinga waingie mkenge huu? Je hii ni janja ya kutaka kuiwezesha serikali ambayo imeonekana wazi kushirikiana na IPTL kuendelea na biashara tofauti na mapendekezo ya Bunge kuwa serikali basi inunue mitambo ya IPTL kuepusha kuendelea kuibiwa? Kwani lazima IPTL? Kwanini Tanesco wasinunue mitambo yao na kuendelea kutoa umeme badala ya kulanguliwa na kuibiwa na mafisadi hawa? Je wanataka kutuziba macho tuwahalalishe na kusahau escrow? Kwanini IPTL inaonyesha “ukarimu” baada ya kukaribia kuisha mkataba wake uliosainiwa mwaka 1995 na kupaswa kumalizika mwaka 2015 kama siyo gea ya kutaka kuendelea kutuibia?
Ingawa serikali imeshikwa na kigugumizi kuhusiana na kutekeleza mapendekezo ya Bunge, Tanzania kwa sasa ina uwezo na kila sababu ya kuachana na kutumia umeme wa ulanguzi wa IPTL unaozalishwa kwa kuchafua mazingira tokana na kutumia mafuta badala ya gesi ambayo tunayo kwa wingi sasa. Je tatizo ni nini? Ni ile hali kuwa gesi haitatoa ten percent ya wakubwa?  Kwa vile tuna gezi, hivyo, tuwekeze kwenye mitambo ya gesi na kama ni kuzalisha umeme au waje wawekezaji wengine ambao hawajatuibia chini ya makubaliano mapya baada ya kuumizwa na IPTL kwa miongo miwili.
Inashangaza sana kuona wale waliotuibia kwa miaka mingi eti leo wawe na huruma nasi. Wamepata lini hii huruma na udhu wa kutujali umeanza lini wakati kwa miaka yote wametulangua, kutuibia na kutuchuuza? Hapa lazima kuna namna si bure. Kwa vile watanzania licha ya kuwa wenye serikali ndiyo wateja wakubwa wa umeme, kuna haja ya kugomea huruma hii inayolenga kutuumiza zaidi. Kuna haja ya kugomea huduma za IPTL ambazo hazina faida kwa taifa. Na lazima tuhoji ni kwanini serikali inaendelea kulala kitanda kimoja na IPTL. Rejea serikali kushindwa hata kuwawajibisha na kuwachunguza watuhumiwa wa wizi wa escrow. Rejea serikali kuendelea kukaa kimya bila kutekeleza maazimio ya bunge. Hii ni dharau kwa bunge na watanzania wote waliokasimu madaraka yao kwa wabunge wao walioamua kushughulikia kadhia ya IPTL. Imefikia mahali IPTL inaonekana kama serikali ndani ya serikali. Je ni kwanini serikali hailioni hili na kuona aibu inayopata hadi wafadhili wake wanaamua kuondoa fedha yao? Je watanzania watapata faida gani tokana na ushirika wa serikali na IPTL na msimamo wake wa kugoma kushughulikia wezi wa escrow?
Ni jambo la hatari kwa taifa kuishi kwa kutegemea hisani hata ya mafisadi na wezi wanaoibia umma kila uchao. Wengi wanashangaa huyu Harbinder Sethi Singh aliyetangaza kushusha bei ya umeme wakati hata umilki wake wa IPTL ni utata mtupu. Je anataka kutumia hadaa hii kuhalalisha umilki wa IPTL kama walivyofanya wamilki wa sasa wa UDA? Je tutaendelea kuwa shamba la bibi wakati tukijiwa wazi IPTL imekuwa ikituibia?
Tumalizie kwa kuwataka watanzania waamke na kuachana na kugeuzwa mbuzi wa shughuli au shamba la bibi ambapo kila mwizi huja na kuiba atakavyo huku akijifanya anawasaidia. Hatuhitaji huruma ya hivi bali haki ambayo ni kuachana na IPTL kama ilivyopendekezwa na Bunge. Bila kufanya hivyo, licha ya taifa kuendelea kudhoofika kiuchumi basi tuwawajibishe watawala wasiotaka kuliona hili.
Chanzo: Dira. 

No comments: