The Chant of Savant

Tuesday 13 January 2015

Amani itaondolewa na ufisadi na si mataifa ya magharibi

Baada ya wimbi la ufisadi kutikisa taifa letu, kumeanza kujitokeza dalili za woga miongoni mwetu. Hii ni baada ya kuwepo manung’uniko mengi toka kwa wananchi wanaoona kama mambo yanakwenda ndiyo siyo. Rejea mfano, vijana toka Geita walioamua kutembea kilometa yapata 1,000 kwenda ikulu kumwambia rais awawajibishe watuhumiwa wa ufisadi ikiwa ni pamoja na kumtaka apambane na ufisadi kwa vitendo. Japo polisi walifanikiwa kuwazuia vijana hawa bila kosa lolote, ukweli ni kwamba hali ya taifa letu si nzuri.
Baada ya nyufa, tena nyingi, kujitokeza, wapo walioanza kutafuta jinsi ya kupata adui wa kumtupia lawama. Mmojawapo wa walioonyesha wasi wasi huu dhahiri ni shehe muu Issa Shabaan Simba aliyekaririwa akizituhumu nchi za magharibi wakati akihutubia mkesha wa Maulid ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Mazoezi, Korogwe. Shehe mkuu aliwaasa watanzania kuwa makini na uchonganishi wa nchi za magharibi akidai zinafanya hivyo ili ziweze kuuza silaha.
Ni bahati mbaya kuwa shehe mkuu hakutoa mifano ya nchi ambako nchi hizi zimefanya hivyo na lini zimeanza kufanya hivyo. Japo ni kweli kuna baadhi ya nchi za kiafrika zimegeuzwa soko la silaha na wizi wa raslimali zake kama DRC, hali kwa Tanzania ni tofauti. Tanzania hakuna cha uchonganishi wala nini zaidi ya uongozi mbovu na ufisadi. Hata hivyo, wanaodhani kuwa amani inaweza kutoweka tokana na uchonganishi wanashindwa kuona ukweli wa kadhia hii. Kwa mfano, huwezi kudai eti nchi za magharibi zinatuchonganisha kana kwamba sisi ni taifa la mataahira wanaoweza kuambiwa gombaneni bila sababu tukafanya hivyo. Hii haingii akilini hata kidogo.
 Nadhani kama tutagombana si kwa sababu ya kuchonganishwa bali kuchoshwa na mfumo wa kujihudumia ambapo wachache wanawatumia wengi kujineemesha wakati wengi wakiendelea kuwa maskini bila sababu ya msingi. Nchi yetu ina raslimali ambazo zinachezewa na watawala wetu. Rejea mfano kutoroshwa wanyama wengi tu hapo Oktoba 26, 2010 kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro. Tangu ufiadi huu kufanyika serikali imekaa kimya kana kwamba hakuna kilichofanyika. Baya zaidi, hata hawa wanyama walkioibiwa hawakupelekwa kwenye nchi za magharibi bali Qatar. Mtuhumiwa wa jinai hii ni raia wa Pakistani aliyeshirikiana na watawala wetu wanaojifanya kutojua lolote kuhusiana na kadhia hii.
Ni bahati mbaya hata viongozi wakubwa wa dini wanaliona hili na kulifumbia macho wakitengeneza maadui bandia ili kuwaaminisha wananchi na kuwanusuru watawala marafiki zao. Hapa hatujaongelea madai kuwa ndege ya rais wa China iliondoka na shehena kubwa ya pembe za ndovu. Hili lilipotokea, wakubwa zetu walitoa majibu ya kitoto yasiyoingia akilini na wakanyamaza. Mchezo kwisha. Kwa sasa tuna wananchi wengi wa China wakifanya magendo ya vipusa na biashara ya kimachinga huku wamachinga wetu wakipigwa, kufukuzwa na kunyang’anywa mali zao kila uchao. Hawa hakika, ndiyo watakaotuchonganisha kwa vile wanaziba maslahi ya watu wetu waliokatishwa tamaa na uongozi fisadi na mbovu.
  Hawa wanaosema eti nchi za magharibi zinatuchonganisha ili amani itoweke wauze silaha wanashindwa kutwambia ni kwanini nchi hizi hizi za magharibi zinapotoa fedha ya kuendesha serikali yetu kwa zaidi ya aslimia 40 hauwi uchonganishi.Wakitupa fedha ya kuendesha serikali yetu fisadi hatulalamiki
Kama hatutaki uhusiano nao basi tujitegemee.
          Pia wanashindwa kusema kama hizi nchi ambazo si za kimagharibi hazituchonganishi. Bahati mbaya hazichangii hata bajeti ya serikali yetu mzigo
China wanatuibia hata pembe za ndovu na kutujazia wasaka riziki. Hata wanyama wetu waliopotoroshwa kwenda kwenye nchi za kiarabu hakuna aliyeliona hili na kulipigia kelele. Tunajenga tabaka la viongozi wa aina gani ambao wanataka kutumanisha katika uongo ili tusiuone na kuufanyia kazi ukweli? Ni bahati mbaya sana walipoimbiwa wanyama wetu hakuna hata moja iliyopinga ujambazi huu.
Kwanini tunakubali kuchonganishwa? Je tunachonganishwa au tunajichonganisha, kuchonganishana wenyewe na kutafuta maadui wa bandia ili kupata namna ya kuzoa wafuasi?
Nadhani hakuna kitu kinatuchonganisha na kitatuchonganisha sana kama taifa kama ufisadi ambapo kikundi kidogo cha watu kinawaibia wengi na kutajirika huku wao wakiendelea kuwa maskini wa kutupa. Bila kuwabana hawa na kuwawajibisha, hizi mbinu zote za kutaka kutengeneza maadui wa bandia hazitafuta dafu. Tunachonganishana sisi kwa sisi yaani baina ya mafisadi na waathirika wa ufisadi. Hili ndilo tatizo na sababu itakayoondoa amani ambayo nayo si amani chochote kwa vile hakuna haki. Huwezi kuwa na amani bila kuwa na haki. Huwezi kuwa na amani sambamba na ufisadi. Lazima uchague moja, amani au vurugu tokana na kushindwa kupambana na ufisadi. Haiwezekani wezi wanaoibuliwa kila siku waendelee kutanua wakitukoga na kutufungulia kesi kila siku nchi ikawa na amani. Ni bahati mbaya sana kuwa hata wakubwa zetu wa kiroho hawakemei zaidi yaw engine kuwa washirika wakubwa wa mafisadi kama ilivyogundulika kuwa maaskofu wawili waandamizi walikatiwa fedha ya escrow.
Cha msingi kwa viongozi wetu wa kiroho ni kuacha kulala kitanda kimoja na viongozi mafisadi.  Kwanini kuweka nchi zote kwenye kapu moja kama si ujinga? Hivi kitendo cha Uswizi kutuambia kuwa kuna wakubwa zetu mafisadi, wezi, wachoyo na wenye roho mbaya walioiba fedha yetu na kuificha huko serikali ikajifanya haisikii ili watu wake wasiumbuke nacho ni uchonganishi? Kama ni uchonganishi basi ni mzuri.
Tumalizie kwa kuwataka wote wanaoamini kuwa tunachonganishwa na nchi za magharibi ambazo zimekuwa zikifadhili serikali yetu wawe wakweli na kuliangalia tatizo halisi badala ya kutengeneza maadui bandia. Nchi za magharibi zikiacha kuifadhili serikali yetu nchi haitakarika. Kama huu ni uchonganishi basi ni mzuri.
Chanzo: Dira

No comments: