The Chant of Savant

Tuesday 27 January 2015

Kijiwe chaomboleza ndata



 Pamoja na kwamba ndata huwa wanatughasi hata kutubambikizia kesi wanapotudaka, hatuna kinyongo nao zaidi ya kuwaonea huruma kwa wanavyotumiwa wakijiona hadi kuhatarisha maisha yao. Baada ya kutokea mashambulio mengi kubwa likiwa la hivi karibuni pale Ikwiriri, kijiwe kimekaa kama kamati kutoa rambirambi na tamko. Kinatoa shule kwa ndata wajitambue na kuchukua hatua kabla hawajamalizwa.
Mgosi Machungi siku hizi anajilawa kweli kweli. Leo kamuwahi hata muuza kahawa utadhani kuna upupu kitandani mwake. Nani anajua? Huenda bi mkubwa kamwekea mgomo. Hayo tuyaache.

Mgosi baada ya kuridhika kuwa  yakama au korum imetimia, anatafuna mic, “Tilishawambia kuwa wanatumika kishiasha lakini walitidhaau. Unaona sasa majambazi yanawaua kama swaa na kuchukua vya moto vyao kiahisi kana kwamba ni vichanga?”

“Mgosi nawe kwa kuanzia stori katikati huna mfano! Kumbe unaongelea mauaji ya ndata kule Ikwiriri siyo?” anauliza Mchunguliaji huku akijiweka vizuri kwenye benchi.

Mpemba aliyekuwa ndiyo amemaliza kuagiza kahawa anakwea mic “Yakhe hii yantisha sana hadi nataka nirejee zangu Pemba. Yawezekanaje hawa wanioitwa majambazi wavamia vituo na kupora silaha kirahisi hivi kama hakuna namna hata baada ya kuwa hii ishatokea kule Mwanza na kwingineko?”

Kapende hangoji Mpemba aendelee. Anakula mic kinomi, “Kwani ukienda Pemba unadhani utanusurika wakati kaya ni moja Ami? Hapa dawa si kufanya kama akina Kanji ambao wakisikia tatizo hukimbilia kaya jirani hadi mambo yapoe. Tunapaswa kusimama na kuwatetea hawa jamaa wanaoonekana kushindwa kujitetea hata wanapohujumiwa kwa kutumiwa vibaya na watafuta ulaji,” Kanji anamkata jicho la hasira kusikia akitaja magabacholi lakini hasemi kitu.

Mijjinga huku akiweka vizuri mavazi yake tokana na kupenda kuulamba na kuonekana kama Peedeejee, anapoka mic, “Hivi kama hawawezi kujilinda wataweza kutulinda kweli au ni kutumia kodi zetu kuwaneemesha wakati tukihangaishwa na wahalifu?”

“Kumbe wewe huwa wanakulinda! Kama kuna wanachonifanyia sikingine bali kutudunda tunapoandamana kupinga ujambazi uwe wa bunduki au kalamu. Kwa vile umewalenga, huenda wakaelewa somo,” Mipawa anajibu huku akitabasamu.

“Usemayo ni kweli. Wenye kulindwa ni wanono wanaoweza kuamuru ndata hata kuwakomesha wabaya wao binafsi. Mnaojidanganya kulindwa mmeliwa na mtaliwa sana,” Mbwamwitu anachomekea huku akimtazama Mgosi kwa chati akijua fika asivyopenda neno kuliwa.

Mzee Maneno anaamua kumpa sapoti Mbwamwitu japo huwa wanakosana mara kwa mara kutokana na maneno yake ya kufyatua. Anasema, “Kweli, wangekuwa wanatulinda si wangewakamata majizi na mafisadi yanayotuibia kila uchao. Si wangewakamata hata hawa wadokozi wa kura zetu wachakachuaji.”

“Yakhe usemayo nkweli. Wangekuwa wanatulinda si wengeenda kamata wale walokataa hata kuapisha viongozi kwa vile eti waloshinda upinzani.”

“Wankamate nani wakati wote chama moja dugu yangu. Usinikumbushe nshike nshike wa Segerea wa kuapishana kwa kutumia mawakili baada ya wachakachuaji kuzidiwa ujanja na people power,” Anachomekea  Kapende.

Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu,“Hapa halindwi mtu. Tunalindwa na Mungu vinginevyo, naona ndata kama wanyanyasaji wanaotumiwa na wanono, finish. Nadhani hawana haja ya kunung’unika wala kuonewa huruma hasa ikizingatiwa kuwa wao ndiyo wamewalea majambazi n ahata wengine kushirikiana nao wasijue hawa jama hawana dini.”

Baada ya Msomi Mkatatamaa kumaliza kusoma gazeti lake la kitasha anaamua kutia guu huku kila mtu akiwa na hamu ya kusikia atasemaje. Anakohoa kidogo na kubwia kahawa yake na kusema, “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hawa ndata waliwalea majambazi hata baadhi yao kufikia kushirikiana nao wasijue kuwa hawa hawana dini kama alivyosema msemaji mmoja aliyepita. Kimsingi, huu si wakati wa kuwalaumu ndata bali kuwasikitikia na kuwapa darasa wajue kuwa nao wanaliwa kama wale wanaodhani wananyanyasa kwa vipigo kila siku.”

Anabwia kahawa na kuendelea, “Kwa waliosoma mambo ya kiutawala tunajua fika nani wa kulaumiwa. Ulitegemea nini kwenye kaya ambapo kila mtu  anaruhusiwa kujiibia bila kushughulikiwa? Unategemea nini kwenye kaya ambapo kila mja anaruhusiwa kutajirika bila kutoa maelezo ya alivyopata huo ukwasi? Kama kuna kitachowamaliza ndata si kingine ni hiki. Pia kile kitendo cha kujiruhusu kutumika kuwa kikwazo cha ukombozi lazima kitawagharimu hata maisha yao kama ilivyotokea. Na huu si mwisho wa filamu yenyewe. Watanyotolewa roho wengi tu.”

“Kumbe tatizo ni kubwa kuiko tinavyoiona!” anashangaa Mgosi Machungi.

Msomi anaendelea kudema, “Hivi mlitegemea nini wanene kufunga ndoa na mafisadi na wezi? Kufanya hivi ni kuweka kaya kwenye autopilot. Kwa wale tuliopanda ndege autopilot ni mfumo wa kuendesha ndege bila rubani au rubani kuifanya ndege ijiendeshe yenyewe.”

Kabla ya kuendelea, Sofia Lion Kanungaembe anauliza, “Kweli ndege inaweza kupaa bila rubani jamani?”

Msomi anajibu, “Nilitegemea swali hilo. Usingeuliza ningeshangaa. Ukweli ni kwamba si ndege tu. Siku hizi kuna hata magari yanaweza kukatisha mitaa bila dereva. Hilo si muhimu leo. Muhimu ni kwamba tangu wanene walipojiingiza kwenye mashindano ya kuibia kaya, basi imebaki kama haina mwenyewe. Kwanini majambazi wa mitutu wasiichukue iwapo wanaona wenzao wa kalamu wameishafanya hivyo? Umemsikia mnene akilaani jinai hii au kueleza atakavyopambana nayo? Kimsingi, ndata wasipogutuka watatolewa kafara na wataliwa wakijiona kama wale wanaowanyanyasa.”

Kijiwe kikiwa kinanoga si mvua ikaaza kunyesha!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 28, 2015.

No comments: