The Chant of Savant

Saturday 24 January 2015

Mlevi apanga kubadili jina

Japo sera ya uga huu ni kuepuka kadri iwezakanavyo kutaja majina ya ngurumbili. Hata hivyo, tokana na uzito na umuhimu wa suala la leo tutavunja huu mwiko wa kutaja majina hata kama siyo ya watu wanaoishi hata kufanana nayo. Hivyo, atakayeingia mkenge akadhani majina yatakayotumika hapa ni yake atakuwa na kibarua cha kuthibitishia mahakama kuwa kweli majina ni yake bila kukosea hata nukta. Hata hivyo sheria husema: To every general rule there is an exception to it.
          Kuna majina matatu au manne yaninyima usingizi.  Majina haya yanifanya nikonde. Nimejaribu kuvuta mibangi na kupiga ulabu ili kujisahaulisha majina haya bila mafanikio, majina haya yamegeuka majini kwangu. Kwani yanaanza kuninyonya damu akili na mawazo.
          Kwa vile nina usongo, tuseme hata uroho wa ulaji, kuanzia wa kisiasa hata kiwekezaji na hata kutorohsa nyara za taifa la shamba la bibi la Danganyika. Ili kutengeza njuluku ya kuweza kuwahonga wapika kura ya kula wapumbavu, sorry, wajanja, lazima niwe na njuluku sawa na mafisadi wanaotumia njuluku kutaka kuukwaa ukuu. Siku hizi bila kuwa na kufuru ya njuluku hupati ulaji hata kama ni wa nyumba kumi. Tangu utumishi wa umma ugeuke utumiaji umma, lazima mwenye kuutaka uwe na mshiko wa kuwashikisha wauza kura ya kula.
          Kama nataka kugombea uhishimiwa na kuupata kirahi lazima nibadili jina na kuwa Riz Kitegemezi badala ya mlevi. Hivyo, tukikutana mitaani siku zijazo sitaki nisikie jina langu la Mlevi Mkuu bali mwana wa mkuu Riz au ikipungua ikazidi basi niite Jan Makambale kama siyo God Mgimua au Imma Nchimbvi kama siyo Hussein Muinyi au Adam Milima ya Kigoma.
          Kwa vile nataka nipate dili za kuwa-srew walevi lazima nibadili jina na kuitwa Jimmy Rugemalayer. Najua nikiwa na jina hili nitavutia wakubwa wanaotafuta makuwadi wa kusimamia biashara yao fichi ya nyuma ya pazia kama ambayo wajina wangu amekuwa akifanya kwa takribani kwa miaka 20. Mungu akupe nini zaidi ya jina tamu linalovutia na kuwahamasisha wakubwa wakutumie au, tuseme, mtumiane kuwaibia walevi?
          Kwa vile huyu jamaa ameishachafuka sana na pia akiamua kushupaa hakuna pa kumbwaga, nina wasiwasi. Wakubwa wanaweza kuachana naye akabaki na akina Anna Kajuamlo, Jaji Mujuulizi na Ruhangaisa na nshomile wengine. Hivyo basi napanga kujiita Harbinger Seti Sing Song of screwing boozers. Ukiwa na jina kama hili unakuwa na uwezo wa kuwaweka wanene mfukoni mwako na kufanya utakavyo hata ukiamua kudhalilisha kaya kama wenye majina haya wanavyofanya kila uchao bila kuguswa. Ukiwa na jina hili , hata wafwadhili waking’akia dili zako wenye kaya wanajifanya kutojali wala kusikia kwa vile unayefanya mambo ni wewe mwenye jina tukufu duniani.
          Kwa vile kusafirisha wanyama nje kunalipa, napanga kubadili jina niitwe Kamran Ahmed ili nami nipate wakubwa wa kunitumia kusafirisha wanyama hai kwenda Qatar. Najua dili italipa hasa ikizingatiwa kuwa nikikamatwa watanitoa korokoroni na kunitafutia hati ya kusafiria na kutokomea ili nisiwataje.
          Ili kusafirisha pembe za ndovu bila kushughulikiwa, napanga kubadili jina na kujiita Abdul Kinamna au Ivory Kang Xi Pingpong Dong Kong ili nisafirishe vipusa na kuukata haraka kama siyo kupewa ulaji kwenye chama twawala kama Abdul Kinamna ambaye anaendelea kutesa huku kashfa yake ikisukumizwa chini ya busati. Hii Bongo usicheke wala kudhani hii ni mipango ya kibangi bangi au ulabu. I am dead serious guys. Nikishaitwa Ivory Kang Xi Pingpong Dong Kong nitaweza kupanga jumba la bei mbaya maeneo ya Msasani na kukusanya kago bila kubughudhiwa na ndata wala mashushu uchwara kama Rama Igondhuz wanaoaminika kutumika kuwapiga akina dk Steve Ulimboka na Absalim Kibanda.
          Ili kusafirisha miunga bila kusumbuliwa lazima nibadilishe jina niitwe Masogangege. Najua nikishaanza kuitwa mr Angie Masogange nikitia timu pale Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa mzee Mchonga washikaji zangu walioajiriwa pale kuruhusu miunga ipite hawatanisumbua zaidi ya kutaka niwakatie chao na kila mmoja achukue hamsini zake. Nitapita utadhani napitisha bidhaa halali au vitu vya maana. Kama twiga wanapita itakuwaje midawa isipite?
          Ni raha na ujiko kuwa na majina matakatifu kama vile Rugemalayer, Singasinga Harbinger, Dong Kong, Riz na mwengine mengi. Uwiiii! Nitaukata kama sina akili nzuri. Ngoja kwanza nisokote bangi inibangue nipange mipango mingine mikuu ya kuwa bilionea ghafla bin vu kwenye kaya hii ambako wizi umehalalishwa na utajiri wa haraka ni halali.
          Ikizidi ikapungua najiita  Malegelesi au Lukaza kama wale jamaa zangu wa EPA kama siyo Roasttamu la Aziz wa Kagoda ili nichonge dili jingine na HEPA niwahepe wachovu na kufaidi njuluku zao kama hawa jamaa wanavyoendelea kuzila huku wengine wakitangazwa kuwa mabilionea wakati ni wezi watupu. Kwani hatujui wala kuona?

          Ukihomola fedha za HEPA unaambiwa na mkuu urejeshe utadhani ulikopa wakati ulikwiba tu. Hii ndiyo Bongolalaland ambapo ubongo huwa hauna matumizi zaidi ya utumbo.
Chanzo: Nipashe Januari 24, 2015.

No comments: