Tuesday, 27 January 2015

Mfumo fisadi usiwatoe kafara askari wetu

Wakuu wa Jeshi la Polisi wakikenua baada ya kutupia cheki na fisadi Harbinder Sethi Singh mwizi wa escrow

         

          Tanzania sasa iko msambweni. Inatenzwa kana kwamba haina viongozi, na kama wapo, hawaoni wala hawasikii, ukiachia mbali kutofaa wala kujihangaisha kupambana na majanga yanayowakabili umma ambao sasa ni yatima.     Kuvamiwa kituo cha polisi cha Ikwiriri, Pwani hivi karibuni na wanaosemekana kuwa majambazi ni kiashiria cha uoza wa mfumo fisadi. Askari wawili wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu waliripotiwa kufa huku bunduki saba na risasi 60 ambazo, bila shaka, madhara yake yatakuwa makubwa baadaye zikiibiwa. Inashangaza polisi wanaopaswa kulinda usalama wetu nao si salama. Je hapa nchi ni salama? Ajabu hata kadhia hii ilipotokea, serikali haikuja na tamko stahiki lau kuonyesha kuwa kuna serikali. Je kuna magenge ya watu yanayotaka kuingia msituni kama ilivyowahi kudaiwa na baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati wa bunge la katiba wakisema kuwa kama rasimu ya jaji Warioba ingepita wangeenda msituni? Je hawa siyo sehemu nzuri ya kuanzia upelelezi? Je kuna kitu watu hawa wamenusa kiasi cha kuanza kujiandaa au ni matukio tofauti? Jikumbushe kauli za John Komba, mbunge wa Mbinga na William Lukuvi (Ismani)? Ni bahati mbaya. Hata waheshimiwa hawa walipotoa madai hatari kama haya, hawakuhojiwa kwa vile ni vigogo wa chama na serikali.

          Ifahamike kuwa Ikwiriri si kituo cha kwanza wala mwisho cha polisi kuvamiwa. Ilishatokea kule Mkamba Kimanzichana na Bukombe Geita. Kinachogomba ni kwanini serikali, hata baada ya kuvamiwa kituo cha kwanza, haikuchukua hatua kuzuia kurudiwa kwa jinai hii kama hakuna namna? Unaweza kutoa hitimisho lolote hasa ukizingatia kinachofanyika kwenye kushughulikia kashfa za wizi wa mabilioni ambapo baadhi ya wezi wanaonekana kutoguswa hata wakitenda jinai kiasi gani. Hawa wanashindwa kuanza kuanzisha majeshi yao?

          Ukivuka mpaka ukajielekeza kwa kinachofanyika Nigeria ambako kundi la Boko Haram linaihenyesha serikali au Somalia ambapo al-Shabbaab wanaipa hali ngumu serikali nchini humo na nchi jirani ya Kenya, unaweza kujua ninachomaanisha hapa. Hata haya makundi kama al-Houthi kule Yemeni, al Qaeda Maghreb na mengine mengi yalianza hivi hivi.  Je wizi huu wa silaha toka vituo vya polisi unaashiria nini kwa taifa ambalo liko msambweni kutokana na kukosa uongozi makini na wenye visheni?

           Zama za awamu ya kwanza, kitu kama hiki kingetokea, mipaka yote ingefungwa na wahalifu hawa wangesakwa na kutiwa adabu. Lakini sasa nani afunge mipaka wakati watu wameziba masikio wakihangaishwa na wizi wa fedha za umma na kuusaka ukuu bila kuwa na ajenda yoyote ya kuufayia umma zaidi ya kuibia na kuutumia watakavyo kama ambavyo imezoeleka kuwa urais kwa sasa ni kijiko kikubwa cha kuchotea utajiri kwa mwenye kuwa nao pamoja na familia, marafiki, hata waramba viatu wake?

          Kwa matukio haya matatu ya kuvamia, kuua askari, kupora silaha, kuharibu mali ya umma, kuruvuga amani, kutenda jinai, kumilki na kutumia silaha kinyume cha sheria na kutishia usalama wa taifa, ni ushahidi kuwa taifa letu si salama tena. Kama tunashindwa na magenge ya wahalifu wawe wanatumwa na wakubwa wanaotishia kwenye msituni au wanasukumwa na jinai yao, je tukivamiwa na taifa jingine tutafurukuta kweli? Inakuwaje tunapata polisi wengi wa kuwapiga wapinzani na waandamanaji lakini tunakosa hata polisi wa kujilinda?

          Uvamizi wa vituo vya polisi licha ya kulidhalilisha jeshi la polisi, unatishia maisha ya askari wetu ambao hawakwepi lawama kwa kujiruhusu kutumika kisiasa huku maslahi na usalama wao vikiwa hatarini.  Ili kuwa salama askari wetu wanapaswa kuasi na kuacha kutumiwa kisiasa kama walivyofanya wenzao wa Tunisia, Burkina Faso na kwingineko ambako serikali zilizokuwa zimelala kwenye usukani zilifurushwa baada ya askari polisi na jeshi kukataa kutii amri za kuzuia waandamanaji waliolenga kukomboa nchi zao.

           Polisi wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu. Wana mishahara na marupurupu kidogo sawa na watanzania wengine ikilinganishwa na wanasiasa. Pia wanaisha maisha ya chini sana. Ukienda kwenye Kota zao, nyingi zinatia aibu. Wengine hata sare zao zinaonyesha ugumu na uhovyo wa maisha wanayoishi. Hapa hujaongelea udhalilishaji na chuki wanavyopambana navyo baada ya kutumiwa kisiasa kuwapiga na kuwaumiza watu wasio na hatia waliopaswa kuwalinda. Je kuvamiwa kwa vituo vya polisi ni jinai ya kawaida au chuki za wananchi dhidi yao? Tunapaswa kuzama zaidi.

          Japo lolote lawezekana, mazingira ya ukosefu wa maadili yaliyojengwa tangu kuondoka serikali ya awamu ya kwanza ni ya kulaumiwa kwa matukio haya. Watu wanataka bunduki ili wafanya ujambazi na kuwa matajiri wakijua fika mfumo wetu haumbani mtu kueleza alivyopata utajiri wake. Huu ni motisha mkubwa kwa wanasiasa na wahaloifu bila shaka.

          Wakati umefika wa kuwataka watawala wetu wahakikishe usalama wa watanzania wote wakiwamo polisi wanaoshughulikia usalama huu. Pia umefika wakati wa polisi kuuhoji mfumo na mamlaka zinazowajengea mazingira ya kufanya kazi na kuuawa katika mazingira magumu kirahisi hivi.  Wavunje ndoa na wanasiasa na mafisadi na kufunga ndoa na umma.Tunatuma salamu za rambirambi kwa jeshi la polisi tukishauri IGP ajiuzulu kwa vile ameshindwa.

 Chanzo; Tanzania Daima Januari 28, 2015.

No comments: