The Chant of Savant

Saturday 31 January 2015

Mlevi aonya: Mwaogelea vinyesini mwajiona!

          Shalom le kulam,
Kila mvua zikinyesha kwenye jiji la Bongosisalama wataalamu wa ushenzi nao huonyesha sayansi yao ya kufungulia maji ya vyooni na kuchanganyikana na ya mvua ili kukwepa gharama ya kunyonya vyoo. Ni bahati mbaya kuwa huu mchezo umekuwa ukiendelea pamoja na madhara yake kiafya kwa walevi. Sijui hili nalo linahitaji wafadhili au wataalamu wa jinai kulitambua ili wahusika wachuke hatua? Je hawa wanaonyamazia maangamizi haya kwa walevi wanafaidika vipi kutokana na jinai hii au ni uzembe tu na ujinga n ahata upumbavu wa kutotambua kuwa magonjwa huvuruga mipango ya kaya ya maendeleo? Hata hivyo nani anajali iwapo maendeleo kwa wakubwa walio wengi ni wao kupata hata kama ni kwa kuwauza walevi na raslimali zao kama ilivyo?
Siku moja mlevi mwenzangu, baada ya kupiga mibangi aliniacha hoi nilipokuwa nikilalamika baada ya kurejea Uswekeni toka Kariakoo baada ya kuogelea kwenye mavi yaitwayo maji ya mvua. Baada ya kufika zangu kwenye baa ya Mama Coltide na kupata kanywaji, nilipoanza kunywa nikasikia kama harufu ya kinyesi vile. Nilidhani mwenzangu alikuwa ameachia hewa mbaya. Baada ya kumvaa nikimtaka aache kuachia hewa mbaya kwenye kadamnasi, naye alinikaba akisema alidhani mie ndiye nilikuwa nimeshua (kwa kisambaa) yaani kutoa hewa mbaya.  Kwa vile tunapendana na kuheshimiana na huyu mlevi mvuta bangi, ilibidi tutafute chanzo cha tatizo la harufu mbaya.
Jamaa aliniuliza kama nilikuwa nimekwenda Kariakoo siku hiyo. Baada ya kumwambia kuwa nilikuwa natokea kule, alisema, “Hakuna haja ya kukamatana uchawi wala kutoana macho. Kumbe hujui kuwa mvua imenyesha leo na umeogelea kwenye maji ya chooni!”
Ugomvi wetu uliishia pale jamaa alipojisemea, “Lisirikali linaona lakini haioni.” Nilipomuuliza alimaanisha nini kusema kuwa lisirikali linaona lakini halioni, alijibu kuwa tatizo linajulikana sema wakubwa hawataki kulifanyia kazi tokana na kuwa bize kwenye kupiga dili kuanzia escrow hadi bomba la gesi.
 Hivyo, tuligundua kuwa tatizo linajulikana lakini kila anayehusina anajifanya kutojua kuwa lipo.
Ukiangalia wakazi wenyewe wa katikati ya jiji na mambo yao ya kutia shaka, unashindwa kuelewa uanzie na kuishia wapi. Mambo fanyika kama iko Bombei! Veve iko soma Mahabharata? Iko jua Ugrasrava Sauti au Bhagavad Gita?  Basi kama iko jua sunskrit basi tafsiri hii Theudorena meridarkhena pratithavida ime sarira sakamunisa bhagavato bahu-jana-stitiye. Hebu tuache hindi. Mijitu kwa ubinafsi na ujinga hata ukatili linafungulia maji ya chooni lisijue kuwa magonjwa hayachagui. Nalo laweza kuugua hata kunyotoka roho. Je ni wangapi wanaliona tatizo hivi? Hata hivyo, tusishangae. Kama watu wananywesha maji ya chooni kwa kuhadaiwa kuwa ni ya kisima, unategemea nini?  Anayebisha kuwa hanywi maji ya chooni hasa kwa wakazi wa jiji wanaotumia ima maji ya visima au mizega ajitokeze nimuelimishe.  Hebu nikuulize japo kilevi. Je unajua hawa vijana wanaouza maji kwenye mizega wanapoyachota? Usiniambie kuwa wanayachota kwenye mito iliyotapakaa Dar ambayo mingi yake imejaa uchafu wa viwandani na majumbani bila kusahau kinyesi. Kama wanachota huko basi wewe unayenunua jua unakula uchafu tu taka usitake. Juzi juzi nilizurura kwenye kaya jirani kuanzia kwa kaya ya Nyayo hadi kule walikonyongana kwa mapanga. Guess what. Nilikuta miji yao mikuu ina maji ya uhakika safi na salama. Je sisi tulirogwa na nani ambao pamoja na kuwatangulia wenzetu kuunyaka uhuru kutokuwa na maji ya uhakika? Je wajua kuwa katika kaya hizi hata umeme si aghali wala wa mgao kama kwetu? Ajabu ya maajabu wenzetu hawana vyanzo vya umeme kama vyetu tunavyotukana kwa kutovitumia! Umeipata hiyo? Kama hujatosheka sema nikupe dozi nyingine.
Turejee kunywa, kufulia, kuogea na kuogelea kwenye vinyesi.FYI kama unategemea kunywa, kufulia, kupikia hata kuogea ujue huna tofauti na inzi. Tofauti ni kwamba inzi ni mdudu. Hana akili wala nguvu ya kujikomboa na kujiondoa kwenye kadhia hii tofauti na wewe unayetenzwa kama mdudu wakati u mja. Tunazidiwa na mijuzi ambao hunywa maji ya mvua na si ya vinyesi! Ni ajabu kuwa mvuta bangi na mlevi anaweza kuliona hili wakati wale wanaojifanya wazima hawalioni! Mtaendelea kunywa maji ya chooni hadi lini kwenye karne ya 21 au ndiyo maisha bien yenyewe mliyoahidiwa?

Usitake kunitapisha kusema eti hayo ndiyo maisha poa na mswano mliyoahidiwa na wasanii wenu. Yangekuwa hivyo, wengine wangeishi kwa kuiba maji na umeme? Kwani hatuwajui? Sijui na zoezi la kunyaka vishoka wa umeme na maji nalo limeishia wapi. Hata hivyo, kama tutasema ukweli, nani amkamate nani wakati naambwa kuwa lisirikali ndilo linaongoza kwa kutolipa ankara za umeme na ma-water? Ama kweli jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani! Unategemea nini toka kwa lisirikali ambalo waingereza huita sitting duck au bata aatamiaye? Ikizidi ikipungua wale wanene wanaokalia uchumi huitwa lame duck, kwa kisambaa. Hakuna kilionikera kama kusikia kuwa kuna wadhiri mzima wa Ma-water wakati hakuna ma-water kayani. Je huyu analipwa kwa kazi ipi iwapo walevi wanaogelea kwenye vinyesi kama inzi?  Ajabu waziri mwenye eti ni prof. Prof au porofedha kama siyo profedheha kama wale wa escrew au yule aliyejificha nyuma ya kampuni jambizi la Uda huku akiwatangulia matapeli wasio na hata nduru wakijifanya ndio wenye mali wakati wenye mali hii ya ufisadi wanajulikana. Hayo tuyaache. Nadhani huyu angeitwa wadhiri wa, vinyesi, sorry, mabomba yasiyotoa maji. Au tuseme waziri wa kukusanya malipo bila kutoa maji.
Chanzo:Nipashe Januari 31, 2015.

No comments: