Wednesday, 21 January 2015

Rais ajitoe kwenye makucha ya mafisadi

          Hali ilivyo, rais Jakaya Kikwete ametekwa na mafisadi kiasi cha kutofurukuta hata baada ya wananchi kulalamika na kupiga kelele. Inavyoonekana, Kikwete hasikii wala haoni. Ametekwa kiasi cha kuacha maswali mengi kuliko majibu. Wengi bado wanashindwa kuelewa ni kwanini Kikwete amejiruhusu kuonekana mhimili wa mafisadi dhidi ya umma. Wanashindwa wamuweke upande gani.
          Baada ya kuibuliwa kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha za umma toka kwenye mfuko wa escrow, mengi yamefichuka pia. Mafisadi watawala wakishirikiana na maajenti wao, waliliibia taifa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hadi sasa hakijulikani. Mwanzoni tuliambiwa zilikuwa zimeibiwa bilioni 200. Baadaye tukaambiwa kumbe zilizoibiwa zilikuwa shilingi bilioni 300 na ushei. Taarifa za mwisho ni kwamba tuliibiwa shilingi bilioni 400. Je kutaibuka ukweli na namba nyingine?
          Pamoja na utata kuhusiana na kiasi cha fedha kilichoibwa, serikali imeendelea kukaa kimya ikionyesha kila dalili za kulalia upande wa pili. Rejea maazimio ya bunge kuwa Kikwete awawajibishe watuhumiwa walioonekana kutenda kosa asifanye hivyo. Ajabu mtuhumiwa mkuu, waziri wa Nishati na Madini profesa Sospeter Muhongo anaendelea kutesa huku umma ukiteseka. Kitendo cha Kikwete kumkingia kifua Muhongo kimeacha maswali mengi kuliko majibu. Je lao ni moja au ni woga tu? Je anatoa picha gani kwa umma uliomchagua akiuaminisha kuwa angeulinda pamoja na mali na fedha zake?  Kwanini Kikwete anasitasita kumchukulia hatua Muhongo wakati ukweli uko wazi, alitenda kosa?
          Kinachotatizo zaidi ni mantiki ya Kikwete kumfukuza waziri wa zamani wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi profesa Anna Tibaijuka kwa kosa si la kusaidia au kushiriki kuibiwa fedha husika bali kupokea pesa kiduchu. Je alimtoa kafara kuuridhisha umma na wafadhili kutaka mambo yapoe Muhongo na wenzake waendelee? Ionekanavyo kwa mizania ya Kikwete, kupokea fedha za wizi ni kosa kubwa kuliko kuiba fedha yenyewe. Isingekuwa hivyo, watuhumiwa kama Harbinder Sethi Singh na James Rugemalira wangekuwa korokoroni wakingoja kupewa haki yao. Ilavkwa Kikwete si hivyo. Kama ilivyo kwenye kitabu cha Shamba la Wanyama cha George Orwell, wanyama wote ni sawa  ila wengine ni sawa zaidi. Haiingii akilini. Watu waliopokea kuadhibiwa kabla ya waliowapa hiyo fedha ya wizi. Je Tibaijuka akisema ameonewa au kutolewa kafara ataonekana kituko kama alivyokuwa aking’ang’ania wakati dalili zote zilikuwa wazi kuwa alikuwa amekalia kuti kavu? Je kwanini Kikwete anatenda kinyume na fikra na akili za kawaida?
          Wapo wanaoona kama rais ametekwa na mafisadi. Pia wapo wanaoona kama rais aliagiza fedha husika zikwapuliwe kutokana na jinsi alivyoshughulikia wizi mzima. Ikumbukwe. Hii si mara ya kwanza kwa Kikwete kuwanusuru mafisadi kwenye kashfa nyingine ya mabilioni EPA ambayo hadi kesho haijawahi kukanushwa wala kutolewa na maelezo na Kikwete baada ya kutuhumiwa kuwa alikuwa nyuma ya jinai hii ili kupata mtaji wa kushindia urais. Rejea jinsi watuhumiwa wakuu wa ufisadi kama Rostam Aziz walivyookolewa na Kikwete kiasi cha sasa kuambiwa eti ndiyo mabilionea wanoongoza kwa utajiri nchini na si wizi wa fedha za umma.
          Hali ilivyo ni kwamba umma umekata tamaa kiasi cha kuwa watazamaji. Baada ya Kikwete kufanya kile waingereza huita leap service inaonekana hata wafadhili wamenyamaza kiasi cha kupoteza matumaini ya watanzania. Wengi wanashangaa mantiki ya Kikwete kuwataka wezi wa EPA kurejesha fedha lakini asifanye hivyo angalau dhidi ya wezi wa escrow. Je hii ndiyo lala salama ambapo wahusika, kama walivyokusanya mtaji wa kuingilia, wanakusanya mtaji wa kuondokea? Je hii ni stahiki na haki kwa watanzania? Je mtu aliyefanya hivi atashindwa kuhakikisha kuwa atakapoondoka madarakani anaacha kibaraka wake wa kumlinda kama alivyofanya Benjamin Mkapa baada ya kutuhumiwa kwa kashfa mbali mbali ikiwemo ya EPA ambapo mwanasheria aliyesimamia uhamishaji wa fedha za EPA aliwataja vigogo wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)?
          Kama upuuzi uliofanyika 2005, hakuna shaka. Rais ajaye atakuwa mateka wa mafisadi kama ilivyo kwa Kikwete ambaye ameonyesha wazi kuwa tayari kulaumiwa kwa kuwalinda mafisadi. Ameziba masikio na midomo. Amewadharau watanzania kuwapuuzia. Amedharau na kulipuuzia Bunge na hata wafadhili ili kunusuru watu wake. Je ni kwanini kama hakuna jinsi anavyonufaika na watu hawa? Imefikia mahali Muhongo na wezi wa escrow wanaonekana kama serikali ndani ya serikali. Kulikoni? Je kwa namna hii Kikwete, serikali yake na chama chake hawajetekwa na mafisadi kama si kuwa sehemu yao? Je kigugumizi cha Kikwete kinatokana na nahau kuwa waarabu wa Pemba hujuana kwa viremba? Je kwa muda mfupi uliobaki kwa Kikwete kuondoka ofisini, kama ataendelea na msimamo wa sasa wa kuwalinda mafisadi, watanzania wamejiandaa kufanya nini kuhakikisha haki yao haipotei? Je watawaachia kila kitu wanasiasa na wafadhili au kuchukua hatua mujarabu ili kutoa onyo kwa watawala wajao kutowatenza kama shamba la bibi? Je wataendelea kunywea na kugeuka kondoo wa kafara arariwaye bila kujitetea? Je ukimya, au tuseme kutojali au woge huu utalifikisha wapi taifa?
Tumalizie kwa kumtaka Kikwete ajiondoke kwenye makucha ya mafisadi. Alichaguliwa na watanzania na si mafisadi. Asikubali watanzania wamkumbuke kama rais aliyesimamia na kuwezesha ufisadi. Kuna maisha baada ya urais.
 Chanzo: Tanzania Daima Januari 21, 2015.

No comments: