The Chant of Savant

Tuesday 6 January 2015

Kijiwe chafunga mwaka na pongezi kwa wafadhili

 
Kijiwe kimemaliza mwaka kivyake vyake kwa kutoa msimamo wake dhidi ya ufisadi na jinsi wafadhili walivyojitahidi kumtoa nyoka pangoni hata kama hatukumkata kichwa. Kwa mwaka mzima tulikuwa tunawashangaa hawa jamaa kutaka kujaza maji kwenye pakacha. Kitendo chao cha kumbana Njaa Kaya hadi akalazimika kumtoa kafara Annae Kajuamlo si cha kupuuuzia.
Mijjinga anaingia akiwa na gazeti la Dangayika Ever mkononi. Anaamkua na kupoka mic, “Wazee mnaunaje huu mwaka tunaoanza? Je mnadhani mambo yatabadilika au yataendelea kuharibika hasa kwenye lala salama ya jamaa yetu?”
Mgosi Machungi anakwanyua mic na kujibu, “Hivi titategemea wafadhiii hadi lini? Hawa wakikamiiishiwa maslahi yao wanachomoa. Hivyo, tisiwategemee sana hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo wanawaweka wezi madaakani kwa kuwapa njuuku ambazo wanavuja kwa kutumia jina letu. Kubomu na kukopa ili wakwapue.”
 “Mgosi usemayo kweli. Hata kama si watu wa kutegemewa hata kama wakimegewa wanabadilika lau wamejitahidi kuwaadhirisha walaji wetu waso na haya wala maya ya kutenzwa kitwahuti wallahi,” Mpemba anajibu huku akitupia ugolo kinywani.
Msomi Mkata Tamaa anatia guu, “Hapa wa kulaumiwa ni wadanganyika wenyewe kwa kupenda kuliwa. Mgosi anamkata jicho. Maana huwa hapendi kusikia neno kuliwa.”
Msomi naye anamkata jicho Mgosi haraka na kuendelea kudema, “Nadhani hakuna aliyewekwa pabaya kama Njaa Kaya. Nataka kuona atakavyowanusuru washirika zake hasa Endelea Chenga, Sossie Muongo na wale majanki wa mahakama kubwa wanaotumiwa na mafisadi kama nepi chooni. Kama wafadhili wanatupenda basi waache kutoa misaada yao uone kama patakalika.”
“Nadhani baada ya kumtoa kafara Anna Kajuamlo Tiba, jamaa anaweza akawanusuru wenzake. Anaogopa nini iwapo alishaitoa kaya kafara kwa akina Rugemalayer na Sing na majambazi wengine? Hata hivyo, anashindwa kuelewa kuwa hatakaa kwenye ulaji milele. Yuko wapi Tunituni Beni Makapi?” Anauliza Mipawa huku akipokea kipisi cha sigara kali toka kwa Kapende.
Mheshimiwa Bwege anakamua mic, “Mie sipendi kuwalaumu hawa makuwadi. Unaweza kukuta hii IpTL ni mali ya wanene wenyewe. Ila siku kikiumana watatafuta pa kwenda wasipate. Hata hawa wafadhili nao wanatuzengua. Si waache kutoa misaada waone tutakavyoamka na kufanya kweli.”
“Nakuunga mkono. Katika kaya ya matapeli na sera za kimazingaombwe lolote lawezekana. Kimsingi, hawa satahiki yao ni kunyongwa na miili yao kupewa mbwa wale au kutupwa chooni. Sipendi kusikia upuuzi wa baadhi ya wasomi wanaosema eti wafadhili wakisimamisha misaada watu wa chini ndiyo wataathirika wakati huwa hawapati hata senti ya hiyo misaada yao. Wanyimeni tuwapige chini haraka.” Anachomekea Mchunguliaji.
“Hata hivyo, tuache kuwalaumu wala kuwategemea wafadhili. Sisi kama wanywa kahawa tumefanya nini kuleta mabadiliko? Huu nao ni ufisadi wa kimkakati. Yaani wafadhili watoe njuluku sisi tushindwe hata kupambana na wanaoziiba hadi wafadhili waje kutusaidi utadhani sisi ni vifaranga au mayai! Nani anakumbushia njuluku zilizofichwa Uswizi na visiwa vya Jersey?” Msomi anaongea huku akisogeza laptop yake pembeni.
“Mzee hapa umenena. Nasi tunapaswa kulaumiwa. Maana tumekuwa tegemezi hata kimawazo utadhani vichwa vyetu vimejaa tope kama watawala wetu. Maana ukiangalia upuuzi na ujambazi unaoendelea bila shaka kuna mshipa unaokosekana kwenye bongo zetu. Inakuwaje kaya nzima inakuwa ya ngurumbili woga, wezi, mafisadi, wababaishaji, wapenda raha, wapiga midomo, wavivu, na wasanii?” Mijjinga anaongea kwa usongo na kumalizia kwa kusonya.
Mgosi Machungi anakatua mic, “Mgoshi umeua. Huoni matapei wakubwa na wadogo kutoka kila kaya walivyojazana kayani mwetu? Wapo wanaokuja kama wawekezaji wakati ni wachukuaji. Wengine wanakuja kama wachungaji wakati ni wachunaji. Wengine wanakuja kama wana muziki wakati ni waganga njaa.”
Kapende anabwia mic, “Mgosi usemayo ni kweli tupu. Hawa matapeli toka nje wakifunga ndoa na wale wa kisiasa unategemea nini? Hukusikia mchunaji mmoja anayejulikana kutumiwa na fisadi fulani wa Richmonduli alivyodai kununua chopa utadhani hatujui kuwa anayenunua ni Ewassa mwenyewe? Ukiuliza amepata wapi hii njuluku kama si ya kifisadi au bwimbwi anashika kigugumizi. Je analipa kodi? Upuuzi mtupu.”
Sofia Lion aka Kanugaembe hangoji waendelee kunema. Anakwiba mic, “Sasa masuala ya kulipa kodi unatuuliza sisi tukupe jibu gani? Kama una ushahidhi halipi kodi si ufungue kesi.”
Kanji kuona mshikaji wake katia timu naye anaamua kufyatuka, “Swahili penda sema sana bila tendo. Kama naona vatu ibia veve kwanini hapana fukuza yeye? Hii Ongo, Tibajuta na Masi nakosea sana, naiba juluku najaza gunia na box kama dagaa bwana. Hii Gemalira na Singh ni jambazi natumiwa na kuba. Mimi sema kaama Sofi nasema, peleka yote hakamani ijue kama kunguru ni nyama au boga.”
“Leo Kanji umeona mwanga. Nadhani sasa unajua ni kwanini kunguru kimbia India kuja Afrika,” Mzee Maneno anachomekea.
“Tani ingine baya dugu yangu. Mimi sema kama kunguru iko nyama au boga sasa kunguru ya Hindi naleta nini dugu yangu?”

Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si dala dala likaturushia maji! Tukiwa tunajiandaa kulifukuza ili tumtie adabu dereva Msomi si katuzuia na kusema, “Kuwaadhibu wadogo na kuwachoma vibaka mnaweza wakati mnahusudu na kusujudia mibaka.” Hakuna aliyepinga wala kujibu zaidi ya kunong’ona.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 7, 2015.

No comments: