Wednesday, 9 March 2011

Fujo na vurugu vitaletwa na CCM


Wimbi la mapinduzi kaskazini mwa Afrika lilipaswa kuwaogofya watawala wababaishaji na wezi barani. Lakini ajabu bado kuna watu tena wanaoonekana na kudhaniwa kuwa wazima wanafanya mzaha na mambo ya kitoto na maisha ya watu waliowaamini. Wanacheza makida makida na maisha ya watu wanaowawezesha kuishi kupitia kodi zao!

Hakika hawa ni viumbe wasio na shukrani wala mshipa wa utu.

Maandamano yalipowang’oa watawala wa Misri na Tunisia, mlevi mmoja wa madaraka Muamar Gadaffi alisema yaliyotekea kwenye nchi tajwa yasingeweza kutokea nchini mwake.

Mungu si binadamu. Hazikupita wiki hata mbili mlevi huyu akajikuta kwenye matata tena makubwa kuliko ya waliomtangulia kupigwa teke.

Tumeanza na matukio ya Maghreb kuonyesha kuwa umma ukiamua kila kitu kinawezekana na waota mchana wanatimuliwa kama mbwa koko.

Hii maana yake ni kwamba maandamano yanayoendelea yakiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanapaswa kuungwa mkono. Ingawa walevi wa madaraka wanataka kuwageuza watanzania mabwege kwa kusema eti CHADEMA inalenga kupeleka nchi pabaya. Ni ajabu! Hivi kati ya CCM na CHADEMA nani ameishaipeleka nchi kubaya?

Tuchukue fursa hii kumkumbusha rais Jakaya Kikwete aliyehutubia taifa na kukaririwa akiwalaani CHADEMA mahali ambapo alipaswa kulaaniwa yeye na genge lake.

Hivi CHADEMA kusema kuwa malipo ya Dowans ya mabilioni ya shilingi ni jambo la kuipeleka nchi pabaya au kulipa? Hivi kulaani na kupinga kulanguliwa umeme ni kuipeleka nchi pabaya? Kweli kupinga mgao wa umeme wa miaka nenda rudi ni kuipeleka nchi pabaya? Kama hivyo ndivyo basi huku “kuipeleka nchi pabaya” ni kwema kuliko alikokwishaiuza nchi Kikwete.

Kikwete anapaswa kutambua kuwa mambo yafuatayo asipoyashughulikia yatamuondoa madarakani na si CHADEMA:

Mosi, kunkandamiza haki za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Pili, mauaji ya raia wasio na hatia. Rejea mauaji ya Arusha, milipuko ya mabomu kule Gongo la Mboto na Mbagala.

Tatu, kupanda kwa gharama za maisha na kuzidi kushamiri kwa ufisadi unaokingiwa kifua na Kikwete huyu huyu. Hapa hujagusa mfumko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.

Nne, kuendelea kupunjwa, kunyonywa na kudanganywa wa wafanyakazi.

Tano, ukosefu wa ajira na mazingira mabovu ya kazi.

Sita, kuendelea kuingia mikataba ya kijambazi kwenye maeneo mbali mbali.

Saba, Kikwete kuendelea kukumbatia na kuwalinda mafisadi na watuhumiwa wa kashfa mbali mbali kama vile kughushi vyeti vya kitaaluma.

Saba, kujuana na kulindana. Rejea kutoshughulikiwa kashfa ya watoto wa vigogo waliogundulika kuajiriwa Bank of Tanzania (BoT) kwa mazingira yenye utata. Hili unaweza kuliona hata kwenye baraza la mawaziri ambamo kuwa watu kama Hussein Mwinyi na Emanuel J Nchimbi, au wakuu wa wilaya, Nape Nnauye, Rehema J Nchimbi, na nyadhifa nyingine hasa kwenye balozi zetu nje.

Nane, matumizi mabaya ya pesa ya umma. Rejea kuandamana karibu kila mahali ughaibuni na mkewe na kuficha majina ya wanaoandamana naye huko.

Tisa, kutoa ahadi za uongo. Rejea ahadi ya maisha bora kugeuka maisha balaa kwa watanzania. Yako wapi maisha bora? jibu, hata akina Nyerere, Mwinyi na Mkapa hawakutatua matatizo yote. Hivi ndivyo alivyonukuliwa Kikwete akisema wakati wa kuishambulia CHADEMA.

Kumi, kuunda uongo na uhasama kwa kutumia udini ambao haupo bali kuzushwa na serikali ya Kikwete.

Kukimbia matatizo ya ndani kwa kisingizio cha migogoro ya kimataifa. Rejea Kikwete alivyokimbilia Mauritania wakati wa msiba wa wahanga wa milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto. Alishindwa hata kutangaza siku moja ya maombolezo kitaifa ukiachia mbali kutowajibika!

Kumi na moja, kuchakachua uchaguzi na noti mpya.

Kumi na mbili, kuendelea kugawa raslimali zetu na kuzidi kuingia mikataba ya uwekezaji ya kijambazi mipya kama huu unaoanza kupigiwa chapuo wa Dowans II.

Sababu za wananchi kutoogopa kuingia mitaani kupambana na ufisadi na ikiwezekana kumlazimisha Kikwete ama atimize wajibu na ahadi zake au aachie ngazi:

Mosi, kutokana na ukali wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) hakuna mtawala mwenye ubavu kwa sasa anayeweza kuua halaiki. Kwa woga wa hili na yaliyotendeka Arusha, Kikwete hana jeuri ya kuamrisha mauaji mitaani.

Pili, kubadili msimam kwa Marekani kwa kuacha kuunga mkono wezi na maimla barani Afrika. Kuingia kwa Barack Obama na makosa aliyotenda George Bush, Marekani imeamua kuacha wananchi walete ukombozi wao bila kuingilia kuokoa watawala. Tumeliona hili Libya.

Tatu ni wananchi kuelewa kuwa anachosema Kikwete kuwa CHADEMA inatishia amani ni tafsiri yake kuwa ama watanzania ni wapumbavu au amani ni wao na genge lake kula watakavyo huku umma ukizidi kuteketea. Hili ni tusi kwa watanzania. Ina maana watanzania hawajui maana ya haki, vurugu na amani hadi Kikwete awafundishe? Je kama CHADEMA ingekuwa tishio kwa amani watanzania ni wapumbavu waikubali badala ya kuilaani?

Kama kuna mtu anayetishia kuvunjika amani Tanzania si mwingine bali Kikwete na chama chake ambao wanawachokoza wananchi kwa kufanya maisha yao yawe magumu halafu wanakuja na porojo za kitoto. Huwezi kuwa na amani bila haki wala utulivu bila uadilifu. Wasibweteke na kipindi walichokaa madarakani wakihomola. Hata akina Hosni Mubarak na Zine al Abidine Ben Ali waliwahi kupitia mpito huu wasijue ndiyo wimbi la kuwakumba lilikuwa lawangoja. Ni bora Kikwete na wakwasi wenzake wakasoma alama za nyakati. Kama kuna anayevunja Tanzania si mwingine bali Kikwete na CCM kwa kuwadhulumu na kuwaweka rehani watanzania.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 9, 2001.

No comments: