Wednesday, 9 March 2011

Unataka kupitisha bwimbwi airport?

Mwenzenu nimepata zali la mentali. Washitiri wangu wamenisukia kupiga mzigo njia panda ya kwenda ulaya ilmradi niruhusu mabomu yao yapite nami nipitishe yangu au kupewa cha juu changu na kuwa bwenyenye na bopari.

Ukiwa na bwimbi au magendo nyingine we nitonye. Unanikatia changu unapitisha bwimbwi lako au mabomu bila kulipa hata hiyo kodi. Unaenda kuwauzia watoto wetu mie hiyo hainihusu. Unaenda kudhamini wanasiasa mafisadi kupata mtaji wa kuingia madarakani ili waibe mimi hainihusu. Mie nachukua changu mapema wajao watajaza wenyewe. Watajijejei na kujilaumu kwanini walizaliwa na mentali kama mimi na mpenda fweza kuliko utu.

Bongolalaland ni nchi nzuri sana. Ukighushu shahada unateuliwa kwenye kabineti. Ukikwapua banki kuu unafungwa miaka miwili halafu unaachiwa na kuja kutumia kama huna akili nzuri.

Tuongee mambo ya zali la mentali na jinsi wachovu tunavyolala makapuku na kuamka mabopari. Unaweza kuamini kuwa mzee mzima nimepata mshitiri akaniunga na immagireisheni ya uhamiaji? Sitamtaja jina. Maana hata wale walioingizwa kukuu na mafisiahadi hawawataji washitiri wao.

Jamaa yangu ambaye amefanya kazi hapa kwa takribani miaka mitano ana majumba magari na akaunti nono. Huyu jamaa tulikuwa tunasota wote kijiweni kabla ya shangazi yake kuwekwa nyumba ndogo na waziri wa nonihino. Nasikia huyu shangazi mtu aliunganishiwa na yule mama mwenye kusimamia kampuni la kuchimba gesi ambaye ni nyumba ndogo ya dingi wa kaya. Huyu bi mkubwa anaitwa mama Raha---no too much. Nadhani kimeishaeleweka. Ambaye hajanipatapata atajaza jaza mwenyewe.

Baada ya kukutana naye nikiwa nimepigika si ndiyo akanipa hii laini. Laini yenyewe ilikuwa simpo tu. Kama niko tayari kutafutiwa kazi na kufanya kazi ya kupitisha mabomu yaani bwimbwi la wahusika niseme. Mwenzenu sikujivunga. Hilo ndilo zali langu la mentali. Siku hizi kama huna mkubwa au jina kubwa ujue umekwisha.

Mwanzoni nilianza kujivunga nikisema hii ni kuhujumu kaya. Nikiwa nashangaa shangaa jamaa si alinitolea laivu kuwa mimi ni nani iwapo watu tena waheshimiwa wanafanya kazi chafu kama yule kijana wa mkubwa fulani aliyenyaka ubunge hivi karibuni anayetetea Dowanis kuliko hata walevi waliompigia kula.

Baada ya kuona sielewi somo alinipa dozi ya mwisho iliyonifyatua hadi nikageuka ghafla kuwa mbweha wakati nilikuwa simba kabla ya hapo. Alinipa stori ambayo nadhani kila msomaji anainyaka. Ni stori ya watu waliouza mama zao, ndugu zao hata makaburi ya babu zao na bado wakaendelea kuwaamanisha walevi kuwa watawapeleka kwenye nchi ya asali na maziwa, ulabu na mibange! Ajabu walevi hawajastukia usalata huu!

Aliponipa mfano huu mbona akili ilizibuka nikachangamkia tenda ya kuhujumu kaya yangu mwenyewe! Naomba Mungu siku moja yasitokee yaliyomtokea Kibaraak kule Masri maana sitakuwa na pa kujificha. Maana siku hizi walevi kwenye baadhi ya kaya wamechetuka kweli kweli.

Kila siku naomba amani na utulivu visitoweke ili niweze kuendelea kutanua hata kama walevi wanatanuliwa na dhiki. Amani na utulivu maana yake ni kwa wenye njuluku kuwatumia makapuku. Hii ndiyo amani ya kaya tunayoimbiwa kila uchao na wenye amani ya kuhomola watakavyo. Amani ni ukoo wa wateule kula hata bila kunawa kwa miguu na mikono wakitapika kama mainzi lakini bila kubughudhiwa. Mungu akupe nini unapojikuta kwenye kundi hili la wateule hata kama ni wachafu kama pig?

Juzi nilicheka rafiki yangu mmoja aliyeletewa shahada ya kughushi alipotoa wazo moja kali sana. Alisema ili kutumia shahada yake vizuri basi angeanza kujiita Kalumekenge Malisera Ewassa Kimdunge.

Mwanzoni sikuelewa mantiki ya kubadili jina. Kumbe ukiwa na jina kubwa na shahada kubwa hata kama ni ya kughushi unapata ulaji na hakuna mtu wa kukufikisha kwa pilato. Ingekuwa hivyo mbona wale jamaa waliotuhumiwa kughushi wangekuwa weshaozea Keko kama si Segerea? Haya tuyaache.

Nina miezi sita tangu nianze kibarua hiki almas. Nimeishapunyua njuluku namalizie hekalu langu kifungua mimba maeneo ya Salasala. Mchuma wa kukogea wachovu ninao tena mjapanizi. Akaunti yangu si haba. Ina mimba tena mapacha. Nina akaunti karibu kila benki hapa Bongo. Nyumba zangu ndogo zote nina mpango wa kuzijengea mabangaluu ya kukata na umma.

Uchovu una madhara yake sawa na kuukata. Tangu zinitembelee washikaji hawabanduki kila ninapokwenda kukata kilaji. Ninaandamana na msururu wa walaji utadhani name ni rais! Ama kweli siku Sir God akikurememba hakuandikii email wala kukubipu. Yeye anatwanga tu na unaona mambo yake. Ila tuache utani. Wakati mwingine heri huzaa shari kama shari iwezavyo kuzaa heri. Nisipokufa kwa ngoma au ulabu basi nitaishi hadi miaka 150.

Maana tangu zinitembelee nawabadilisha kama barabara. Pamoja na kutokuwa handsome, bado napendwa. Sijui napendwa mimi au pochi, hili kwa sasa halinishughulishi. Sasa hivi najinoma na vimwana kuliko hata jamaa yangu Lihumba wa Bunch of Thieves. Hata hivyo napaswa kutumia ili kuondoa mawazo kutokana na njia inayonipatia hii pesa haramu ya kuchuuza ndugu zangu.

Unaweza kuamini kuwa safari zangu siyo zile za Sumbawanga na Mbamba Bay. Siku hizi name napanda pipa kwenda kwa maza kutanua kinomanoma na dogo dogo zangu kama Njaa Kaya.

Name humua kujivuvumua kutuliza hasira zitokanazo na kutumiwa kufanya kazi chafu ya salata. Unadhani bila kulewa hii dhambi si itakunyotoa roho. Hivi ni roho ngapi zinaangamia kutokana na kibarua changu kipya cha kuruhusu bwimbi liingizwe kayani huku jamaa zangu magabacholi wakivusha dola kama hawana akili nzuri?

Nimesahau kuwapa mchapo mmoja wa neema zangu. Nina mpango wa kununua jumba Dubai ili kuwekeza huko. Mambo yakichafuka hapa naishia umangani na kwenda kujinoma kwenye mali zangu kama akina Dadi Balaaali.

Kituko cha mwisho, je ulimuona Vasco da Gama alivyokwenda kujinoma baada ya mibomu kudedisha walevi badala ya kutangaza lau siku moja ya kuadhimisha kikaya achia mbali kukaa matanga?

Naona pipa linatua toka Pakstani. Ngoja niwahi getini kupitisha shehena.

Kulaleki! Nimejikwaa!
Chanzo: Tanzania Daima Machi 9, 2011.

No comments: