Wednesday, 30 March 2011

Hii mitoto ya CCAM imenikera sana

WANAOKUMBUKA utawala wa kupigiwa mfano wa shujaa Hastings Kamuzu Banda pale Malawi, watakumbuka Chitukuko Cha Amai M'Malawi kilichoanzishwa na mistress wake kama alivyoitwa, Cecilia Kadzamira.

Baada ya Kadzamira kuwa karibu na mkuu, aliona ni bora kumtumia kupata ulaji. Hapa ndipo ilikuja filosofia ya Mbumba za Kamuzu, yaani wanawake wa Kamuzu kwa lugha nyepesi. Msishangae huyu kayapataje haya. Niliwahi kualikwa huko na Ngwazi mwenyewe ili kuona nchi zinavyoendeshwa mchakamchaka. Ilikuwa mwaka gani tusiulizane.

Acha twende kwenye mada ya mose wa lelo. Hivi karibuni kumetokea mchezo mchafu sana kayani. Mchezo huu usipouliwa mbali tutachenjiana huko tuendako. Hivi unajisikiaje unapomuona mke wa kijiwe au mwanae wakitanua kana kwamba nao ni wakuu?

Wanatoa matamko ya kisiasa wakitumia hata mishangingi na midege ya umma kufanya upuuzi wao! Nani aliwachagua na lini? Je, huu si ufisadi aina mpya ambao wachovu na walevi, sijui, hawajaustukia au wanaridhika nao!

Wakati kupe hawa walioko mgongoni mwa mkuu wakitanua, nao wamewakaribisha kupe wengine chini ya magenge mbalimbali, yawe ya umri au jinsia. Magenge haya yamejisahau kiasi cha kujifanya wenye zizi wakati yako mgongoni mwa ng’ombe. Je, kosa hapa ni la makupe tu au na wale wanaonyamazia ufisadi huu wa kimfumo?

Ingawa vita ya kunguru ni neema ya panzi, juzi sikufurahishwa na tamko la makupe waliotaka eti kulikumbusha lisirikali liwafunge midomo CHAKUDEMA kisiwaamshe wachovu na walevi kupamba na ufisi na ufisadi. Kama wengeshamubuliana wao kwa wao ningewaandikia nyimbo za kuwasifu. Lakini kuanza kuzuia ukombozi wa walevi wameniudhi sana.

Sitaacha kuwauliza kila mara. Mnaongea kama nani wakati ajenda yenu ni njaa na ufisi? Kagombeeni kwenye uchaguzi muone kama ni rahisi kama mnavyodhani hata kama mnatumia sayansi yenu ya uchakachuaji.

Ni ukupe kiasi gani jitu zima kudandia mgongoni mwa mtu halafu linajiona lenyewe ndiyo lenyewe.

Kilichonikera zaidi ni kuona hawa wadudu wakipayuka wakati wakilaumu wengine kupayuka. Kwani kupayuka vibaya kama unajua unachopayuka?

Bila aibu eti yanasema kuna wana genge wanaopayuka payuka mambo ya siri ya ulaji kwenye magazeti ya udaku. Eti makupe haya yanasema hawa jamaa wanyamaze yanyonye maana ni zamu yake kunyonya.

Mbona yenyewe yamekwenda kupayukia kwenye magazeti hayo hayo kama kweli siyo minyani kutoona mikalio yake?

Hii mitoto ya Chitukuko cha Amai M’ Bongolaland kimenikera sana. Nimekereka nusu ya kujifunga mabomu na kulipua mtu. Yaani Bongolaland imekuwa kaya ya vitukuko na vituko siyo? Leo CCAM. Kesho MAWA (Maualaji ya Washirika wa Bedroom wa Madingi). Jana Fursa Sawa kwa Wezi Wote (Equal Opportunity for First Thieves)!

Hawa jamaa wa Umoja wa Vikupe wa Chama Cha Mafisadi (UV-CCM msikosee na kuifananisha hii na UV-CCM ya chama tawala. Ni bahati mbaya vifupi vimefanana) wamenikera sana. Sasa natoa onyo. Wakiendelea na utaahira wao nitaenda zangu Kandahar kufanya mazoezi ya kuja kuwabinladen haraka sana iwezekanavyo kabla hawajavimbiwa. Maana naona wamekula wamelewa wamejisahau sana.

Kwanza, huu si wakati wa kuogopa mtu tena mtu mwenyewe wa kudandia madaraka ya mume au baba. Nawashauri CHAKUDEMA waendelee kudema, kutesa na kunema. Msiogope kitu wala mtu hata kama ni mtoto wa mkubwa. Utaogopaje wakati madevu Mureno Okampo yupo? Kwanza nilisoma naye na kufundisha naye sheria pale Chuo Kikuu cha Havard.

Hivyo, nikimtonya kuwa kuna majambazis yanataka kuhujumu demokrasia kwa kuanzisha ghasia atakuja haraka na kuwasukumizia lupango. Waulize manyang’au wa pale jirani wanavyohaha kumuepuka hata kwa kupiga kampeni za kimataifa za upuuzi.

Tena nimekumbuka. Ngoja nichukue fursa hii kuwalaani wale wapambavu waliotaka eti kuandamana kulaani majeshi ya Uropa kumpa kichapo Mlamali Kashafi. Eti mazezeta haya yanasema eti wanaoshambuliwa ni waislamu!

Je, hao wapinzani wa Kashafi ni wakristo kule Benghazi? Wangejua Kashafi mwenyewe anavyowakandia aliposema eti watu wanataka kumpindua ili waanzishe serikali za kiislamu, wasingefanya upuuzi huu tena mchana. Hapa uislamu uko wapi na kwanini uislamu?

Mbona hatuwaoni mkiandamana kumtaka Gbagbo Badboy akitoe baada ya kushindwa kuchakachua uchaguzi? This, if anything, is but double standard and megalomania. Samahani naongea kimombo kwa vile Mwenambago amepanda.

Kashafi mwenyewe mnayemtetea si muafrika kama mnavyodhani. Hivi hamkusikia hivi karibuni akiwaambia wamanga kuwa kuanzia sasa Libia si nchi ya kimanga bali ya kimakonde? Hii ni baada ya umoja wa wamanga kuruhusu Kashafi achapwe na watasha.

Bila shaka hawa ni al-Qaeda. Maana Kashafi anasema wapinzani wake ni maajenti wa al-Qaeda. Inaonekana hawa jamaa, kama UVCCM hawasomi magazeti.

Hawajui Kashafi alivyowanyea wapinzani wake kwa kuwapakazia kuwa ni al-Qaeda na wala unga walioghilibiwa kumpindua kiongozi mpendwa asiyependwa!

Hakuna watu walevi kama wabongolalalanders. Jana mlitaarifiwa kuwa uuzaji wa Seliteli umeiingizia Bongolalaland tobo la dola 308,000,000 sawa na madafu 500,000,000,000 hamuandamani. Mnaendelea kujikomba kwa akina Kashafi ili wawatupie rupia mbili! Je, nyie si mataahira?

Hamkuandamana kuwalaani Duwanzi na washirika wao wenye madaraka walipopanga kujilipa madafu 94,000,000,000 tena kwa kuwaweka kizani kama mimende!

Nani aliwaroga nyie walevi? Acheni ulevi mtaliwa mnajiona. Hata hivyo, sorry, nimekosea. Mliwe mara ngapi iwapo mnaliwa kila uchao usiku na mchana. Huko nyuma hamkuwa hivi sijui mmeingiliwa na nani?

Ngoja nivuke barabara kabla ya mataa kuzima hawa vichaa wa daladala wasijenigeuza past tense!
Chanzo:Tanzania Daima machi 30, 2011.

No comments: