Wednesday, 23 March 2011

Nini kitafuata baada ya Loliondo?

Hakuna ubishi. Ambilike Mwasapile sasa ni jina kubwa Tanzania. Hii ni kutokana na bwana mchungaji wa kanisa la KKKT kuwavuta wengi kutokana na kile anachoita “dawa” yenye kutibu magonjwa mengi yaliyoshindikana. Je anatibu kweli au ni ombwe letu la kufikiri? Ni mapema kutathmini. Yeye anadai alioteshwa na Mungu awatibu wenye shida. Kwanini sasa na si kabla?

Ingawa madai kama haya si mapya kwa watu wenye tabia ya kumtumia Mungu kupata mlo wao, kidogo ni ya ajabu. Je ni kweli Mungu ameona ukweli wa mambo kuwa watanzania ni wagonjwa na hakuna mamlaka zenye kuwapa huduma kuondokana na hili? Je kwanini Watanzania na si mataifa mengine? Je ni kwa vile watanzania ni wacha Mungu kuliko wengine? Je kuna namna ya usanii kama baadhi ya watu wanavyoanza kustuka? Je kweli kuna Mungu nyuma ya hili au ni kwa vile Mungu haonekani na hawezi kukanusha bali anatumiwa? Je hii ni kutokana na ukweli kuwa watanzania ni wepesi wa kuamini kila kitu? Maswali ni mengi kuliko majibu.

Kwa vile wengi wanaonyesha kuamini huduma za Mwasapile, hakuna jinsi ya kuweza kuwazuia wasiende au kuwastua. Maana ni uhuru wao kikatiba hata kama wanachoamini kisingekuwa na maana yoyote. Lakini pamoja na hilo, tujiulize. Baada ya sifa za babu kupungua na kuzoeleka, nini kitafuata? Je tushughulikie “magonjwa” na kusahau mengine? Tunauliza swali hili kutokana na kugundua kuwa kama nchi na hata jamii, tumetelekeza mijadala muhimu na bongo zetu na kujiingiza kwenye imani za ajabu. Je huu si ushahidi tosha wa ugonjwa wa jamii husika?

Kinachosumbua sana ni ukweli kuwa na watawala wetu wametugeuza wapuuzi kwa kujifanya wanashabikia tunachoshabikia kiasi cha baadhi ya wanasiasa kutumia fursa hii kujionyesha kama watu wema na wenye kutoa misaada! Je hii nayo si rushwa ya namna yake? Maana, wagonjwa hawana miiko. Hawawezi kuuliza hayo maelfu na hata mamilioni yanayotumika kusafirisha wagonjwa yamepatikana kihalali au kulipiwa kodi. Je huku si kutumia ujinga na matatizo ya wananchi kujipatia umaarufu?

Kila uchao tunasoma ushuhuda wenye kutia shaka wa “walitibiwa” na dawa ya babu. Je ni kweli wamepona au wengine wanatumia fursa hii kuendelea kutuzuga tusijadili hoja za muhimu kama kuendelea kuwekwa kizani au wanafuata mkumbo? Je baada ya ukweli kudhihiri, nini kitafuata? Je tutarudi kwenye kujadili masuala muhimu kama Dowans au kurukia kumshutumu na kumlaumu babu kwa kutuchelewesha na hata kutudanganya?

Ukiondoa Tanzania, hakuna nchi duniani unayoweza kuishawishi kuwa dawa za kuota zaweza kutibu ugonjwa kama Ukimwi ambao umeshindikana miaka mingi. Ni Tanzania tu ambapo mtu anaweza kuamka na kujiita Profesa, shehe, mchungaji, askofu na mamlaka yasifanye kitu. Nani atafanya nini iwapo wanaopaswa kufanya hivyo nao ni wasanii wenye shahada za kughushi japo si wote? Nani ana muda na masuala ya maadili iwapo fasheni ya tawala za kisasa ni madili? Kila mtu yuko bize na ugonjwa wake na hata babu yake na dawa yake! Kesho usishangae akatokea mtu akidai ameota ndoto kuwa katiba ibadilishwe na kuongeza muda wa mihula ya urais au hata kuvunja muungano.

Kwa vile tu jamii ya wagonjwa na wepesi wa kuamini, akitokea mtu wa namna hii atafanikiwa. Atashindwaje kufanikiwa iwapo kila siku unawasikia wapuuzi wakidai tuombee amani? Amani haiji kwa kuomba bali kutenda haki. Ajabu, wababaishaji hawa bado wanaitwa viongozi wa kiroho wakati ni viongozi waroho!

Atashindwaje iwapo tuna sifa kubwa ya kuwekeza kwenye umbea na imani za kusadikika? Ingawa kwenye uwekezaji mwingi kuna rushwa, kuna uwezekano kuwa wawekezaji wengi waliotuingiza mjini kama Richmond, waliwapata watawala wetu kirahisi kutokana na tabia hii ya kuamini kila upuuzi hata uwe wa wazi.

Sishangai ni kwanini uchumi wa Tanzania kwa miongo yote umekuwa ukimilkiwa na wageni hasa kutoka bara Asia. Sababu ni rahisi. Ni kuamini kuwa wenzetu wanajua biashara kuliko sisi wakati biashara yenyewe si nyingine bali kutumiwa na watawala wezi kuficha siri zao. Anayebishia hili akamuulize mzee Idd Simba ambaye licha ya kuwa mchumi na mwanasiasa mashuhuri, ana uzoefu wa kutosha. Alipoandika kitabu chake juu ya wazawa alikaripiwa na kunyamazishwa kutokana na kuwagusa pabaya watawala.

Tuhitimishe kwa kuuliza tena na tena. Je baada ya ukweli wa Loliondo kujulikana, kitafuata nini? Je Loliondo ni zaidi ya matatizo yetu sugu kama vile mgao, kulanguliwa umeme, ufisadi na ubabaishaji?

Chanzo: Tanzania Daima Machi 22, 2011.

No comments: