Wednesday, 30 March 2011

Kweli Makinda ni chaguo la mafisadi


Hakuna shaka kuwa waliofuatilia majibu na namna spika wa bunge Anna Makinda alivyohemka na kuchemka baada ya mbunge wa Arusha Godbless Lema (CHADEMA) kudai waziri mkuu Mizengo Pinda alidanganya bunge wamemjua Makinda ni nani?

Sijasoma ushahidi wa Lema. Ila nikikumbuka Pinda alivyoliambia bunge kuwa watanzania watatu waliuawa kwenye vurugu za Arusha, naona uongo wa wazi. Maana waliuawa watanzania wawili na mkenya mmoja kiasi cha Kenya kuja juu. Pamoja na kuwa Pinda aliongopa mengine, hili pekee lilitosha kupata karipio. Maana hata kuku wanajua kuwa waliuawa watanzania wawili hata walikozikwa kunafahamika, majina, jinsi, umri na shughuli zao. Je Pinda hasomi hata magazeti? Na Makinda je? Hili halikuhitaji digrii ya uchunguzi ua ubukuzi bali common sense kwa pande zote.

Hata hivyo tusimshangae Makinda. Maana wengi walishangaa kuona Makinda alivyochukia na kuchachamaa utadhani Pinda ni Mungu ambaye hapaswi kutenda dhambi. Walishangaa zaidi na kuuliza mantiki ya ukuu wa mhimili mmojawapo wa dola. Walikereka kuona mkuu wa mhimili unaopaswa kuwa mfano tena ukiitwa mtukufu kutumika kama nepi.

Alipoteuliwa kugombea nafasi ya uspika akitumika kumwengua Spika wa zamani, Samuel Sitta, wengi walishuku na kusema wazi kuwa alikuwa chaguo la mafisadi ili kumtimua Sitta wapitishe mambo yao.

Bahati nzuri au mbaya Makinda hakutoa majibu yanayoingia akilini kukanusha hili. Wapo walioenda mbali na kudai mmojawapo wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi wa kutisha aliyeko karibu na rais Jakaya Kikwete mbunge wa Igunga Rostam Aziz alimfuata na kumtaka agombee naye akakubali kugombea. Makinda hajawahi kukanusha hili kwa majibu yanayoingia akilini.

Japo rafu iliyochezwa kumchomoa Makinda kusikojulikana kwa kisingizio cha kuwafikiria akina mama ni historia, kwa wenye kumbukumbu hili halitafutika. Ndani ya nyoyo za akina Sitta ukweli ni kwamba Makinda ni tunda la uchakachuaji, udhalilishaji akina mama na hata ufisadi.

Kila mti utaujua kwa matunda yake. Taarifa kuwa Makinda alimlazimisha mbunge Lema kutoa uthibitisho wa uongo wa Pinda kuepusha malumbano ni za kusikitisha. Kwani Pinda si binadamu ambaye tena ameishaongopa mara nyingi tu? Rejea alivyojivuvumua kuwa atakomesha ununuzi wa magari ya bei mbaya bila kutoa namna atakavyokomesha hili na yakaendelea kununuliwa huku yeye akiishia kulalamika na hatimaye kuficha uso wake.

Hii inathibitishwa na kuja kwa Pinda na kile kinachoonekana kama madai ya ajabu- kukataa shangingi jipya na kushauri apewe mtu mwingine badala ya kulirudisha lilikonunuliwa. Ushauri wa namna hii licha ya kuwa wa woga ni wa hovyo. Maana waziri mkuu ndiye mwenye mamlaka ya kuamuru nini kinunuliwa na nini kisinunuliwe.

Hapa Pinda alionyesha udhaifu usiokifani. Nao ni uongo. Wapo wanaoona: kushindwa kutumia wadhifa wake na kuishia kulalamika na kususa ni kuongopea umma kuwa anafaa wakati hafai.

Rejea usanii wa Pinda wa kutoa amri magari ya umma yasitumiwe nje ya ofisi na saa za kazi. Mbona juzi yameonekana Loliondo kwa babu yakifanya shughuli binafsi na hajasema lolote?

Taarifa za ijumaa ya tarehe 11 mwezi huu ni kwamba Makinda amekataa ushahidi wa Lema zinazidi kumfichua Makinda na waliomsimika hapo alipo kwa faida zao binafsi.

Turejee kwa Makinda. Hivi karibuni alikaririwa akisema, “Lema aliwasilisha vielelezo kimaandishi kama Bunge lilivyomtaka, kuhusu hatua gani atachukuliwa, hizi ni taratibu za ndani siwezi kuziweka hadharani,

Makinda anamaanisha nini anaposema hataweka hadharani hatua atakazochukuliwa Lema zaidi ya kuishiwa? Je kama ataadhibiwa kwa siri Lema atawaambia nini wananchi waliomtuma kuwawakilisha? Je Lema atakubali uhuni huu? Kwanini suala la umma,. tena lililoibuka hadharani mbele ya bunge, ligeuzwe la chumbani? Hili si suala la mke na mume bali la umma ambao ungetaka kuona ama Lema akiadhibiwa kwa kumsingizia waziri mkuu au waziri mkuu akiwajibika kwa kulidanganya bunge.

Hata kama Pinda hatawajibika au kuwajibishwa kutokana na serikali ya sasa kutokuwa na ustaarabu huu, angalau umma utajua mbivu na mbichi.

Kuficha utatuzi wa suala la Lema-Pinda-Makinda ni ushahidi tosha kuwa nchini hatuna utawala wa sheria bali ubabaishaji mtupu ambapo kikundi kidogo cha watu kinaweza kuuteka umma na kujifanyia kitakavyo kama ambavyo Makinda anadhamiria kufanya. Tusiruhusu uhuni huu. Makinda anataka kulidhalilisha bunge kwa maslahi ya mtu mmoja. Je wabunge nao watakubaliana na uhuni huu?

Kwa majibu ya Makinda, unapata kujua asivyofaa kiasi cha kuamini shutuma kuwa alipendekezwa na mafisadi ili kulinda maslahi yao. Kama tunamzushia basi atupe msingi wa kuingilia uhuru wa mbunge na kuminya haki zake hata anapoleta ushahidi mzito.

Bunge ni mali ya wananchi. Linapaswa kuendeshwa kwa sheria, viwango na taratibu na si mapenzi ya mtu au kundi la watu.

Isitoshe uspika ni cheo na si utukufu wala kuwa na thamani kuliko wabunge na watu wengine. Kuna haja ya kumbana Makinda atende haki na ikishindikana zifunguliwe kesi za kumtaka aachie ngazi kutokana na kutaka kuligeuza bunge biashara binafsi. Nawashauri CHADEMA, kuliongeza hili kwenye ajenda yao ya kuwaambia wananchi uchafu wa CCM ambao umegeuza maisha yao kukosa maana na kuwaongezea mateso kwa ajili ya kulinda genge la watu wachache.

Makinda asipokuwa makini, ataondoka pale amechafuka zaidi. Kwani uteuzi wake licha ya kuwa udhalilishaji wa akina mama, utaonekana kuwa machukizo hata kwa wanawake wenyewe. Maana haiingii akilini kwenye nchi yenye katiba inayoharamisha ubaguzi wa aina yoyote mtu kuchaguliwa kwa jinsia yake. Ingawa hili lilipoibuka Makinda alikaa kimya, kwa haya madudu anayofanya aamini asiamini baadaye ataumbuka.

Tumalize kwa kumpa ushauri Makinda asome alama za nyakati. Maana kuna kesho na hakuna kisicho na mwisho chini ya jua. Je kwa matendo ya Makinda tumuweke kundi gani?
Chanzo:Tanzania Daima Machi 30, 2011.

2 comments:

chib said...

Ndugu, tumeusoma uchambuzi wako barabara

NN Mhango said...

Ndugu yangu Chib, shukrani kwa kusoma uchambuzi wangu na kutoa maoni yako japo mafupi.