How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 2 March 2011

Misri wana neema hawamtaki Mubarak, Tanzania mmelogwa?

BAADA ya kushuhudia maandamano ya kuangusha wezi wenye madaraka huko Maghreb, nimeanza kufanya utafiti juu ya hulka na tabia za watu duniani.

Nilifikia hitimisho hili baada ya kushuhudia Hossein Kibaraak akidondoshwa na nguvu ya umma pale Masri huku Mwamali Kashafi akizidi kugeuka kuku alaye mayai na vifaranga vyake.

Yule shujaa tuliyemzoea katoweka zamani gani! Nafasi yake imefichua shetani anayeweza kutumia madege ya kijeshi kumaliza watu wanaodai haki na heshima yao! Kweli madaraka yanaficha mengi nimegundua.

Katika utafiti wangu nimegundua kuwa kumbe nyuma ya sura nzuri kunaweza kuwa na ukatili na ubaya vya kutisha! Hii ndiyo siri ya watu wenye tabia ya kuchekacheka kuwa na tabia tofauti nyuma ya pazia. Ni wakatili hakuna mfano.

Kwa kimombo watu wa sura kama Kashafi huitwa flamboyant au warembo, tuseme. Ila ukiwachunguza, si warembo kitu bali maharamia waliofunikwa na bashasha.

kitaka kujua nimaanishacho hebu angalia sura na hulka za wezi wa Dowanis. Most of them are beautiful if not flamboyant. But in actual fact they are but vampires.

Lo! Samahani kwa kumwaga ung’eng’e. Hii imesababishwa na mwenembago na si kujidai ili mjue nimesoma. Najua: mnajua nimebukua. Sijafoji kama wale wasoheshima vihiyo waliotuhumiwa kughushi wakanywea na kuthibitisha kuwa kweli walighushi kuanzia kura hadi shahada.

Wako madaktari wengi vihiyo walioghushi tena bungeni na kabitenini. Hata pale Site mkuu wake mpya ni kihiyo aliyeghushi. Muulize Bachelor yake aliipata wapi.

Sasa tuachane na gendaeka wachache. Tuangalie umma ambao nimejipa kazi ya kuutafiti na kutoa matokeo ili yatumika kusaidia kuleta ukombozi.

Kwa utafiti huu wa kisayansi nimegundua kuwa nami ni sehemu ya mapinduzi matakatifu yatakayofuata baada ya watu kujua udhaifu wao. Isitoshe ni juzi juzi nilikwa Benghazi, Tobruk, Sabha, Kuffra, Ghadames, Berdi na kwingine kwingi.

Maana nilikwenda kule kuwashauri njagu wasijiingize kwenye kulinda maiti inayonuka na kujiletea aibu na dharau bure toka kwa umma. Nashukuru Subhanna wengi walinisikiliza na kutia akilini hadi wakamuasi jamaa. Hata wale marubani waliogoma kushambulia waandamanaji nilikuwa nimeongea nao siku moja kabla ya kitendo hiki cha kishujaa na kizalendo.

Najiuliza. Wangekuwa mandata wetu hata magesi yetu hovyo wangeweza kufanya hivi wasiogope kuwakasirisha mabwana zao wanaowafuga kama mbwa? Ila ukiondoa wakubwa wao, ukiwachunguza wa chini ni makapuku kuliko hata walevi wenyewe lakini bado wanatumika na wasijijue. Jamani amkeni kwani nanyi mnaliwa. Muulize Nyangenyange na Shimboshimbo. Wataanza kukutisha utadhani si kweli!

Nimegundua: wamanga wakipatwa na ukosefu wa kazi hawajiingizi kwenye umachinga au udokozi wa mali ya umma kuganga njaa. Wanaingia mitaani kinaeleweka. Waswahili, kwa upande wao, ni tofauti. Wanafanya nini? Kila mmoja anajua.

Nimegundu wamanga, japo wanalalamika umaskini, ikilinganishwa na wenzao walevi wao wana nafuu tena sana. Nilishuhudia Cairo umeme ukiwaka masaa 48.

Pamoja na kutokuwa na vyanzo vya maji kama vyetu, hawajui neno mgao au ulanguzi wa umeme wala maji. Nilipowaambia kuwa kayani kwangu umeme ni ishu walinishangaa na kuuliza kama wanakaya wa kaya yangu ni watu au mbuzi.

Nimegundua pamoja na watawala wa kimanga kuwa wezi, kwa kiasi fulani wana nafuu. Wana angalau maadili ya utawala siyo haya Madili ya watawala ninayoona uswahilini.

Kitu kimoja wamanga walivumilia na sasa wameamua kuachana nacho-kutawaliwa kwa muda mrefu huku wezi wao wakila kwa muda mrefu mikono na miguu bila kusali wala kunawa.

Gonjwa jingine lililowachelewesha wamanga ni kujuana. Kila rais alikuwa anataka kumrithisha mwanae urais asikue urais ni wa umma. Wao wanatawalana kwa makundi ya kikabila tofauti nay a kifisadi kama ulevini.

Kitu kimoja wezi wa kimanga walijua. Hawakuacha wanakaya wao wawe makapuku kwa kuwupuuzia, kuwanyonya na kuwadhalilisha kwa kiwango cha wamakonde. Walihakikisha bei ya mkate, umeme, petrol na mahitaji ya muhimu na lazima inakuwa ya chini huku wakijitahidi kuwajengea watu maskini majumba ya kuishi.

Juzi nilicheka nusu kunyotoka roho. Nilicheka pale imla wa Saudia aliporejea kutoka kwenye matibabu na kumwaga zaidi ya dola 35,000,000,000 kwa wanachi wake ili wasimbarake au kumgadafi. Je hili ni jibu?

Maskini hajui kuwa kwa kumwaga kitita hiki amethibitishia umma kuwa kumbe anazo na hivyo watazidi kumdai zaidi. Hata utoe pesa kiasi gani, huwezi kununua uhuru na haki za watu. Huwezi kununua haki za binadamu wala demokrasia.

Je huku si kutapatapa? Heri mfalme anazo za kuwahonga wananchi wake. Je wale niwajuao watahonga nini iwapo wana uroho na akili kama panya? Watahonga nini iwapo wachukuaji walishachukua kila kitu?

Nimegundua wamanga ni wajanja. Hawaogopi kupigwa risasi wala kumwagiwa upupu na kudondoshewa mibomu ya michozi. Mswahili anaishi kwenye zizi na bado anaendelea kuaminishwa kuwa hayo ndiyo maisha bora.

Kwa wale wenye nyumba za maana walio wengi wanatembea na suto la wizi nyoyoni mwao. Kwani wamezipata kifisadi hadi wengine hata kutotaka zijulikane kuwa ni zao kama mimi ilivyonitokea kule G’Mboto hivi karibuni.

Hata hivyo nisiwalaumu sana walevi. Ulevi umewamaliza akili kiasi cha kutenzwa kama wanyama hasa kondoo ambaye waweza kuchinja wakati wowote na asifurukute.

Kuna swali linanisumbua sana. Tunisia wako milioni kumi lakini wana akili kuliko wabonglalalanders milioni zaidi ya 40. Anayebishia hili aniambia wabongolalalanders pamoja na wingi wao wamefanya nini la maana zaidi ya kuzidi kuishi kizani kama kupe, mende na panya? Jaribu hili kwa watunisia au wamasri uone.

Masri kuna barabara nzuri, umeme ni twenty four hours, maisha ni nafuu ikilinganishwa na wabongolalaland lakini bado wamemtimua kibaraak.

Najiuliza wangekatiwa umeme au kuibiwa njuluku kama hizi wanazolipana kidowans dowans si wangemnyotoa mtu roho? Wangekuwa wanagawiwa giza badala ya umeme hali ingekuwaje? Bila shaka kungechimbika bila jembe. Bila shaka kusingetosha hata kwa wiki moja.

Ngoja niwahi taarifa ya habari nisijeikosa fursa ya kumuona Mwamali Kashaffi akiburuzwa mitaani na kuchapwa bakora baada ya kuangushwa. Nanyi wangu make mkao wa kuliwa. Du kumbe ni kweli! Khalas kweis Intahabib yuuni.
Chanzo: Tanzania Daima Februari 2, 2011.

No comments: