Wednesday, 16 March 2011

Njoo kwangu msiende Loriyondo

MUNGU anatupenda hasa walevi Eimeeen. Bongolalaland imebarikiwa kupata tabibu asiye na kifani dunia nzima, Amiin. Baada ya kutokewa na God na kuniamuru nianzishe dhehebu la The Holiest and Highest Mighty Tarbenacle (THHMT), nimeamua kutoa huduma ya utatuzi wa matatizo mbali mbali bure.

Kuna wahuni wamelipa jina la utani dhehebu langu tukufu lililodhamiria kuondoa matatizo ya walevi. Wanaliita Tuamke Haraka Haraka Matatizo Tuondoshe. Kwa kiasi fulani hawajakosea. Maana dhehebu hili ndiye mkombozi wa pekee awezaye kuwafikisha walevi kwenye nchi ya ulabu na bangi bila wasi wasi baada ya wasanii kuwaahidi hili wakaishia kuwauza utumwani mwa wachukuaji, wachakachuaji na mafisadi. Tuachane na haya ya watani.

Seriously, nimejitenga na wivu, chuki na njaa kama Zaa-kalia Ka-Tortoise ambaye amenukiliwa akilalamika kuwa usanii wake umekosa walaji baada ya kuibuka kwa babu. Babu kakonga roho yangu kuwafichua matapeli wanaomtumia Mungu kuwaibia walevi. Mie nasema wazi. Simchukii babu. Maana wajinga ndio waliwao. Akinipiku kwa kuvuta umati wa wachovu, sitalalamika bali kwenda kuuza nyanya.

Mimi ni tofauti na hawa waota ndoto. Nimemuenga God kwa maninga yangu mawili. Hivyo, tiba yangu si ya kubangaiza wala nini, niaminini.

Baada ya kuona watu hasa vigogo wanavyohenyeka kwenda Loriyondo na ugogoro na utata uliojitokeza kutokana na tiba wanayofuata kule, hatimaye, God amesikia kilio chenu.

Amenituma niwasaidieni. Msiulize tuliongea au kukutana linin a wapi. Hili haliwahusu. Amenipa mamlaka niyatumie lau kujipatia raha hata senti kidogo nikitaka.

Vigogo msiogope kuja kwangu. Hata kama mmeishaikanyaga miwaya nitatunza siri zenu ilmradi tukatiane chochote kitu. Mie siruhusu mle peke yenu ndiyo maana God amenituma kwenu.

Nimeamua kutibu matatizo yote ili kuwaonea hasa huruma vigogo ambao wameonekana wakihaha kwenda kule. Anwani yangu ni simpo. Alhaj, mtakatifu, maulana, nguli, gwiji,mchunaji, sorry mchungaji wa wachungaji, daktari wa madaktari, shehe wa mashehe, mtakatifu Mpayukaji Msemahovyo mjukuu wa mzee Waambie Waelewe, MB, MBA, MSc, DM, PhD, DD, LLD, MPHDM, kwa Mfugadog Bongo, Bongolalaland.

Mnaziona shahada zangu? Si za kughushi. Mie nimesoma sana na si mchunaji bali mchungaji wala si shehena bali shehe.

Mungu amenipa karama hii baada ya kugundua kuwa wabongolalaland ni wagonjwa wa roho, akili na mwili. Hivyo aliona ni bora kumtafuta mtu muadilifu na mwelevu kama mimi.

Mimi siyo kama wale matapeli wanaojivisha uchungaji na ushehena wa kujipachika na uombezi wa kuibiana na kuhadaana. Mimi sitibii njaa wala kutaka sifa. Situmii luninga, magazeti ya udaku wala radio kutangaza huduma yangu. Pia ninayo dawa ya kuzuia TAKUKURU kukukamata hata ukichukua kitu kikubwa. Nina zindiko la kuwazuia walevi kukustukia unapowaliza.

Mie si mpenzi wa kujisifu. Mimi ni kama brigedia Al Adui wa Duwanzi, sipendi sifa. Ila ukweli ni kwamba ni mimi yule yule aliyewapa zindiko kina Dowans, Kagoda, Richmond, IPTL, Net Group, EPA, Zumbe wa mauaji ya Kirosa na wengine wengi tu.

Mjapo kwangu mnatoka ukiwa kile Wajapani huita shin Jin Rui au viumbe wapya. Mie silazimishi uwe na imani. Wala sitaki uwe na kile wahindi huita satyagaraha. Uje ukiwa dasht e kavir au dasht e lut (chumvi au mchanga) mie nitakutibu uwe binadamu. Samahani kwa kuongea kijepu na kigabacholi. Nimewahi kuishi kule. Au niongee kihawaii?

Anyway, mkitoka kwangu mtakuwa wapya na kuambiana heri ya mwaka mpya au Hau'oli Makahiki Hou. Nasema “Uyavutha Umlilo” kwa wale ndugu zangu wazulu au moto wawaka; mtakuja. Tuachane na lugha za watu.

Natenda miujiza ambayo haijawahi kutendwa na yeyote popote juu ya nchini, chini ya bahari na angani. Kwa mfano, nina dawa ambayo ukiinyunyizia nyumbani umeme unawaka na unaepukana na kulanguliwa na Tanidowanesco.

Natibu ukimwi, umaskini, mgao wa umeme, ugumba wa aina zote hata wa mawazo, hofu, matatizo ya kupata mume, kuongeza upendo, kuondosha nuksi na mikosi, kushinda uchaguzi, kukinga maandamano, kuzuia kuvunjika kwa amani, msongo wa roho, presha na chuki dawa hiyo moja.

Nina uwezo wa kuongeza uwezo wa kufikiri, kujiamini, kuridhika, kuvumilia hata kama unaliwa, kuona visivyoonekana na kupanua utajiri.

Pia natibu magonjwa ya migawanyiko, mitandao, msongo wa mawazo, kuzuia kushitakiwa ukighushi vyeti, kuzuia kustukiwa ukichakachua iwe pesa au uchaguzi na mengine kama hayo.

Kuhakikisha praivesi (faragha) yenu inatunzwa, nitatibia vigogo na akina mama uani na chumbani. Nifafanue.

Vigogo wa kiume nawatibia uani na akina mama wawe vigogo au la natibia Guest House. Hili ni sharti nililopewa na God. Najua bila kutoa maelezo mtaanza kuguna na kuuliza kunani.

Kwa akina mama, kama una sura mbaya au ni mzee utatibiwa na vigogo uani. Kama ni kidosho, nimeagizwa nikutibie Guest House ili kuondoa nuksi. Nadhani naeleweka. Pia tiba hii lazima ifanyike usiku kizani ili shetani asiweze kukuona na kukuweka alama na kulipiza kisasi.

Sababu nyingine ya kutibia uani ni kuepuka wezi kuiba teknolojia yangu, pia kuhakikisha wadaku wa magazeti na runinga hawapati picha za vigogo wanaoumwa hasa Ukimwi na ufisadi na kuwaanika. Pia akina mama wazee hawaogopi kiza ni watu wazima.

Wanafunzi hasa wa vyuo vikuu wanaotaka kupata mikopo haraka na kushinda mitihani yao waje kwangu haraka. Wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji wanaohofia mikataba yao au ukwepaji kodi wao kugunduliwa na kushitakiwa hata kufilisiwa njooni haraka.

Wale walioshindikana yaani ambao wanahisi hawawezi kuolewa au kuzaa waje haraka. Wanasiasa hawana haja ya kwenda Bwagamoyo kwa mambo ya uchaguzi. Waje kwangu watashinda hata kama hawana sifa. Chama kinachotishiwa kunyang’anywa ulaji kifanye haraka.

Sitaki niseme mengi. Nadhani mmeona ukweli wangu. Hivyo nategemea mtamiminika kwangu badala ya kwenda Loriyondo.

Wajinga ndio waliwao. Naona kinokia kinalonga. Huenda wameanza kujiingiza. Haloo profesa mtakatifu hapa!

Chanzo: Tanzania Daima Machi 16, 20011

2 comments:

Jaribu said...

Inakatisha tamaa. Wakati mwingine nilikuwa nasema ni uchakachuaji ndio umeirudisha CCM madarakani, lakini nikiangalia hao waliopiga kura wenyewe wanazugwa na khanga na fulana. Na ndio hao hao wanaofurika kwenye ujinga huo wa Babu. Sasa ikiwa basic biology yenyewe ndiyo shida, issues ambazo ni a bit more complex sijui itakuwaje? Ndio maana CCM iko mbio kuwapatia usafiri na traffic control.

NN Mhango said...

Jaribu you are dead right. Watu wetu ni kama popo kwa sasa. Hawana tofauti na bendera lijapo suala la upepo. Kama popo wakiona kuna ulaji sehemu au kudhania kuna nafuu hukimbilia kule wanapohitajika ndege. Upepo ukigeuka wakasema ni zamu ya wanyama, popo hawa hukenua ilmradi wapunguze matatizo ingawa nayo hayapungui zaidi ya kuongezeka.