Friday, 6 February 2015

Hata kuapisha washindi nongwa!

 
Baada ya kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao bila shaka umekula fedha nyingi tu, wengi walidhani watawala lau wangetenda haki na kufanya mambo yanayoingia akilini. Lakini ni bahati mbaya kuwa hali haikuwa hivi hasa baada ya kufanyika uchakachuaji wa nguvu na si kama ule wa kificho tuliozoea. Mengi tena ya kutia aibu yametendeka.  Wapinzani wamehujumiwa kama kawaida na kipindi hiki.  Hujuma imefanyika mchana kweupe hadi kuzaa utamaduni mpya ambao, kwa bahati mbaya, watawala wetu hawataki kuukubali wala kuuelewa.  Kwa mara ya kwanza, mwenyekiti wa mtaa ameapishwa na wakili wa kujitegemea badala ya wale waliopaswa kumwapisha. Je ni kwanini hii ilitokea? Kuna sababu kuu mbili, kwanza, shinikizo la wananchi kutaka waliyemchagua aapishwe kuepuka kuchakachuliwa au kuporwa kiongozi wao. Na pili, ni kutokana na wahusika kugoma kufanya hivyo huku wakitoa visingizio visivyoweza kumshawishi hata kuku. Tatu, wananchi wametoa tamko kuwa sasa wamebadilika na hawakubali kuchezewa hasa kura na chaguo lao.
  Baada ya kuapishwa kwa Mwenyekiti wa mtaa wa Mtaa wa Migombani – Segerea Japhet Kembo, vimetoka visingizio vya uongo na ukweli toka kwenye halmashauri ya wilaya ya Ilala. Wakati haya yakiendelea, habari kutoka Rombo Kilimanjaro zinapasha kuwa wapo washindi, bila shaka, toka upinzani ambao hawakuapishwa eti kwa vile ofisi ambazo wanapaswa kuzitumia ni za CCM! Upuuzi mtupu. Ofisi zote nchini ni mali ya watanzania na si vyama. Hivyo sababu kama hizi ni za kitoto na hazijengi bali zinabomoa demokrasia na kuwachochea watu kujichukulia sheria mikononi.
Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Segerea, Gango Kidera alikaririrwa na vyombo vya habari akisema “Endapo kutakuwa na utata wowote utakaojitokeza baada ya mwenyekiti na wajumbe wake kuanza kutekeleza majukumu yao, basi nguvu ya umma itatumika kuamua hatma ya hali hiyo, tutaandamana na wananchi wanasubiri kuona hilo linatokea.” Hili si tamko lelemama wala kupita. Licha ya kuonyesha uimara na mhusika kujua anachofanya, linaonyesha wazi wananchi wamebadilika na wamechoka na mizengwe. Ni vizuri watawala wakapokea ujumbe huu na kuufanyia kazi badala ya kuukejeli kama ilivyotokea baadaye ambapo  mbunge wa jimbo la Segera Makongoro Mahanga aliukejeli kwa kusema, “Ni woga tu ndiyo unaowasumbua kwasababu jina langu ni kubwa sana huku Segerea ndiyo maana wanaweweseka.”  Kama si kutapatapa, hapa jina kubwa ua dogo linaingiaje? Hapa ugomvi wala tatizo si ukubwa wa jina bali uapishwaji wa viongozi walioshinda kwenye uchaguzi basi. Huyu anayekuja na kujenga hisia na maadui wa kupapasa hajitakii mema wala hao wakubwa zake. Watu wameishachoshwa na kukatishwa tamaa na jinai ya uchakachuaji. Mkiendelea kuwaibia na kuwakejeli mnaweza kujikuta pakanga bila kutarajia.
 
Ni makosa na ujinga kuona kuwa kitendo cha wananchi kujiapishia kiongozi wao ni kuvunja sheria au cha woga. Kilichofanywa na wananchi wa Segerea ni ushahidi kuwa sasa wamechoka na wako tayari kwa lolote kuhakikisha wanatendewa haki. Hawa si woga wala wajinga hata kidogo. Na anayewadharau au kuwaona kama woga au wanaotapatapa basi anajichimbia kaburi bila kujua. Kama wameanza na mwenyekiti wa mtaa ambaye kisiasa kwa watu kama mawaziri wanaweza kumuona ni mtu mdogo, asishangae siku moja wakamwapisha mbunge wao hata rais ikibidi. Ukisikia mabadiliko na mwamko ndiyo hivyo.
          Mawazo na hisia za wananchi wa Segerea vinawakilisha watanzania wengi sehemu mbali mbali waliochoshwa na dhuluma hasa uchakachuaji. Huu unaweza kuwa mwanzo tu. Maana dhuluma imetamalaki nchini huku wanaoitenda wakifanya makosa kuwa watanzania hawawezi kubadilika utadhani wao ni mawe.
Kitendo cha kukodisha wakili si cha kitoto wala woga. Kwanza, wahusika wameonyesha kuijua sheria kiasi cha kuitumia bila woga. Sijui kama wakili aliyekubali kufanya hivyo, angewaridhia ilhali akijua anavunja sheria.          Wanachoonyesha akina Makongoro ni ujinga na kujiridhisha. Hata hivyo, kwa wanaojua tuhuma ambazo alishindwa kuzikanusha za kughushi shahada, wanaposikia anayosema hawamshangai. Hayo ndiyo matunda ya elimu ya kughushi inayomnyima mwenye kuighushi uwezo wa kuchanganua na kupembua mambo vizuri na vilivyo. Na ni bahati mbaya wengi wa waliojaa serikalini ni wa namna hii. Hawana uwezo mzuri wa kupambanua mambo hata wale wanaoonekana kusoma kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Profesa Anna Tibaijuka kujifanya asingeachia ngazi na kama kinachoendelea na Profesa mwenzake Sospeter Muhongo ambaye anaendelea kung’ang’ania ofisi ya umma asijue cheo ni dhamana. Wasomi wenye utata au walioshindwa kuelimika kama hawa unategemea waishauri nini serikali zaidi ya kuipotosha?
          Sheria ya uchaguzi inaruhusu kufanya hivi na hata hao wajumbe wawili ambao hawapo kwa leo watakaporudi nitawaapisha, ni suala la kutaarifiana tu,” alisema Idd Msawanga aliyemwapisha Kembo.

          Sababu kubwa iliyotolewa na waliokataa kuwaapisha viongozi waliochaguliwa na wanachi ni kwamba, kuna pingamizi toka CCM. Hata kama kuna pingamizi, halihusiani na uapishwaji. Maana hata kwenye ubungu mtu anapotoa pingamizi, hakuzuii mshindi kuapishwa. Kama kunakutikana kukiukwa sheria, matokeo husika hubatilishwa na mahakama na uchaguzi mdogo hufanyika. Hii ndiyo sheria, ndiyo ukweli na ndiyo utaratibu. Haya mengine ni usanii tu. Segerea na kwingineko wana haki ya kuwa na viongozi wa kuwahudumia bila kujali kama kuna pingamizi wala nini. Kwanini pingamizi linakuwa issue inaposhindwa CCM? Lingekuwa limewekwa na wapinzani unadhani kuna ambaye angesitisha uapishwaji eti kwa vile kuna pingamizi? Wakati umefika kuwaambia CCM kuwa hakuna cha milele. Wakati wao kuanza kujiandaa kuachia ngazi umefika. Wafanye hivyo bila kutubughudhi na ujinga na upendeleo kama ilivyotokea Rombo na Segerea.
Chanzo: Dira,

No comments: