Saturday, 7 February 2015

Wakati wa kuwatafunana umeanza


          Wakati wa kuhadaana, kutumiana, kulana na kugeuzana mabunga unaanza. Kiranja mkuu aliyepo anafungafunga virago kuwaachia wengine ulaji wa dezo. Hata bi mkubwa atakuwa na kibarua cha kuzurura huku na kule kusaka mshiko kabla ya kampuni sorry Ngo yake kuanza kudoda kwa kukosa wachangiaji baada ya kuachia ulaji. Trip za ughaibuni za mara kwa mara ndiyo usahau kabisa. Tunangoja walaji wajao tuone nao watakula kwa staili ipi. Tunangoja kusikia jina la kampuni sorry Ngo ya bi mkubwa ambaye lazima ataanzisha ili kuchanganya mshiko na kuwa milionea bila kutoa jasho. Unacheza na kura ya kula nini?
          Wakati wa sandakarawe?  Amina. Mwenye kupata? Apate.  Na mwenye kukosa?  Akose, ndiyo unaanza. Wanaojipitisha kutafuta ulaji wanajifanya wakarimu wakati kwa miaka mitano hawakuonekana karibu na wachovu walipokuwa. Wala huu ukarimu wao uchwara wachovu hawakuuona. Ni ukarimu au ulimbo? Walikwina? Nasikia alikwina mwenyewe amesema mwaka huu haingii kwenye debe. Sijui ndiyo hayo mambo ya urahisi au ndiyo hivyo zake zimeisha? Aende zake salama. Eshatuhujumu kwenye mjengo. Tuachane na alikwina.
          Ngoja turejee kwenye mtafunano na mtumiano na mdanganyano.
Leo wasaka tonge kupitia siasa wanakuja na aina mpya ya upendo na ushirikiano urafiki na ukaribu ili wapate kura ya kula. Ila wakiishainyaka mjue ndiyo imetoka. Wataanza kuzungukwa na mabausa, ma-bodyguard na upuuzi mwingine kuogopa msiwaibie wala kuwadhuru. Hivyo, mapenzi na ukarimu mnavyoonyeshwa ni vya msimu tu wa ulaji. Mkishatoa kura mjiandae kuliwa japo mlitegemea kula.
          Kwa upande mwingine wachonga maneno wameishaandaa visu vyao yaani kalamu. Kwa lugha ya kijiweni hii tunaiita kubagending kama siyo kurweyependekezingimu. Kwa lugha rahihsi ni kwamba waandishi nyemelezi hugeuka kile ambacho sis wana falsafa hupenda kuita nepi  za wale wanaowatumia kuwachafua wenzao au kuwapamba wakati ni uchafu mtupu.
 Wapo walioanza kutunga vitabu huku wengine wakiandika makala za uongo na ukweli kuwauza kuwasifia au kutaka wale wanaotaka wawatoe ulaji wapiti ili nao walipwe fadhila. Kalama iliyopaswa kuwa silaha ya ukombozi, msimu huu, inageuka silaha ya usaliti na uchangudoa wa kimaadili ili wahusika wapate madili.
          Niwaonye nyemelezi walioamua kutumia matumbo yao badala ya vichwa.  Ukishatumiwa unatupwa kama ganda la muwa. Ukishajulikana, hata kama utalipwa fadhila, unageuka changudoa milele anayeweza kujiuza ili mradi apate atakacho. Kama umejiingiza kwenye mchezo huu mchafu uhakikishe unapewa chako mapema. Maana wanaokutumia ukadhani unawatumia wanajua kuwa huwapendi wala huwafai bali kula vyao. Waandishi wengi watajiingiza kwenye huu mchezo wa kujidhalilisha, kujichafua, kuwachafua wengine na hata kusaliti taaluma yao wakitegemea kuula, mtauzana wataula wachache kama wale nepi aliowatumia jamaa yetu anayetimka. Kwa hiyo wale wanaotegemea kuukwaa ukuu wa mikoa au wilaya hata usemaji kwenye ofisi ya rais wafikiri mara mbili. It is not that easy. Many’ill be called and a few will be designated even though it is a filthy game. Samahani, nimechanganya lugha kutokana nakurejea juzi toka Londoni kwa maza.
          Wengi wa nyemelezi watumiwa wanategemea kuwa kama silvia au Mihingio Rweyependekeza. Kitaalamu huu huitwa uchangudoa wa kimaadili ambapo mtu na taaluma yake hukubali kugeuzwa nepi na mwenzake jambo ambalo halina tofauti kwa upande wa aibu kama kushikishwa ukuta. Wanaotegemea ukuu wa wilaya au ulaji kwenye ofisi za wakubwa wajue wanacheza kamari. Wengi wataitwa na kutumiwa lakini watakaolipwa fadhila ni wachache hata kama fadhila yenyewe ni mabaki ya vyeo au upendeleo. Waulize akina Purinsi Baggenda.
Wachovu waliokuwa wamechoshwa na mataputapu ni wakati wa kujienjoi na bia na ulabu wa maana wanywao wakubwa.
          Viongozi wa dini wakae mkao wa kula. Wale wote waliokuwa wamemwasi bwana godi sasa wataingia kwenye majumba yake ili waumini wawaone, wawajue na kuwapa kura ya kulia. Baada ya hapo? Pray back the devil to hell ndugu zanguni.
          Kila kitu ni raha kwenda mbele. Huu ndiyo wakati wa mwaka mpya kwa wachovu ambapo kila raha lazima waipate ingawa wakishavuka uchakachuaji watatelekezwa kama siyo kutupwa kama vile vichanga vitupavyo na dada zangu wanaofanya mambo bila kupanga wala kufikiri. Watahongwa upuuzi kama ulabu, makulaji, fulana, khanga hata njuluku kiduchu. Wahongaji wakishapata wanachotaka wanawaacha wahongwaji na umaskini na ujinga wao na kwenda kuhomola mjini.
          Kwa sasa kila mtaka kula na mtoa kula wako sawa. Hawabaguani wala kuogopana. Ila wengine wakishapata wanachotaka yaani ukubwa, wanaanza kujifungia mofisini wakihimiza makatibu mhutasi wao kutoruhusu wachovu wanaokwenda kuwaghasi huko kwenye ulaji.  Kwa wale waliojizungushia mabaunsa na mabodi gadi, ukimkaribia, ukiwa na bahati wakusukume au kukuvunja mbavu kama si kukupiga risasi au kuamru ndata wakusweke ndani kama wale vijana waliotoka zao Geita kuja kumuona mkuu na kumsaidia busara za kupambana na ufisadi wakaishia kuswekwa ndani. Kosa gani walitenda? Kutaka kumuona mtukufu bila wao kuwa na utukufu. Vijana hawa walisahau kuwa urafiki wao na watukufu ulikwwisha siku walipoweka kura kwenye sanduku la kura wahusika wakachukua wakaweka waa! Hizo ndizo siasa za kichovu na kijambazi za kulana, kukwapua na kukuwapuana. Unamkwapua naye anakukwapua. Mnakwapuana na kukwapua kila kikwapuliwacho na mchezo kwisha. Kaya inazidi kuzama! Akili au matope?
          Tumalizie kwa kuwaonya wachovu kuwa katika mkwapuano huu wakijiachia wakakwapuliwa kura zao wasilalamike. Tumieni busara badala ya njaa kuwapima na kuwajua wanaopaswa kuwaongoza kwenye maendeleo na si kwenye machinjio. Chagueni watu wenye visheni na akili na si wenye kusheheni uroho na ulafi wa madaraka. Hakikisheni hamrudii makosa. Msikubali ahadi za kipumbavu wala kuangalia sura ya mtu wala kusikiliza nyimbo za sifa za wale aliowanunua wampambe na kumwimbia sifa. Mtaliwa mwajiona msipojifunza toka makosa ya 2005.

Zikomo kwa mbiri!
Chanzo: Nipashe Feb., 7, 2015.

No comments: