Tuesday, 24 February 2015

Mnaua elimu na kusingizia lugha!

Taarifa za hivi karibuni kuwa Tanzania imeanzisha mpango mpya wa elimu ambapo elimu ya awali itakwenda hadi kidato cha nne, kama ingekuwa siyo siasa ni ya kufurahisha. Pamoja na kujivuvumua huku, wengi wanajiuliza: Hiyo fedha itatoka wapi –na kama itapatikana –hiyo elimu itakuwa elimu bora au bora elimu?
Hakuna kitu kilichowaacha hoi wengi kama pendekezo kuwa Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia kwa ngazi zote. Mojawapo ya kipengele cha sera mpya ya elimu kinasema, “Lugha ya Taifa ya Kiswahili itatumika kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu na mafunzo na Serikali itaweka utaratibu wa kuwezesha matumizi ya lugha hii kuwa endelevu na yenye ufanisi katika kuwapatia walengwa elimu na mafunzo yenye tija kitaifa na kimataifa.” Huwezi kuwa na tija kimataifa kwa kufundisha lugha ambayo hata kama ni ya kimataifa, haijapanuka ikilinganishwa na lugha pana ya kimataifa inayoondolewa na kuweka Kiswahili. Hii ni siasa na hata mantiki ya kufanya hivyo ni haba sana.
          Kimsingi, kinachofanyika ni kusingizia lugha kwa mafanikio haba jambo ambalo linaonyesha upofu wa wahusika kuhusiana na chanzo cha matatizo ya elimu nchini. Nadhani kama watanzania wangekuwa makini wasingehitaji kutapatapa kutafuta namna ya kuendeleza elimu. Wana marejeo ambayo ni wakati wa awamu ya kwanza ambapo elimu ilisifika kimataifa na kujenga kizazi cha kisomi kikilinganishwa na cha sasa. Hivyo, badala ya kuhangaika warejee huko watapata jibu la kutosha.
Mfano kipengele kimojawapo cha sera mpya ya elimu kinasomeka, “Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu msingi ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu.’’ Huu ni upuuzi mtupu. Kwanini wahusika wasirejee namna ya ufundishaji wakati wa awamu ya kwanza ambapo idadi ya vitabu vilivyotumika katika somo ilitegemea aina ya somo na kiwango cha elimu. Huwezi, kwa mfano ukafundisha Kiswahili darasa la tano hadi saba kwa kutumia kitabu kimoja ukasema umeelimisha wanafunzi. Wanafunzi wanataka kuanza kuzoea kutumia na kusoma vitabu vingi ili wanapokwenda mbele wawe na uzoefu. Hapa Kanada mtoto wa darasa la tano anasoma vitabu vingi kuliko mtu wa kidato cha kwanza Tanzania.
 Kama wahusika wanaogopa kuwa wanafunzi hawatasoma, wajiulize zama za awamu ya kwanza watu walisomaje na kufundishwa kwa vitabu vingi? Kulikuwa na motisha katika elimu. Mwalimu Julius Nyerere alikuwa msomi na mtunzi wa vitabu. Alishiriki na kutoa mihadhara chuoni mara kwa mara. Nyerere hakutungiwa vitabu bali alijitungia mwenyewe. Je kwa sasa hali ikoje? Viongozi wanatungiwa vitabu utadhani ni maiti au mataahira au vichanga wasioweza kuandika vitabu vyao? Mbona rais Yoweveri Museveni ameandika kitabu?
Chini ya Nyerere Elimu ilikuwa ndiyo ufunguo na si jinai   kama ilivyo sasa baada ya kuzika sheria ya maadili ya utumishi wa umma.
Nadhani tatizo kubwa la elimu yetu ukiachia mbali walimu kutolipwa vizuri, ni kutowajibishwa kwa wale wanaovuruga elimu. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, amevurunda na si mara moja wala mbili lakini hakuwajibishwa hadi kusema kuwa hawezi kujiuzulu utadhani ofisi ni mali ya mama yake. Unajiuliza mantiki ya mtu huyu huyu aliyevuruda kwa muda mrefu kuja na kitu kipya tofauti na ukale ule ule tuliouzoea toka kwake.
 Tusisitize kuwa walimu hawana maslahi ya kutosha, wanakabiliwa na mazingira magumu ya kazi, ukosefu wa huduma muhimu kama nyumba kwa walimu, vitendea kazi kama vile vitabu na mbao vya kutosha ukiachia mbali kutokuwapo motisha. Imefikia mahali eti walimu wanaishi madarasani au vyooni. Hivi kweli hawa wanaweza kuwa na motisha wa kufanya kazi au bora liende? Zamani kazi ya ualimu ilikuwa ni kazi yenye kusakwa na kuheshimiwa sana. Lakini baada ya kuingia sera za siasa za wizi na kutowajibika ambapo watu wachache wanaweza kutumia nafasi zao au jinai kujitajirisha na wasishughulikiwe, hakuna anayetaka kazi ya ualimu tena. Wito wa ualimu umekufa baada ya siasa za kuabudia vitu kukubalika nchini hasa chini ya mazingira ya sasa ambapo ufisadi na uuzaji midarati na ujambazi vinalipa kuliko kazi.
Wanafunzi nao hawana motisha wa kusoma kwa vile kuna njia za mkato –hata kama ni haramu –za kupata ukwasi kirahisi na haraka.  Vijana wengi sasa wanafikiri kuimba rap ili kuukata kuliko kusoma. Hapa unategemea nini?
Viongozi nao hawaongozi kwa mfano. Tunaona viongozi wetu kwenye matamasha ya miziki, semina lakini si kwenye shule au vyuo wakitoa au kushiriki mihadhara kama zamani. Mfano mzuri ni kwamba rais Jakaya Kikwete amekuwa mwepesi wa kuhudhuria misiba, kusafiri je, kukutana na wazee wa Dar es salaam hata makocha wa timu za mpira wa miguu kuliko kutembelea vyuo na kutoa au kushiriki mihadhara. Je hapa motisha kwa vijana utapatikana wapi?
          Nafasi haitoshi. Tatizo la elimu ya Tanzania si jingine bali siasa chafu za kujihudumia zinazosimamiwa na watu wasio na visheni wala uwezo wa kutosha wa kuona mbali zaidi ya usawa wa pua zao na matumbo yap. Hivvyo, kuiboresha hakuwezi kufanywa kwa kuongeza vidato bali kubadili mfumo mzima wa hovyo wa kisiasa unaotupatia viongozi wabovu na wachovu. Kuhusu lugha, hata mkifundisha kwa lugha za makabila yenu, bila kubadili mfumo wa kifisadi na kiherehere yote ni bure.
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 25, 2015.
 

No comments: