The Chant of Savant

Friday 6 February 2015

Utoro wa mawaziri na uzururaji ni janga


 
          Taarifa kuwa mawaziri wengi hawahudhurii vikao vya bunge zinatia kinyaa. Kwa mujibu wa vyombo vya habari ni kwamba utoro wa mawaziri umeshika kasi kiasi cha kusababisha baadhi ya wabunge kuchukia na kuwatolea uvivu.
 Mbunge wa kwanza kuliona hili ni Godbless Lema wa Arusha Mjini aliyekaririwa akisema, “Ndiyo maana mnashinda kwenye (mitandao wa kijamii ya) instagram, facebook na Jamii Forums… mnapiga picha za kung’aa kwa sababu katika vikao vyenu vya kufanya uamuzi, mnajadili mambo ambayo hayana kina cha mawazo. Ndiyo maana nchi hii inakufa.” Sasa kama watendaji wa serikali wanapoteza muda kwenye mitandao ya kijamii, hao wananchi wa kawaida wafanye nini? Je ni fedha kiasi gani inatumika kulipia bills zao za simu, umeme, marupurupu na mapochopocho kwenye mikutano na makongamano na semina visivyoisha? Je ni fedha kiasi gani zinatumika kugharimia matanuzi yao ughaibuni? Hali inakuwa mbaya kuwa wengi wa wakubwa waendapo ughaibuni huandamana na misafara mikubwa isiyo na ulazima ukiachi ambali kukaa kule muda mrefu wakiishi kwenye hoteli za bei mbaya. Namna hii kwanini nchi isikufe? Kwanini uchumi wetu usiwe tegemezi? Je tutajiondoa kwenye kadhia hii vipi wakati hata Katiba Mpya iliyokuwa imependekezwa kuondoa upuuzi huu imeuawa kwa kuwekwa pandikizi yenye kuendeleza wizi huu wa mchana?
          Mbunge huyo wala hakuzungusha wala kufumba. Alitoboa wazi kwani aliongezea,“Mara nyingi hii husababishwa na tabia ya mawaziri ambao mnapokutana kwenye vikao vyenu, mara nyingi mnakwenda kutafuta group picture (picha za pamoja) badala ya kushauri namna gani ya kupeleka nchi hii mbele.”
Sasa tunajua chanzo cha kuzorota kwa maendeleo ya taifa letu ambapo kikundi kidogo cha watu kimeamua kututumia kama kijiko cha kuchotea utajiri bila kufanya lolote la maana. Imefikia mahali waziri wa fedha anaidhinisha malipo yasiyokuwa kwenye bajeti yake hata kwa kumega fedha toka kwenye miradi ya maendeleo kama ilivyobainishwa hivi karibuni ambapo mabilioni ya shilingi yaliibiwa tena kwa kulipwa makampuni hewa.
          Tumegeuka taifa la wasanii, wazururaji na wababaishaji bila sababu yoyote ya msingi. Fedha nyingi zinatumika kwenye vikao,  kulipa safari za nje za wakubwa zisizo na kichwa wala miguu bali uvivu na uzururaji kama alivyobainisha Lema aliyekaririwa akisema, “Angalia Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikwenda kutangaza utalii nje ya nchi akiwa ameongozana na (mwigizaji maarufu wa filamu wa Tanzania) Anti Ezekiel.”  Kama tutakuwa wakweli, huyu anti Ezekiel anatangaza utalii gani zaidi ya ukosefu wa maadili? Sina haja wala silengi kuwatetea mawaziri ila wakati mwingine tunakosea kuwaangalia wao huku tukimgwaya bosi wao. Kama rais ndiye anashika kibendera cha kufanya ziara nyingi ughaibuni na matumizi mabaya ya fedha za umma unategemea mawaziri wapate hiyo nidhamu toka wapi? Ama kweli jogoo aliwafundisha vifaranga kunya ndani. Unapokuwa na rais anayesafiri sana nje hadi watani wake wakamwita Vasco da Gama naye asipunguze tabia hiyo, unategemea nini?  Hakuna ubishi kuwa rais Jakaya Kikwete ni mmojawapo wa viongozi wanaosafiri sana duniani. Mbona wenzake wa Kenya au Malawi hatusikii wakiwa kiguu na njia ziarani ughaibuni? Je ni nini hicho anachotafuta Kikwete ambacho marais wenzake hawawezi wala kustahiki kufanya?
Hili la Nyalandu na Anti limeniacha hoi. Kweli tumegeuka taifa la kisanii na kibabaishaji bila sababu ya msingi. Hata hivyo, wenzetu majirani wanatucheka na kutuona kama hamnazo. Haiwezekani viinchi vidogo kama Rwanda visonge mbele wakati sisi tunazidi kutopea kwenye uombaomba na ukopakopa kusiwe na tatizo. Lazima wenzetu watatucheka sana kama hatutabadili mfumo huu wa kujihudumia. Fedha ya umma inachezewa, kuibiwa na kufujwa.  Imefikia mahali yanaanza kutoka malalamiko kuwa rais anawagwaya ya kuwakingia kifua wezi wa fedha za umma. Rejea kutoshughulikiwa kwa watuhumiwa wakuu wa wizi wa mabilioni ya escrow James Rugemalira na Harbinder Sethi Singh.
          Tangu sakata hili kuanza rais amekuwa akiliepa ukiachia mara moja moja kulazimika kutoa ufafanuzi mfupi kama kumweka kiporo aliyekuwa waziri wa Nishati profesa Sospeter Muhongo au kusema kuwe fedha ya escrow ilikuwa ya IPTL. Wengi hawaelewi. Wanahoji: Kama fedha ya escrow ni mali ya IPTL ilikuwaje rais akawawajibisha wale waliomegewa fedha hiyo ambayo kwa mujibu wa maelezo ya rais ni halali hata kama kazi waliyofanya hadi kulipwa mabilioni hayo hatuijui?
           Tumalizie kwa kusema wazi.Viongozi wasiokaa ofisini au kuhudhuria vikao muhimu kama vya bunge, kimsingi, ndiyo chanzo cha kukwama kwa taifa letu. Maana hawapati muda wa hata kusikia achia mbali kusoma hoja za wabunge na hata ushauri wao. Wengi wameonyesha wazi kutokuwa na visheni wala ubunifu katika nafasi zao zaidi ya kuzitumia kutengenezea fedha hata kama ni kwa kuwahujumu watu masikini wa taifa hili. Wamekosa huruma na hata aibu. Maana ukiangalia matukio kama kutangaza utalii yanayotangazwa kwenye mitandao kila uchao unashangaa hawa wanafanya kazi saa ngapi na kwanini kutangaza utalii kuwe ni kwa vigogo wa wizara na idara kama hakuna namna? Hii nayo ni aina mpya ya ufisadi. Ni uzururaji na wizi wa fedha za umma. Huu ni ujangili unaofanyika maofisini badala ya mbugani. Tena wakati mwingine ujangili huu ni hatari kuliko wa mbugani. Maana ndiyo unaofanikisha ujangili sawa na ule wa kutorosha wanyama hai wa Oktoba 26, 2010 ambao nao haujawahi kushughulikiwa ukiachia mbali sanaa na ubabaishaji tu.
Chanzo: Dira.

2 comments:

Anonymous said...

BORA YA HAO WATORO NA WASIOKWENDA BUNGENI MAANAKE HAWAPTI POSHO
ANGALIA HII MIZEEE INAYOLALA BUNGENI CHA KUSHANGAZA BADO WAZIRI PAMOJA NA PANGUA PANGUA YOTE TOBA WATANZANIA 2015 UKAWA OYEEE
NA LIKIAMKA HAPO KUTWATUKA HATA BILA KIFIRI ANNA MAKINDA HUYAONI HAYA ; HEHHE JINA UMEBADILI BAADA YA KUWA SIPKA ETI ANNE ; AWAMU YA KWANZA MBONA ILIKUWA ANA TENA SI ANNA ; TOBA UKIWA RAIS UTAKUWA NA JINA GANI ANNELISE

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon umeniua na evolution ya Jina Makinda makidamakida. Ila umeniudhi kusema eti akiwa rais. Heri tuwe na kuku ikulu kuliko Makinda sijui ya ndege sijui kenge.