Tuesday, 3 February 2015

Ngumi Zafumka Kijiweni


          Baada ya harakati za mafisadi, tena papa, kuanza kuusaka ulaji kuzagaa kayani, si kijiweni wakatokea wenzetu waliokwishawekwa kwenye mifuko na mikono michafu ya mafisadi wakataka kututenza dhambi ya kujiruhusu kuliwa tunajiona. Wanataka kugeuza kijiwe uwanja wa kampeni uchwara na zisizo rasmi. Tumewastukia na kuwaonya wasituletee upuuzi kijiweni.
          Mbwamwitu amejilawa leo akiwa na lake. Si kawaida yake kuchangamkia mic kabla a wengine. Leo inaonekana kuna jambo. Anakwea mic na kusema, “Wazee, pamoja na kutopenda Chama cha Maulaji (CcM) kuna njemba zinanikuna.”
          Kabla ya kuendelea, Mkurupukaji anamuuliza, “Zipi hizo njemba na zinakukunaje na wapi na kwanini?”
          Mbwamwitu anajibu, “Hebu uliza maswali yako kwa heshima badala ya upuuzi. I am serious. Mind you,”
          “Kwani ulidhani nami natania au umeishakatiwa chochote kitu? Unataka kutuingiza mkenge siyo? Nenda katunge vitabu vya kusifia hawa watu wako waliokukuna kama wasaka tonge wengine walivyokwisha kuanza kufanya. Kwani hatuoni wala hatuna uwezo wa kuona dalili?”
          Mgosi Machungi anakatua mic, “Mbona hatiwaeewi. Mnataka kutiambia kuwa kuna watu hapa wameishaishwa kitu nini? Haya mapenzi ya njemba zako za CcM yalianza lini kama hakuna namna? Haafu unasema bila aibu eti wamekukuna! Utaiwa unajiona eheee!”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anadakia, “Kwani kosa kupenda wana CcM au mnaendekeza unazi? Mtake msitake rais ajaye lazima atoke CcM. Halo halo!” Anagonganisha mkono na Kanji huku Kapende akionyesha wazi kuchukia.
          “Nadhani kama mtu amekosa la kusema bora anyamaze wenye mawazo ya afya na mbolea tulonge. Japo ni haki ya mtu kupenda ampendaye na kumpa kula yake amtakaye ili aliwe, wengi ninaoona sasa wakihanikiza kutaka kugombea ulaji wameishanunuliwa na mafisadi.” Kapende anazoza.
          Sofia anadandia mic, ‘Unaweza kuthibitisha madai haya au umbea kama kawaida? Hivi mmeingiliwa na nini kiasi cha kuchukia watu hivi?”
          “Kama kuingiliwa basi wewe kiongozi. Hivi inahitaji uwe na shahada kujua kuwa wengi wa wanaohanikiza wameishawekwa kwenye mifuko ya mafisadi ambao wanataka wawatumie kutuibia? Hukumsikia babu yenu Kingungeee akituonya au naye ameingiliwa kama unavyotaka kututukana na kutunyamazisha?”
          “Mie sijali nani kasema. Kwani yeye ni nani asiingiliwe na pepo la kuchukia wenzake kama wale wanaotoa mimacho utadhani panya kanaswa mtegoni. Wana sera hao?” Sofia anaongea huku akimtuzama Kapende ambaye anaamka na kutaka kumkata mabao.
          Kanji badala ya kumsaidia Sofi asinaswe mabao anaamka na kukimbilia upande wa pili. Anasema, “Sasa veve Pende naleta wita ya nini? Kwanini nataka onea Sofia? Hapa jiweni sisi kaa ongea siasa. Kama naweza boxing nenda tafuta Tayson veve pigana naye.”
          Baada ya kuona zali linaanza kimtindo, Msomi Mkatatamaa anaamka na kumzuia Kapende asimtie adabu Sofi.
          Kapende anajisemea, “Akushukuru sana. Kama siyo kukuheshimu leo ningemkumbusha kilichomfanya aitwe Kanungaembe huyu changu mpuuzi. Kwanza hatukutaki hapa nenda kwenu CcM na hao walionunuliwa kama dagaa.”
          “Jamani, yamekuwa hayo tena! Sasa matusi ya nguoni ya nini tena kwa watu tunaoheshimiana na kupendana tukiishi kwa amani na utulivu?” Mbwamwitu anongea huku akitabasamu kuonyesha kukubali yaishe.
          Kapende haridhiki, anarusha kijembe, “Kama kupendana kapendane nyinyi. Mie simo kwenye mapenzi ya kibubusa na amani ya uongo kama mnayodanganywa nayo na wezi wenu kila siku. Amani ni wao kuiba na nyinyi kuibiwa siyo?”
          Mpemba anakatua mic, “Hebu jamani tusikiliizaneni. Hakuna haja ya kulumbana kwa vitu tena vitu vyenyewe vya kitoto hivi. Hawa kweli waniowania huu ulaji wa bila kunawa tena kwa miguu na mikono kweli wamenunuliwa. Laiti tungehoji wanikopata hii fedha ya kuruka na madege au kulipa waandishi wawatungie vitabu na wengine kuandikwa vizuri magazetini.”
          Msomi anaamua kurejea, “Hawa wanaopewa njuluku waandike vitabu hawanipi taabu. Kwani huu ni wakati wa kulana na kula wengine. Mara hii mmesahau yule habithi changu wa kimaadili aliyeandika tabu la hovyo la Tumaini Lililorejea akaishia kuaibika na kutokomea hata bila kulipwa fadhila.”
          Kabla ya Msomi kuendelea Mijjinga anadandia, “Hawa wanaotumia vitabu kujitangaza wameingia mkenge hasa ikizingatiwa kuwa wachovu si wasomaji wa vitabu. Heri angetumia mbinu ya kuweka watu kwenye baa, glosari na kumbi za starehe huenda angewapata waliwao wakidhani wamekula. Wachovu wanavyopenda starehe nani atasoma tabu la kurasa nyingi hivyo?”
          Mipawa anadandia mic, “Heri wangewaambia waimbaji wawatungie nyimbo kuliko vitabu ambavyo sina hakika kama havitafungiwa vitumbua na maandazi.”
          Msomi anarejea kuendelea na hoja yake, “Kama nilivyosema kutunga au kutotunga vitabu au kutumia magazeti nyemelezi kuchafuana kama alivyofanya baba yao havinihangaishi.  Kinachonihangaisha ni wizi wa njuluku zetu kwa ajili ya kusaka urahisi. Hamkumsikia mzee wa Mizengwe iliyo-Pinda eti naye anautaka urahisi wakati alishirikiana na bosi wake kuanzisha na kubariki ujambazi wa escrew? Huoni wote walivyonyamaza utadhani hakuna jinai iliyotendeka?”
          Mgosi anamchomekea, “Msomi unachosema ni kwei tupu. Nashangaa kuona Ugemalaya na Sing wakiendelea kutesa utadhani hawakutiibia njuuku. Naamini kwei mkuu naye yumo kwenye dii hili.”
Mpemba naye anaamua kutia guu, “Yakhe mie ndhani hawa wajalaana waniotumia kuandika vitabu lau wangeelekeza mashambulizi kwa wezi wa njuluku ingeingia akilini wallahi. Wanichofanya naoni ni unepi ambapo mafisadi huwatumia kufutia uchafu wao.”

          Kijiwe kikiwa kinanoga si kunguru akamnyea Sofi kichwani!
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 4, 2015.

No comments: