Tuesday, 17 February 2015

Kijiwe Kugomea Kura ya Uchakachuaji


          Baada ya wachovu kustukia rongorongo za kutaka kuwabamiza mkenge kupitia kura ya maoni, kijiwe –kwa makusudi mazima – kimeamua kujitoa kwenye dhambi hii. Hivyo – rasmi – tunatangaza kuwa wanakijiwe –isipokuwa Sofia Lion aka Kanungaembe na Kanji – hatutashiriki ije mvua au jua.
          Mipawa leo ndiyo analianzisha. Anakwanyua mic, “Wanene mmesikia hizi mbinu za kutaka kutuingiza mkenge yaani maandalizi eti ya uchakachuaji wa kupitisha katiba ya mafisadi?”
          “Mgosi hapa suala si kusikia. Tunaona jinsi mafisi na mafisadi walivyodhamiria kutubamiza mkenge wakidhani hatuna kumbukumbu. Nani ashiriki jinai hii wakati tunajua fika jinsi rasimu ya mzee Jose Wariobha ilivyochakachuliwa na kupandikiziwa hii ya kifisadi?” Mijjinga anachomekea huku akimkonyezea Sofi bila kujali kuwa anaweza kufikishwa kwa Pilato kwa kosa la kukonyeza.
          Mgosi Machungi hajivungi. Anapoka mic, “Tiambiane ukwei. Kama hawaeti rasimu ya Waioba wasahau sisi kushiiki.  Tishiiki kwa faida gani wakati tinaibiwa na kubuuzwa? Kama wana mazoba na majuha wao wa kushiiki kuhalalisha kitanzi chao, sisi hatumo au vipi wanene? Wakati mwingine natamani nipige mtu zongo waahi.”
          Kapende anadanda na kunyakua mic, “Usemayo Mgosi kweli tupu. Sisi siyo mazoba wala misukule ya kushiriki maafa yetu. Hawa nadhani wanatafuta sababu ya kuibia njuluku zetu baada ya kufanikiwa kwenye ujambazi wa escrew.”
          “Wanasanyasanya njuluku ya takrima kwa sasa ili wawapate wapenda dezo wasijue wanajiuza na kununuliwa na wasaka tonge kupitia siasa tena afisi kuu!” Mbwamwitu anaamua kula mic.
          Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akibofya ki-Sumsung Galaxy 5 anadandia mic, “Nadhani kugoma kushiriki pekee hakutoshi. Tunapaswa kuweka mikakati ya kuzuia matokeo chachakachuzi yatakayopikwa na kutolewa baada ya vibaraka na waramba makalio ya mafisadi kushiriki uovu huu. Lazima tupange kuandamana tena bila woga. Maana wakitupiga au kutuua ICC haitawaacha. Nadhani hili ndilo jibu la upuuzi na ushenzi huu.”
          Sofia hangoji. Anamchomekea Msomi, “Msijidanganye kuwa mkiandamana bila vibali watawaacha kwa kuogopa hiyo ICC yenu. Hii kaya ina sirikali yake isiyoendeshwa na ICC.Hivyo, kama mtajitia kimberembere na kiherehere mtapigwa kama alivyowahi kusema mzee Mizengwe.”
          “Da Sofi hapa sikuachii. Ngoja nikuchomekee kidogo. Kama hujui nguvu ya ICC basi unapaswa urejee shule. Hukuona pale Kenya ilivyoepusha zali jingine. Unadhani Jadwong Laila angekubali kienyeji hivi?” Mbwamwitu anamchomekea Sofi.
          “Mie mambo ya kuchomekeana siyawezi mwenzangu. Kwanini usiseme tu unachosema.kwani lazima uchomekee. Kwani huwezi kusema bila kuchomekea au unaanza uhuni? Acha kiherehere cha kujifanya unajua siasa kuliko wengine.” Sofi anang’aka huku akimbulia midomo Mbwamwitu ambaye wanajuana kwa utani.
          “Umenikumbusha kiherehere na bwana kiherehere aliyewaambia watoto wa shule kuwa wanapewa mimba kwa sababu ya kiherehere asijue naye alikuwa na kiherehere kuwatukana.” Anachomekea Mheshimiwa Bwege.
          Mpemba anakatua mic, “Yakhe wankumbusha. Huyu bwana kwa kiherehere wallahi sina nfano. Juzi nimensikia akirejea maneno yake kusema eti takokuru wana kiherehere kukamata watu bila uchunguzi asijue naye ana kiherehere kuiweka takokuru chini ya afisi yake.”
          Baada ya Kapende kugundua kuwa wajumbe wanaanza kutoka kwenye mada anaamua kula mic, “Huyu bwana kwa kiherehere sina mfano. Mliona aliyosukumwa nacho kumshambulia jaji Wariobha? Hayo tuyaache. Kama alivyopendekeza Msomi, tunapaswa kutafakari nini la kufanya kama hawa mahabithi wataendelea na mipango yao ya kutubamiza mkenge kwa kutaka tupigie kula katiba ya mafisadi. Mie naona tuanze kuhamasishana tugomee na kuhakikisha kaya haitawaliki.”
          Mijjinga anaamua kurejea, “Jamani hakuna haja ya kukatisha tamaa wala kutishana. Naona sisi tuandamane na kugomea huu upuuzi mengine tutaamua huko kulingana na hali. Tukianza kukadiria nini watafanya tutapoteza hoja na mapambano. Hawa mafisadi lazima wakomaliwe kwa gharama yoyote.”
          “Mie kupigwa au kutopigwa kura havinihangaishi. Kwani matokeo nayajua hata ya uchakachuaji ujao Oktoba. Hukusikia wakisema eti watashinda kwa kishindo wakati hata kampeni ya urahisi haijaanza? Kinachoniuma na kunihangaisha ni jinsi hawa majembuzi wanavyotumia zoezi hili kuiba njuluku zetu. Nasikia wameishapiga zaidi ya bilioni sita za madafu.” Anazoza mzee Maneno.
          Kanji hangoji. Anakula mic, “Hata mimi iko sikia pele taa ya Kwepu (Mkwepu) nakwenda jamatini kuwa juluku nakwishaiba. Jitu ingine tabu sana. Kwanini iba juluku bila fanya kazi yoyote? Kama naangalia jinsi chori naiba jukuku hapa nagudua hapana tumia akili kabisa.”
          Sofi anamkata Kanji jicho la hasira asiamini kama kweli yale maneno yamemtoka mshikaji wake asijue kuwa wenzake wanaangalia nani atashinda na siyo nini. Hawa jamaa kwa kubadilika si unajua.
          Msomi anamuagiza muuza kahawa ampe kahawa Kanji kama ishara ya kufurahia mageuzi aliyofanya. Anaendelea, “Sofi usishangae. Hata nawe utabadilika baada ya kuelimishwa ukaelimika ukaacha kutumiwa na kutumikia mapenzi ya kibubusa wakati wewe ni muathirika kama sisi. Ni suala la wakati tutakupa dozi kama Kanji hadi ubadilike.”
          “Somi mimi heshimu veve sana. Hiyo dozi natoa kwangu nini kama si tusi ya guoni dugu yangu?”
          Huku akijifuta machozi tokana na kicheko baada ya Kanji kubukanya maneno, Msomi anajibu, “Kanji mimi na wewe! Ninaposema dozi namaanisha uchambuzi na ufafanuzi au siyo?”

Kijiwe kikiwa kinanoga si tukapata habari ya msiba wa bibi ya bibi wa bibi ya binamu wa mheshimiwa Bwege!
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 18, 2015.

2 comments:

Anonymous said...

ICC NDIO KIBOKO YA VIONGOZI WA AFRICA WAZUNGU NDIO WANAWAOB=GOZA VIONGOZI WENU AFRIKA MPAKA SIKU YA KIYAMA

NN Mhango said...

Anonymous umesomeka na kueleweka. Karibu tena.