Tuesday, 10 February 2015

Kijiwe Chaistukia Tako-kuru


          Baada ya Mrukugenzi sorry Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupamba na Kuruhusu Rushua (Takokuru) Eddie wa Shea  Hoshea kuja na mizengwe – utadhani yule wa kupinda – kuwa atapambana na rushua, kijiwe kimeamua kumtolea uvivu kwa kumuuliza miswali tena migumu ili kumuumbua na kumsuta aacha hizo za kuleta na kuzua.
          Kapende ndiye analianzisha huku akinukuu gazeti la Maloloso akisema, “  Mmesikia huyu nepi ya mafisadi Eddie wa Shea Hoshea akisema eti kwa sasa wanawachunguza majambazi wa escrew?”
          “Tafadhali mhashamu Kapende usitake kunitapisha kwa uoza huu. Huyu si ndiye Mrukugenzi wa Takokuru siyo?” anauliza Mzee Maneno.
          Kapende anatikisha kichwa kama ishara ya kukubaliana na mzee Maneno.
          Mzee Maneno anaendelea kudema, “Kama sikosei huyu aliwahi kutaka kuwasafisha majambazi wa Richmonduli. Nadhani huyu anatafuta umaarufu.”
          “Huyu hawezi kuwachunguza mafisadi wakati naye ni fisadi anayepaswa kuchunguzwa,” Anachomekea Mbwamwitu.
          Mijjinga anakatua mic, “Usemayo mhashamu Mbwamwitu ni kweli. Huyu jamaa tunatoka kijiji kimoja kule Musoma. Ana ukwasi si mchezo.”
          “Wewe unaongelea ukwasi wa Uswazi wakati hata hapa Dar kwa wazito anayo mijengo ya bei mbaya! Ukitaka kujua kuwa hata hawa Takokuru ni mafisadi na wala rushua, toa amri ya kuchunguza maisha na ukwasi wa maafisa wake.  Hawana tofauti na wezi wa TRa, viwanja vya ndege, uhamiaji, bandari, benki kubwa, biashara, ardhi, madini, mambo ya ndani na sehemu nyingine zilizojaa wezi na matajiri wa kutupwa wanaotumia ofisi za umma kujitajirisha wakati umma ukizidi kufukarishwa chini ya kile ambacho kwa kisomi huitwa pauperization of the hunk by her rulers who – most of them – are either myopic or insane.” Msomi anasema.
          Wakati akiendelea si mzee Maneno anamstua akisema, “Mhashamu Msomi angalia lugha hiyo. Naona umepandisha Mwenembago hadi kusahau utaratibu wa kijiwe kuwa ni kuongea lugha ya kaya.”
          Mgosi Machungi anaamua kula mic, “Usemayo Msomi ni kwei tupu. Sisi tinaona aina ya maisha wanayoishi. Tinawajua hata vimada wao na hata waganga wao. Mimi naona huyu Hoshea anajiiisha pepo. Akiwachunguza hawa wezi wa eskoo atapigwa chini kama wenzake waiopokea uchache kiduchu wakapigwa chini.”
          “Yakhe maneno yako yanshawishi wallahi kutaka kwenda piga mtu. Huyu Washea hana lolote wallahi. Muda wote alikuwa wapi wakati hizi njuluku zaibiwa? Kama asema awachunguza kwanini asiwakamate kwanza kama waharifu wengine wadogo waniokamatwa pale wanipotuhumiwa tu?” Mpemba anahoji huku akiweka vizuri saluni yake.
          Msomi anaamua kurejea, “Usemayo Ami ni kweli. Akijaribu kutia pua yake kwenye ulaji wa wakubwa atapigwa chini. Kama angekuwa na ubavu wa kuwachunguza hawa wakubwa basi angeanzia ikuu ambako dalili zote zinaonyesha kuwa dili zima lilisukwa huko sawa na lile la EPa na Richmonduli. Huoni Chekacheka anavyojichanganya akisema mara njuluku za IpTL mara hivi mara vile? Wengi wanahoji. Kama njuluku ni mali ya IpTL, mbona akina Anae Kajuamlo Tiba, Freddie Were-ma na Saucepie Muongo walitimuliwa? Huu ni uchunguzi wa namna gani unaofanywa wakati watuhumiwa wakiwa nje hata bila kufikishwa polisi? Huenda huu ni upelelezi wa kikubwa unaofanywa kikubwa ili kuficha makubwa ya wakubwa.”
          “Kwanini mnapenda kuzuazua hivi? Nani kakwambia kuwa ikuu inashirika na una ushahidi gani kama siyo chuki binafsi?” Sofi Lion aka Kanungaembe anamchomekea Msomi huku Kapende akimtazama kwa jicho la chuki.
Mipawa ambaye alichelewa kidogo anaamua kula mic, “Sofi utabadilika lini kwa kufanya kazi ya uwakili bila malipo au kuna malipo ya siri unapewa na hawa wezi wakubwa? Maana kila mtu akiwagusa unang’aka kana kwamba lenu moja au wewe ni shushu wao kijiweni?”
          Mheshimiwa Bwege anaamua kukwanyua mic, “Shushu hawe huyu? Kwanza zama za ushushu na kutishana zimeliisha zama gani! Nadhani dada yangu ana kaugonjwa ka kujikomba ili avutiwe kidogo ale kama wale tuliowajadili wiki iliyopita kuhusiana na kutungia wagombea vitabu. Nadhani ni njaa ima ya tumbo au ubongo.”
           Kanji haridhiki na majibu ya mhashamu Bwege. Anakwanyua mic na kudema, “Heshimiwa bwege kuwa na heshima kidogo bwana. Veve sema eti dada Sofi iko jaa bongo. Iko jua jaa ya bongo zuri veve dugu yangu Bwege? Acha Sofi tetea kulu yaveza give yeye juluku au cheo kama ile nyingine Najipendekeza napewa kuu ya vilaya.”
          Kila mtu kijiweni anapigwa na butwaa Kanji kumkaanga Sofia swahiba yake leo.
          Kapende wala hafichi furaha yake. Anakula mic, “Muuza kahawa hebu mwekee kahawa mhashamu Kanji.” Anamgeukia Kanji na kumpa mkono ingawa Kanji haupokea na kusema, “Kanji leo umenifurahisha kuanza kuona mwanga na kujua ubovu wa mtu wako.”
          Kanji hakubaliani na Kapende. Anakwea mic, “Dugu yangu Pende kwanini penda sana fanya mimi jinga. Eti mimi ona mwanga kwani ishi kwa kiza? Eti Sofi iko mtu yangu. Sitaki chonganisha na memsahib jumbani yangu.”
          “Kanji ambia yeye kuwa hindi hapana oa Swahili,” anachomekea Mchunguliaji.
          “Mbona Ushoto wapo walioa waswahili?” Machungi anahoji.
          Mzee Maneno anasema, “Huenda kwa vile mitoto ya kisambaa ni myeupe kama wao.  Au walipigwa kitu unacheza na Tanga nini?”

          Kijiwe kikiwa kinanoga si ngwalangwala ikamgonga msukuma mkokoteni!
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 11, 2015.

No comments: