The Chant of Savant

Tuesday 24 February 2015

Kanji apanga kupeleka toto yake Bombei


          Baada ya waswahili kuanza kuingiza uswahili hata kwenye elimu, Kanji anapanga kuregesha watoto wake Bombay ili wakapate elimu safi warejee huku watawale na kuhomola.
          Si kawaida ya Kanji kuanzisha mjadala. Leo anavunja mwiko huu kwa kuwa wa kwanza kuanzisha jadala.
          Baada ya kupiga kahawa yake anakwanyua mic na kuchonga, “Zee iko sikia hii vatu leta herehere sema eti sasa Sahili tumika sule yote hata Univesiti?”
          Mpemba anadandia, “Kwani kuna ubaya gani kuongeza ujinga juu ya ujinga? Waongelea huu usanii wa juzi wa kuharamisha kimombo kwenda Kiswahili? Kiherehere kitupu kama cha bwana kiherehere mwenyewe anayewashitaki wengine kuwa na kiherehere wakati yeye bingwa.”
          “Kumbe dugu yangu veve jua kuwa sasa ongeza jinga juu jinga. Ukiongeza jinga juu ya jinga napata jinga kuba.” Anacheka na kuendelea, “Veve napanga nini toto yako au vaacha hapa iwe jinga sana?” Kanji anauliza huku akicheka.
          Mpemba anamjibu kwa swali, “Yakhe kwani wewe wapangani na hao watoto wako?”
          Kanji anajibu, “Mimi iko peleka toto vote Bombei. Mimi ona si zuri acha toto haribiva hapa na jinga jinga kuba. Yeye peleka toto yake soma nje nadanganya sisi zani sisi jinga siyo?”
           Msomi aliyekuwa akisikiliza anaamua kutia timu. Anakula mic, “Kanji leo umenifurahisha sana. Naona unaanza kufaidi elimu inayotolewa bure hapa kijiweni. Ni kweli kama ulivyosema ukiongeza ujinga juu ya ujinga unapata ujinga ule ule kama hawa wanavyotaka kuendelea kwageuza wachovu majuha. Hivi kweli kwa ulimwengu wa utandawazi unaweza kufikiri kutumia lugha ndogo kama Kiswahili kufundishia hadi Chuo au choo?”
          Mijjinga anaamua kutuacha hoi.  Anakula mic, “Nilishawaambia mnichague mimi muone elimu yenu itakavyopaa. Sina mchezo na mtu akila kitu kidogo namshushia nyundo kubwa na mambo mswano au vipi? Akighushi mtu natupa lupango bila kumwangalia usoni kama hawa wanaolindana kinyaninyani. Jamani nipeni angalau ubunge muone jimboni kwangu Kisesa.”
          “Nyie mnawashangaa hawa wasanii kupendekeza vitu vya ajabu na kisanii! Wao wanashida gani iwapo wanatumia kodi zenu kupeleka vitegemezi vyao nje vikasome elimu ya maana na kutema umombo kama ndugu yangu Msomi? Hamumuoni mtoto wa mgosi Makambale anavyotaka kugombea urahisi kwa vile amesoma ughaibuni?” Anauliza Mijjinga huku akibofya kisimu chake.
          Leo Kapende kaja na tablet yake. Naona yuko bize nayo kiasi cha kutoshiriki maongezi kama kawaida yake. Si  unajua tena Wachovu akipata kitu kipya lazima awakonge wenzake kinamna.
          Mipawa anaamua kula mic, “Tusipoamka na kuondoa hawa wasanii tutaendelea kuliwa tukijiona. Lazima hawa jamaa wawe wamechanganyikiwa au huenda wanataka kuanzisha shule za English Media na Vyuo vya English Media ili waendelee kupata uchache baada ya kukitoa. Maana haiingii hata akilini.” Mgosi Machungi asivyopenda neno hili, anaamua kula mic haraka haraka, “Kwanza sikuabiani nawe kuwe tinaliwe. Ila nakubaiana nawe mgosi kuwa hawa mafisadi wana ajenda za siri. Kwanza huu ni ujinga sina mfano. Napendekeza titunge sheia ya kuzuia mwanakaya yoyote kupeeka kitegemezi chake kusoma ughaibuni ii tuone kama hawataonja joto ya jiwe.”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kula mic, “Hivi nyie mfanyiwe nini chema ndiyo mshukuru? Hamjui kuwa Kimombo kilikuwa kikifelisha watoto wetu wengi? Sasa mtaona watakavyofaulu hadi muanze kulalamika kuwa wanafaulu sana kiasi cha nyinyi kuonekana hamkuwa na akili shuleni.”
          “Sofi angalia lugha hiyo tusikosane bure,” Mzee Maneno anamtahadharisha Sofi baada ya kuona anavuka mipaka.
          “Acheni uvivu wa kufikiri. Kwani hicho Kimakonde mmeelezewa kitakavyofanya wasomi washinde au mnakariri maneno yao kama kasuku? Nadhani kianchofanyika hapa ni kutapatapa. Bila kuwekeza kwenye elimu hata mkifundisha kwa lugha ya malaika mtafelisha. Njuluku mnaiba na akina escrow na kuwekeza kiduchu kwenye elimu halafu mnategemea mfanye vizuri siyo?” Kapende anaamua kujibu hoja ya Sofi.
          Msomi anarejea, “Kapende umeongea utadhani umesoma mawazo yangu. Niongezee hapo. Hivi unategemea ufaulu uongezeke bila kuongeza marupurupu na mishahara ya wala chaki? Mishahara yenyewe mnawakopa huku wengine wakiishi vyooni. Hivi mwalimu anayelala chooni anaweza kuwa na akili ya kufundisha wenzake kweli? Maprofesa wamevamia siasa mnategemea Vyuoni wasifelishane? Rushwa hadi za ngoni zimeshika kani mnategemea nini? Usanii umegeuka dili ya kuukatia huku mihadarati na ujambazi na ufisadi ukipanda chati mnategemea kuwe na motisha hasa kwa watoto kusoma kweli?”
          Anachukua leso yake na kujifuta jasho na kuendelea, “Kwanini hawataki kuangalia ukweli machoni? Nadhani sababu ya kutofanya vizuri ukiachia mbali bajeti kidogo na kusahaulika kwa sekta ya elimu ni kutamalaki kwa jinai kama vile kughushi vyeti, ufisadi, ujambazi wa kalamu na wa silaha, viongozi kutokaa maofisini wakashikilia kuzurura wakifuja njuluku ambayo ingepelekwa kwenye elimu. Hivi unategemea nini kama wakubwa wenyewe ni vilaza na vihiyo watupu? Hebu angalia viongozi wa kwa akina Joji Kichaka wanavyoandika vitabu. Hapa ukiondoa gweiji Mchonga nani amewahi kuandika kitabu zaidi ya wengine kuandikiwa utadhani maiti au kuokoteza hotuba?”
          Mbwamwitu anaamua kumchomekea, “Hili la maprofwedha kuvamia siasa limenikumbusha maprofedheha kama Anna Kajuamlo Tiba, Saucepie Muongo, J4 Majembe, Jimmy Kapuyanga na madaktari uchwara kama Shchool Kawa-dog wanaoendelea kuvurunda utadhani hawakwenda shule.”
          Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita muuza vitabu akiuza kamusi za kimombo!
Chanzo: Tanzania Daima Feb., 24, 2015.

No comments: