Nani angeamini, katika karne ya 21 pamoja na ahadi kemkem za maisha bora kwa wote, mahindi matano yangemuua mtu? Hii imetokea na si mara ya kwanza wala ya mwisho. Kuna watoto ima wamekatwa vidole hata kuuawa kwa kuiba shilingi mia mbili na matukio mengine kama haya ya kutisha na kusikitisha.
Kisa cha kutisha kilichoripotiwa hivi karibuni na gazeti la Tanzania Daima kuwa mjane Suzana Karumbete (64) alipigwa hadi kukata roho kutokana na kudhaniwa kuiba mahindi matano, kinatisha na kuhuzunisha sana. Na laity kama kisa hiki kingesimuliwa na mtu binafsi, si ajabu msikilizaji angedhani ni uongo wa kawaida.
Ukweli ni kwamba hii aibu imetokea huko Karukekere tarafa ya Kenkyombyo wilayani Bunda mkoani Mara. Kwa vile hili ni tukio ambalo linapaswa kushughulikiwa na polisi, hatutaingia undani wa kisa hiki. Badala yake tutazama kwenye unyama huu unaoanza kuzoeleka.
Hatujui watanzania hasa viongozi waliojitwisha jukumu la kuleta maisha bora kwa wote kwa hiari yao, kama wanasoma magazeti, wanajisikiaje? Kama tukitumia silka ya utu hii ni aibu na pigo kwa jamii nzima ya kitanzania ambayo imegeuka kama mbwa mwenye uchu anayekula vitoto vyake.
Haiingiia akilini kuamini kuwa tuna watanzania tena vijana wanaoweza kukosa utu na akili kiasi cha kuua mjane mwenye miaka 64 ambaye pigo la kuondokewa na mume linatosha kututikisa mioyoni mwetu kama kweli tungekuwa binadamu.
Taarifa kuhusiana na kashfa hii kwa taifa zinasema eti watuhumiwa wengine wamepewa nafasi ya kutoroka huku waliokamatwa wakibakizwa kwa mwenyekiti wa kitongoji utadhani yeye ni polisi! Utawala wa sheria hapa uko wapi iwapo hata kanuni na taratibu ya kawaida isiyohitaji mtu kuwa wakili inavunjwa kienyeji nab ado tunavumiliana? Namna hhii kwanini wazungu wasiendelee kutuchukulia kama wanyama wenye sura za binadamu? Ajabu ya maajabu, tangu tukio hili kuripotiwa si waziri wala mkuu wa mkoa amejitokeza kulaani!
Wakati kashfa hii ikizidi kuchanja mbuga unasoma habari kuwa mbunge toka eneo hili ambaye ni waziri anapata muda wa kutoleana vitisho na vyama ya upinzani vinavyoandamana dhidi ya kukithiri kwa maovu kama haya! Je huyu naye ni binadamu mwenye kufaa kuwakilisha wanadamu wenzake au wanyama kama yeye?
Ajabu nyingine ni kwamba tukio hili linatokea jirani na kwa shujaa na mfano wa kitaifa Mwl. Julius Nyerere. Je polisi na utawala wa wilaya na mkoa mkoani Mara ni wa nini kama uonevu kama huu unafanyika? Hawa wanalipwa kwa kazi ipi iwapo nyadhifa zao zinatumika kunyamazia maovu ambayo tulipigania uhuru kuyateketeza? Mtu mzima na mwenye kuhitaji msaada wa jamii anauawa eti kaiba mahindi matano bado tunavaa suti na kujiita viongozi!
Hapa tunaongelea mjane mmoja. Bado ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, vibaka na vichanga wanaouawa kikatili kila uchao. Ajabu wanasiasa bado wanatoa ahadi za maisha bora na utawala wa sheria!
Je ni matusi kusema kuwa jamii yetu ni mbaya na hovyo kuliko hata ya mahayawani wa mbugani Serengeti? Je Suzana Karumbete siyo suto na kashfa kwetu? Je hadi wauawe ndugu wa watawala ndipo tutastuka? Je marehemu angekuwa polisi au ndugu yake au tuseme mkuu wa mkoa hata rais hali ingekuwaje? Je huu si ubaguzi wa wazi?
Kwanini tumejirahisi hivi kiasi cha kuwa watumwa wa maovu na ubinafsi visivyo na tija kwa vizazi vijavyo? Mtu anayeua mjane wa miaka 64 kwa kusingiziwa kuiba mahindi matano angekuwa na akili si angekwenda kupambana na mafisadi wanaoiba mabilioni? Kwa vile mtu wa namna hii hana akili, hajijui wala kumjua adui yake!
Je huu si mgogoro tosha kijamii na kitaifa? Ajabu tunapata mshipa wa kwenda eti kusuluhisha matatizo ya wenzetu wakati tunayo yetu makubwa! Kwanini wahusika hawajisuti na kutumia japo akili ya kawaida (common sense)?
Kuna nini mkoani Mara? Maana mwaka jana mtoto Matiko Mwita (7) anayesoma shule ya msingi Abainamo wilayani Tarime mkoani Mara eti aliunguzwa mikono yake kwa kudokoa samaki. Hii ni baada ya mtoto kuachwa bila chakula kiasi cha kuamua kudokoa samaki. Je mhusika amefanywa nini ili liwe somo kwa wengine? Kwanini tusitumie jicho kwa jicho kwa watu kama hawa wasio na huruma?
Tuhamie sehemu nyingine. Mwaka 2009 Aden Raphael (35) wa Kijiji cha Ivalalila, Wilaya ya Makete, mkoani Iringa alimuua mkewe Roida Sanga (30) kwa kukata na na jembe kichwani baada ya kunyimwa chakula.
"Mtuhumiwa huyo baada ya kurudi nyumbani alimtaka mkewe ampe chakula na baada ya mkewe kumweleza ukweli kuwa chakula kilikuwa hakipo kutokana na kukosa fedha za kununulia, alianza kumshushia kipigo kabla ya kuchukua jembe na kuanza kumkata kichwani mara mbili hadi kufa,” alinukuliwa kamanda wa polisi wa mkoa Evarist Mangalla.
Je tatizo ni la hawa wauaji au jamii kwa ujumla hasa watawala?
Miaka mitatu kabla ya tukio hili hapo juu Emmanuel Julian [28], mkazi wa Dihinda, Turiani, Morogoro alimchinja mkewe eti kwa kuchukua shilingi 500! Tunajaribu kutoa mrorongo huu ili wahusika waone walivyoiangusha jamii iliyowaamini madaraka. Maisha bora yako wapi?
Na hiyo mifano hapo juu ni tone katika bahari. Karibu kila mkoa nchini una visa vya kikatili na kihayawani kama hivi. Je hapa hayawani ni wale wanaotenda unyama au wale walioaminiwa madaraka wakayatumia kuchumia na kutetea ufisadi? Kwanini tumejirahisi kiasi cha kugeuka jamii ya mahayawani? Kama tuna uchungu na maisha yetu kwanini tusipambane na maadui wa kweli badala ya akina mama na watoto?Chanzo: Dira ya Mtanzania Machi 14, 2011.
3 comments:
Mhango: Ni mambo ya kusikitisha kwa kusema ukweli, binafsi mimi naona hata vibaka wanavyopewa adhabu ya kuchomwa moto au kipigo cha mbwa mwitu ni uonevu tu maana hatujui ni nini kinapelekea mtu kodokoa, pengine ni njaa!
Usemayo ni kweli Matiya, tumeuzika utu na kuanza ibada za vitu tena vidogo tu. Inasikitisha and something has to be done timely.
Ukatili umezidi pamoja na ujinga. Haina maana kumwua mtu kwa mahindi matano wakati viongozi wa serikali wanaiba mamilioni lakini hawafanyiwi chochote. Nakumbuka nilipokuwa likizo Dar, nilikuwa nimevaa miwani ya Shs 1000 wakati niko safarini dirisha wazi, kumbe kuna kibaka ananiivizia kuipora. Jamaa niliyekuwa naye haraka haraka akamputa jamaa mkono kabla haujanifikia. Nikaona hii shida yote ya nini, kama jamaa angekuwa anahitaji miwani angesema tu, hamna haja ya kutoana ngeo.
Post a Comment