Tuesday, 16 September 2014

CCM na makada wake wataangamiza taifa


 Habari kuwa serikali imerejesha nyumba 12 mkoani Sumbawanga zilizokuwa zimetwaliwa na kada Chama Cha Mapinduzi (CCM) Chisant Mzindaya Mbunge wa zamani wa Sumbawanga ni habari njema kwa watanzania wenye mapenzi mema na taifa lao. Maana ni muda mrefu tangu hujumu hii ifumbiwe macho na vigogo wenzake kwa vile ni mwenzao na anafanya kama wafanyavyo wao hata kama hawajagundulika. Ni uroho na roho mbaya kiasi gani kwa mtu mmoja kujitwalia nyumba zaidi ya kumi huku umma wawatanzania ukiishi bila nyumba? Je ni makada wangapi na vigogo wa serikali wamejitwalia nyumba za umma? Rejea kugawana nyumba za umma kulikofanyika chini ya utawala Benjamin Mkapa.
          Mzindakaya kwa kutumia ukada wa CCM aliweza kunyakua nyumba husika zilizotolewa na Shirika laKimataifa la Maendeleo la Norway (NORAD) mwaka 1988 baada ya kukamilisha mradi wake huko Sumbawanga. Kwa kutumia kampuni yake ya Animal Food Industries Limited (Saafi), Mzindakaya alizinyakua nyumba husika kinyume cha sheria na kuzitumia binafsi huku wafanyakazi wa serikali wakihangaika na kukosa mahali pa kuishi.
          Kwa mujibu wa sasa wa Sumbawanga Hilal Aeshi, wafanyakazi wengi wa seriakli walikuwa wakiteseka kutokana na uhaba na ukosefu wa nyumba mkoani mwaki. Alikaririwa akisema, “Nina furaha sana leo kwa sababu hatimaye serikali imerejesha nyumb a zake, sasa majaji na maafisa wengine wa serikali wataweza kuishi kwenye nyumba za kisasa zinazomilkiwa na seriali badala ya kuishi kwenye nyumba za kupanga.”
          Chakushangaza ni kwamba wakati hujuma hii ikiendelea kwa zaidi ya miaka 20 serikali na chama tawala CCM walijifanya kutoona kilichokuwa kinae ndelea kwa vile ilimhusisha mwenzao. Je hujuma hii inachochea hasira na mateso kiasi gani kwa watu maskini wa nchi hii? Je ni mamilioni mangapi Mzindakaya ameibia umma katika jinai hii? Je tunao watu wangapi waroho na wenye kujihudumia kama Mzindakaya nchini ambao wengi ni makada wa CCM? Asitokee mtu akatudanganya kuwa kilichofanyika hakikujulikana kwa viongozi wa juu serikalini. Walijua kila kitu. Sema nani angeweza kumkabili Mzindakaya iwapo nyani wote huiba mahindi? Hii maana yake ni kwamba tangu awamu ya pili hadi ya sasa walijua uoza huu ila chini ya sera yao ya kujuana na kulindana waliamua kujifanya hawaoni. Hata hivyo, nani angemwajibisha Mzindakaya iwapo lao ni moja? Tabia hii ya kihalifu imeanza kugeuka kitu cha kawaida
 Kutokan ana ukweli kuwa Mzindakaya ni mwanachama wa Chukua Chako Mapema. Je tunao makupe wangapi nchini wakiiba na kuunyonya umma kwa kisingizio cha ukada na ukongwe katika taifa linalojisifu kuwa na mabilionea wa ghafla bin vuu baada ya kuacha siasa za Ujamaa? Hii ndiyo sababu kuu ya watanzania wengi kuendelea kuwa maskini wakati wachache wakitokea kuwa mabilionea. Mali ya umma haiumi japo umma unaumia.
          Tunaongelea kutwaliwa kwa nyumba za umma kwenye sakata la Mzindakaya. Je ni mali ya umma na ardhi kiasi gani makada hawa wasio na huruma na familia na marafiki zao wameishajitwalia tangu uhuru? Kichekesho ni pale ambapo wakati akina Mzindakaya wakijitwalia mali zetu huku watawala wakihangaika kofia mkononi wakiomba huku wakiwaacha wahalifu waendelee kuiba mali yetu. Kama mwizi mmoja anaweza kuiba nyumba za umma na kuzitumia kwa miaka 26, je ni kodi kiasi gani amekwepa kwenye biashara zake za kijambazi hasa ikizingatiwa kuwa wahalifu wengi wa namna hii ni wafanyabiashara hata kama ni ya chini ya meza pia. Hapa hatujaongelea utamaduni wa kijambazi ulioanza kuzoeleka ambapo vigogo na wezi hawa huwatafutia watoto wao nafasi nono serikalini na chamani ili kuendeleza ufalme wao haramu.
          Kashfa ya Mzindakaya ilipaswa kutufumbua macho na kutazama mbali zaidi hapa kwa kuhakikisha kila jiwe linafunuliwa na majambazi wote wanaojitwalia mali za umma wanawajibishwa haraka. Kutokupambana na genge hili hatari kwa uchumi na watu wetu ndiyo huo uvivu wa kufikiri. Maana wakiruhusiwa waendelee kama ilivyo, hatutakwepa mafarakano na umwagaji mkubwa baadaye ambapo wengi wasio nacho wataamua kuwakabili wachache walio nacho ili kupata haki yao. Ishara zimeishaanza kujionyesha ambapo watu wetu wamejiingiza kwenye jinai kama ujambazi na mihadarati ambako wakikamatwa wanapatilizwa. Hivyo, siku itafika watakapotambua kuwa kumbe hakuna haja ya kujiingiza kwenye jinai ili kupata maisha bora zaidi ya kushikamana na kuwanyang’anya wakubwa wezi wote mali walizoibia umma. Hakika, haya yatakuwa mapinduzi umma unaoyangojea kwa udi na uvumba.
Sijui umma unawachukuliaje waroho hawa wachache wanaosababisha mateso kwake kama alivyokaririwa mkazi wa Sumbawanga mjini Enos Budodi aliyekuwa na haya ya kusema,“Tatizo la uhaba wa nyumba ni changamoto kubwa sana mkoani hapa… imesababisha baadhi ya watumishi wanaopangiwa kuja kufanya kazi huku kukataa kuripoti au wanafika lakini wakiondoka  hawarudi tena.”
Bila serikali kuwachukulia hatua akina Mzindakaya ijue wazi inajenga mazingira mazuri ya fujo tuendako. Maana umma hautakubali kuendelea kusota wakati kuna watu wanaiba na kutumia mali zake na serikali ikiangalia na kutoa baraka zote. Mchezo huu mchafu usipositishwa na kumalizwa makada husika na chama chao wataliangamiza taifa nao wakiwamo. Ni upogo na upofu, uroho na roho mbaya kiasi gani?  Umma unapaswa kukataa na kupambana na jinai hii kabla haijaliangamiza taifa.Tieni akilini.
Chanzo: Dira Sept., 15, 20

2 comments: