Wednesday, 24 September 2014

Ndoa ya Polisi na CCM mauti ya taifa

Ukitaka kuandamana kirahisi nchini lazima ufanye jambo moja hata kama hulitaki wala haliingii akilini. Panga maandamano ya kuunga mkono upuuzi wowote unaofanywa na wenye madaraka kama kupewa tuzo zenye mashaka au kusema mambo ya kawaida lakini yakapakwa mkorogo na kuonekana si ya kawaida. Kwa ufupi, haki ya kufanya maandamano pamoja na kuwa ya kikatiba, si ya kila mtu hasa wale wanaopinga status quo. Wakati mwingine sioni tofauti baina ya zama za Zidumu Fikra za Mwenyekiti. Hali imezidi hadi nchi inahujumiwa na deni la taifa kuongezeka huku waathirika kama vile polisi wasilione hili!
Katika nchi ya “kidemokrasia” kama yetu, kuandamana ni haki ya kila mtu ila ina masharti hata kama si ya kikatiba. Wanaotaka kuandamana bila kupigwa wala kung’atwa na mbwa wa polisi shurti waunge mkono kila kitu kinachofanywa na serikali ambayo kwa nchi za uswekeni ndio wenye hati milki ya nchi.
          Hili utaliona jinsi polisi wanavyohamanika kuzuia maandamano kuliko ujambazi na jinai nyingine ambazo zimeichafua na kuihujumu nchi yetu. Si uzushi. Kwa sasa Tanzania inasifika kama njia kuu ya kusafirishia mihadarati huku watanzania wakisifika kuwa wabebaji na wauzaji wazuri. Polisi wameshindwa kuikomesha! Ukiuliza kwanini, utaambiwa hawana vifaa hata askari wa kutosha. Jibu ni hilo hili kwa kadhia ya ujambazi ambayo inalisumbua taifa ambapo imefikia hata watu kupigwa risasi na waporaji kwa sababu tu wamechukua fedha kichele toka benki.
          Polisi wa kupambana na uhalifu hawapo, wa kupambana na wanaandamanaji wapo sana tu. Mfano, hivi karibuni ni kule Arusha ambako magari manne ya polisi yalishinda yamezingira nyumba ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyekaririwa akisema, “Mimi naishi njia ya Momera Kijiji cha Ngurdoto. Tangu asubuhi polisi wamezingira nyumba yangu nikaona ili kutosababisha maafa nisitoke.”
          Ajabu polisi hao hao wanapoitwa kwenye matukio ya wizi wanachelewa ukiachia mbali kutoa visingizio lukuki kama kutokuwa na magari au magari kutokuwa na mafuta. Ajabu inapokuja kwenye kuzuia maandamano hata kuwaua kama ilivyotokea huko Arusha Januari 2013 polisi wana zana zote. Polisi hao hao wakiitwa kwenye matukio kama ajali za moto, magari yao hayana maji na upuuzi mwingine. Ajabu wanapokwenda kupambana na waaandamanaji magari yana maji ya washawasha ya bei mbaya ikilinganishwa na maji maalumu ya kuzimia moto! Serikali nayo haina pesa ya kuwalipa walimu, ina pesa ya kununulia mabomu ya machozi na maji ya washawasha! Hata pesa ya kununulia buti za askari haina, ina ya risasi za kuwamiminia waadamanaji. Haina pesa ya kusambaza huduma za afya, ina pesa ya kununulia magari ya kuzuia fujo mbwa na upuuzi mwingine!
          Je tatizo la polisi wetu ni vifaa na nguvu kazi au utashi tokana na kuchagua kutumiwa kisiasa badala ya kitaaluma? Je huu si ushahidi kuwa wengi wa wanaoteuliwa kuongoza jeshi la polisi ama polisi wenyewe ni makada, wanachama hata mashabiki wa chama tawala? Je hapa kuna utawala bora na wa sheria au uimla? Je polisi hawa hawana kadi za chama walizoficha wakionyesha ukereketwa wazi?  Haiingii akili kuona jeshi letu la polisi linapata sifa mbovu ya kuhujumu demokrasia na lisijisute. Je polisi hawajui kuwa si kila amri ni amri halali au ni ile hali ya jeshi kujazwa watu wenye elimu pungufu ukiachia mbali wengi kuw andugu wa polisi?
          Wakati umefika wa kutaka mabadiliko makubwa kwenye jeshi la polisi linalopaswa kuwa la umma na si la chama tawala kama ilivyo. Inakuwa vigumu kutofautisha polisi na wapenzi, makada na wanachama wa CCM. Kama hujuma hii itaendelea vurugu za kwanza zenye kulivuruga taifa zitaanzishwa na tabia ya polisi ya kulalia upande mmoja jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
          Japo wanaowatumia polisi na wanaojiruhusu kutumika vibaya waweza kujiridhisha kuwa watazima sauti za umma, watafanya hivyo kwa muda. Mambo yamebadilika. Welewa na madai ya wananchi vimeongezeka. Vijana wanataka atakayewapa hakikisho la kupata ajira na maisha bora. Wataunga mkono yoyote bila kujali ni chama tawala au pinzani. Na hali ilivyo, kutokana na uchovu wa miaka nenda rudi, ufisadi na kuishiwa visheni kwa chama tawala, mbadala wake uko kwenye upinzani. Hili ndilo linafanya chama tawala kuwatumia polisi kukinusuru bila kujua kuwa zamu itafika na polisi nao watajitambua na kujiona kama waathirika na kuachana na kutumiwa kama nepi.
          Tuliyaona haya DRC zama za kuangushwa kwa jambazi wa nchi ile Joseph Mobutu. Tuliyashuhudia Misri alipodondosha imla wa kule Hosni Mubarak. Ni bahati mbaya, watawala wetu wamenogewa ulaji kiasi cha kujisahau wakapingana na ukweli unatokana na wale wanaowanyanyasa. Polisi hawawezi kuendelea kupiga, kuamru mbwa wang’ate watu na kuuwa bado watu wakawapenda au kuwavumilia. Watawachukia tu na wale wanaowatumia. Bila kujitambua, polisi wetu wataliangamiza taifa nao wakiwamo. Maana ukiangalia ufisadi unavyoongezeka huku deni la taifa likifura na kutuathiri wote wakimwamo hata hao polisi, unashangaa mantiki ya jeshi la polisi. Hawaoni kuwa wanaowalinda wanazidisha umaskini wakati wao wakijineemesha? Je tatizo ni njaa ya ubongo au upogo wa kimfumo ambapo wengi wa wanaoshughulika na ulinzi na usalama wanafundishwa woga wa kijinga kiasi cha kubariki hata jinai?  Inakuwaje polisi wanavunja katiba kwa kuzuia maandamano wakati wakijua fika kinachopingwa ni cha kweli na halisi wasistuke? Inahitaji darasa kubwa kuliko hili.
Chanzo: Tanzania Daima  Sept., 24, 2014.

No comments: