Saturday, 27 September 2014

Mlevi kwenda The Hague kuwashitaki 'ndata'


Baada ya kugundua kuwa ndata wetu wamenogewa na
uonevu kwa walevi, mlevi anawataka waache ka-unafiki ka kufanya undata na siasa kwa pamoja wakati katiba inakataza. Baada ya kuwanyotoa roho walevi wengi wakiwamo waandishi wa umbea, tulidhani wangeshika adabu na kukoma na kutambua kuwa walevi nao ni watu.  
Walimnyotoa roho Dav Mwangosi. Tulivumilia. Walimtesa daktari Steve Ulimboka. Tuliminya. Walishindwa kuwakamata watesaji wa Absalim Kibanda. Tulikula pini. 
Inaonyesha wamegeuka ‘mbwa’ aliyeonja mayai.  
Dawa yake ni mpini ndipo kuku waokoke vinginevyo ukicheka naye unaula wa chuya.
Uonevu ulioonyeshwa na ndata hivi karibuni kwa kuruhusu mbwa kuwang’ata waandishi wa umbea si wa kuvumilia. Lazima tutoe tamko tena kwa herufi na sauti kubwa ili waelewe kuwa, tutachenchiana kama hawataacha.  
Hata wale wanaowaamuru kufanya huo unyama nao waache wakijua kuwa ulaji unaowatia kiburi unatokana na walevi hao hao wanaoamuru mbwa kuwaumiza. 
Nilipandwa na hasira nusu ya kurejea kwenye dojo kupiga karate ili nipambane na ndata ki-Bruce Lee kama siyo bi mkubwa kunizuia kwa kuwaonea huruma ndata wasio na huruma.  
Sijui ni kwa sababu kaka yake ni ndata?
Hakuna kitu kilinisononesha kama picha za vidosho wakikimbia wasing’atwe miguu na mbwa.  
Inabidi tuwaambie ndata kuwa hizo njuluku wanazolipwa kutufanyia unyama ni matokeo ya kodi zetu. 
Hata hao wanaowaamuru ni walaji na wanyonyaji wanaotegemea jasho na njuluku zetu.  
Wanapaswa kutuheshimu na kuheshimu haki na utu wetu kama binadamu. Kama ni kupimana misuli, nadhani Mboe saizi yake si ndata bali wanasiasa wenzake tena wenyeviti kama yeye. 
 Hivi hawa wanaomuandama kwa kuamriwa na maadui zake hawajui kuwa kibao kinaweza kugeuka akawa bosi wao siku moja?  Basi jamani undeni chama chenu cha siasa mkiite CPP yaani Cops’ and Politicos’ Party au anzisheni Chama Cha Polishi (CCP). 
Kwa vile inaonyesha kuwa wao na mabosi wao hawasikii, napanga kwenda zangu The Hague kufungua kesi dhidi yao.  
Wanaweza kudhani natishia kilevi na kibangi bangi, si kweli. 
Kwanza, yule bibie Bensoda ni mwanafunzi wangu wa sheria ukiachia mbali afisa mkuu bwana Mochochoko kuwa mshirika wangu.  
Hivyo, nikiamua nao wanaweza kunyea debe tena si kwa kesi za kubambikizwa kama zile wanazowabambikia walevi. 
Nasikia walitaka kumtia adabu Mboe eti kwa kutaka kusababisha vurugu! Hayoo! Hivi kati ya Mboe na nyinyi nani anasababisha vurugu? Mbona wapo vingunge waliotishia kupindua kaya hamkuwakamata au mnatenda kwa upendeleo na woga?  
Hivi kweli kuna vurugu kama kutishia kuangusha lisirikali la kaya hata kama ni la hovyo? Mbona Mura Were alipotishia kumkata shingo Kafulia tena kwa kumwita nyani asijue nyani wanasabisha ebola hamkumshughulikia? 
Mbona wenzenu walivyokwapua mshiko pale kwenye kituo cha Msimbazini Kariakooni hamkuwakamata au mnadhani tumesahau?  
Acheni unafiki wa kuchagua makosa wakati yote ni makosa. Kinachoshangaza ni ile hali ya ndata kushindwa kutambua kuwa hao wanaowapiga na kuwaonea ni ndugu zao.  Ni wajomba, shangazi, mama, watoto, baba, babu na jamaa zao.  
Hili halihitaji shahada wala bangi nyingi.  Hawa mnaowatesa wanafanana sana nanyi kuliko hao wanaowatumia.  Wanaishi kwenye mbavu za mbwa za wenyewe wakiwadhalilisha na kuwahangaisha sawa nanyi. Wanaishi kwa kubanana sawa nanyi. 
Wengi wao hata viatu vyao vimesagika soli sawa nanyi kwa kuponda mguu kutokana na ukapa. 
Hao wanaowatumia nanyi mkawatumikia wala hawafanani nanyi.  Wao wanaishi kwenye mahekalu mnayolinda usiku na mchana.  Wanalipiwa pango la hekalu na kodi za walevi.  
Wanatanua tena si wao tu bali hata na watoto, marafiki na waramba viatu wao kwa kodi hiyo hiyo. 
Pia hao mnaowadharau wanawadharau kama mnavyowadharau mbwa mnaofungulia wawaume walevi.  
Hivi kweli kuna siku mliwahi kufikiria kuwapa heshima mbwa wenu hao? 
Basi hali ni hiyo hiyo kwa upande wa pili. 
Anayekudharau hukutumia au kukuamuru kufanya mambo ya hovyo kama kuonea walevi. Hivi walevi wakiungana wakaamua kuwatokea na michupa yao mtaweza kuwazuia kwa wingi na ulevi wao? Thubutu yenu! Mnadhani wataendelea kutojitambua? Nadhani mnavyowatenza ni uamsho na kumbushio tosha kuwa waamke wapambane na uovu bila kujali aliyeko nyuma ya uovu huu.  
Hata hivyo, ndata mna bahati. Kati ya vimwana waliotishiwa kuraruriwa mapaja na midog yenu angekuwamo bi mkubwa wangu mbona ningenyotoa watu roho kwa karate kung-fu, jet kune do na madudu mengine yenye majina magumu yakijapani ambayo ninayamanya kama sina akili nzuri.  
Mie ni sensei wa nguvu ati!         Huwa napiga hakuna mfano. 
Nakumbuka wakati nikisomea hii fani niliwahi kuwachapa walimu wangu mpaka wakasema kuwa hawakuwa wamewahi kuwa na mwanafunzi kama mimi. 
 Hivyo, walinipa usensei kabla ya hata kumaliza robo ya mafunzo. Hayo tuyaache.
Kwa vile ninapaswa kuwahi sehemu kupata msokoto na kichupa lau kuamsha akili, kwa leo naishia hapa niwatahadharisha ndata kuacha uonevu, vinginevyo mzee mzima nitaingia mtaani full masnonda.  Na nikiingia tusilaumiane kwa yatakayowapata.  
By the way, kama ndata wanaona siasa ni dili si waanzishe chama na kuendelea kuvaa magwanda yao kama wenzao wa Chakudema ambao wanatunishiana misuli nao wasijue kesho wanaweza kuwa mabosi wao. 
CHANZO: NIPASHE 

No comments: