Tuesday, 9 September 2014

Je Zitto Kabwe amekumbuka blanketi asubuhi?

          
Hivi karibuni vyombo vya habari zilizomkariri Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe akiwalaumu wapambe kwa kumchonganisha na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe. Hii ni baada ya Kabwe kukumbwa na shoka la CHADEMA dhidi ya wale kilichowaita wasaliti. Hadi taarifa hizi zinatoka, Kabwe aliishafukuzwa CHADEMA. Anaendelea na ubunge kwa amri ya mahakama kutokana na shauri juu ya kufukuzwa kwake kuwa mahakamani.
          Kabwe alikaririwa akisema, “Sina shida yoyote na Mbowe, naamini ipo siku tutagundua wapambe walituathiri na ndiyo waliotufikisha hapa.” Ni kweli. Kabwe na Mbowe hawana shida kama watu binafsi.  Kabwe ana shida na chama alichotaka kukisaliti kutokana na ushahidi uliotolewa dhidi yake akashindwa kuukanusha au kuuvunja.
Wapo wanaodhani Kabwe amekumbuka blanketi asubuhi. Wanaona kuwa, hata asingizie shetani, hafai kurejeshwa kundini. Pia wapo wanaodhani kuwa wanaweza kuyaongea na kuyamaliza.  Je ni kwanini Kabwe ameliona hili akiwa amechelewa hivi? Je ni ukweli kuwa kuna watu waliwachonganisha Kabwe na Mbowe? Je Kabwe anamaanisha kuwa mashtaka ya kusaliti na kuhujumu chama ni ya uongo? Je kwanini hakuyaona haya mapema na kumwendea Mbowe wakayamaliza? Je tatizo ni baina ya Kabwe na Mbowe au Kabwe na CHADEMA? Maswali ni mengi kuliko majibu.
          Kwa waliofuatilia mtafaruko mzima watakubaliana nasi kuwa tatizo la kufukuzwa kwa Kabwe siyo tofauti binafsi baina yake na Mbowe. Kabwe alikufukuzwa baada ya kugundulika waraka uliokuwa unalenga kuhujumu chama. Pia ifahamike.  Kama kuna adui ambaye Kabwe anapaswa kumlaumu, si mwingine bali yeye mwenyewe, hasa kiu yake ya madaraka. Hivyo, Kabwe hana haja ya kumsaka mchawi. Na kilio chake kinaweza kuchukuliwa kama machozi ya mamba hata kitubio cha kweli. Inategemea na unavyoliangalia suala zima.
          Je inawezekana kuwa Kabwe amegundua kuwa mpango wake wa kuanzisha chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT), umegonga mwamba kiasi cha kutamani asamehewe na kurejeshwa kundini?  Je CHADEMA watamsikiliza na kutimiza anachotaka? Je kama watafanya hivyo, watamwamini tena? Je hapo baadaye hawezi kukikomoa chama na kuondoka wakati wakimhitaji?
          Kwa hali ilivyo,Kabwe amenasa.  Haoni pa kutokea isipokuwa kurejea kundini jambo ambalo laweza kuwa gumu sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano. Kuonyesha alivyokwama, Kabwe alikaririwa akijipa matumaini ya kurejeshwa kundini pale aliposema, “Hivyo ndivyo ninavyoiona na huko mbele usishangae kuona tunafanya kazi pamoja. Kwangu mimi nimeshasahau kila kitu nimelia Umra na kila kitu nimesamehe.” Je wahusika wako tayari kumsamehe hasa ikizingatiwa kuwa sakata lake lilikipa chama wakati mgumu ambapo kiliingia kwenye kutoa maelezo badala ya kukabiliana na uhuni kinaofanyiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)? Je gharama na hasara alizokisababishia CHADEMA zinaweza kusahaulika na Kabwe akasamehewa?
          Wapo wanaodhani kuwa, licha ya tamaa ya madaraka, Kabwe anatumiwa na CCM kuihujumu CHADEMA. Katika hili Kabwe alikiri kwa kusema, “Moja ya vitu ambavyo nashutumiwa na wenzangu ni kwamba mimi natumiwa na CCM lakini haijawahi kutokea kiongozi yeyote wa chama hicho, licha ya kuwa na uhusiano nao mzuri, kunitaka nijiunge nacho.” Je kusema kuwa ana uhusiana mzuri na CCM na hakuna aliyewahi kumtaka ajiunge nacho kunatosha kufuta tuhuma? Kwanini Kabwe hakuwataka CHADEMA na wale wote wanaodai anatumiwa na CCM kuthibitisha kama hakuna namna?
          Pamoja na kukanusha kutumiwa na CCM na kusema kuwa hakuna aliyewahi kumtaka ajiunge nacho, Kabwe alijichanganya aliposema, “Niishie kusema kwamba viongozi wengi sana nimezungumza nao. Wapo walionipa pole kwa yaliyonikuta na wengine kuniomba niungane nao, lakini sikuona sababu ya kutoka chama hiki kwenda chama kingine. Utapata faida ya siku mbili tatu katika kurasa za mbele za magazeti kuwa Zitto kaingia chama fulani lakini hutapata sustainable benefit (manufaa ya kudumu).” Je hawa “viongozi wengi” aliozungumza nao ni wa vyama gani? Hata hivyo, Kabwe amegundua kitu kimoja muhimu. Anasema, “… lakini sikuona sababu ya kutoka chama hiki kwenda chama kingine. Utapata faida ya siku mbili tatu katika kurasa za mbele za magazeti kuwa Zitto kaingia chama fulani lakini hutapata sustainable benefit (manufaa ya kudumu).” Hili ni kweli. Hata katika makala yetu ya Je ACT itakufa kabla ya kuzaliwa? Tuligusia hili kwa kumpa mifano ya watu kama Dk. Masumbuko Lamwai, Dk. Warid Kaboro, Augustine Mrema na wengine ambao walilewa umaarufu ndani ya vyama vyao wakavihama na kuporomoka huku wengi wakihadaiwa na CCM na kupewa ulaji wa muda halafu baadaye wakatupwa kwenye jalala la taka kisiasa. Je Kabwe ndiyo amelijua hili?
          Japo kukiri makosa na kuomba msamaha ni uungwana, wakati mwingine ni kupoteza muda hasa makosa yenyewe yanapokuwa yatokanayo na kuvunja uaminifu, kupanga uasi, kutumiwa na maadui na hata kupoteza muda na fedha za chama kwenye kesi. Je CHADEMA watatumia usemi kuwa hakuna adui wa kudumu kisiasa bali maslahi ya kudumu, hivyo watakaa na kuyamaliza na Kabwe? Je watampa masharti gani ili asiwarejeshe waliko? Je Kabwe yuko tayari kuomba msamaha hadharani ndipo CHADEMA wamfikirie? Tunangoja kusikia upande wa pili. Je Kabwe amekumbuka blanketi asubuhi? Time will nicely and accurately tell.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 10, 2014.

No comments: