Saturday, 20 September 2014

UDA: Serikali imebariki ufisadi?

          Vyombo vya habari hivi karibuni vilimwonyesha waziri wa Serikali za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Bi. Hawa Ghasia pamoja na na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Meck Sadiki wakishuhudia utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano baina ya UDA na wamiliki wa daladala ili kushinda zabuni ya kuendesha Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi (DART). Kwa vigogo hawa wa serikali kuhudhuria, bila shaka, UDA ilitoka kwenye hafla hii kifua mbele ikithitibisha kushinda vita ya kulitwaa na kuliendesha shirika hili kiujanjaujanja. Utiaji saini huu ulifanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere hivi karibuni.
Kwa wanaokumbuka majibu ya waziri mdogo wa Fedha, Adam Malima mbele ya bunge alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kawe Halima Mdee (CHADEMA) aliyetaka kujua maelezo kuhusiana na hisa za UDA, wameshangaa na kukatishwa tamaa. Malima alikaririwa akisema, “Jiji la Dar es Salaam lina hisa 51katika UDA na serikali ina hisa 49.” Baada ya UDA kuendelea kujitangaza na kujitanua, wengi wanauliza: Hizo hisa 49 zimeuzwa lini na kwa bei gani iwapo serikali ilisema bado inashikilia hisa zake? Je zabuni ya kufanya hivyo ilitangazwa lini? Je Malima alikuwa akidanganya umma au kusema mambo asiyo nayo uhakika? Je kitendo cha waziri mwenzake na mkuu wa mkoa kushuhudia utiaji saini tajwa siyo kuihalalisha UDA kinyemela? Je huku siyo kupingana baina ya watendaji wa serikali? Je ukweli hapa ni upi?
Kuonyesha namna serikali inavyojikanganya huku watendaji wake wakipingana wazi na hadharani, Ghasia alimpongeza Mkurugenzi  Mtendaji wa UDA, Robert Kisena na viongozi wa vyama vya wamiliki wa daladala mkoani humo kwa uamuzi huo wenye tija kwa Taifa kwani utaongeza ajira na kupunguza umaskini. Ni bahati mbaya waziri hakuonyesha hiyo tija na ahadi ya kuongeza ajira. Ajira gani na tija ipi iwapo wamilki wa Dala dala wanaendelea kuminywa na kuondolewa kwenye biashara na UDA?
Naye Sadiki alikaririwa akisema, “Serikali inatambua jitihada zinazofanywa na wazawa kwani haiwezi kutumia mabilioni ya fedha kujenga barabara hizo halafu mtu wa kuziendesha atoke nje, hii itakuwa aibu na dharau.”
Sadiki aliongeza, “Kuungana kwenu, kutaishawishi Serikali baada ya kutangazwa zabuni, ianze kuwafikiria nyinyi kwa kuwapa kipaumbele kwani hii ni ishara kwamba, mmedhamiria kupambana katika zabuni.” Huu ni ushahidi kuwa UDA, pamoja na kufahamika kuwa ilipatikana kifisadi kama alivyowahi kudai mbunge wa Temeke Abbas Mtemvu, ni kama imeishashinda zabuni husika. Je huu ndiyo uwazi na utawala bora kwenye kuendesha shughuli za umma? Je kwanini Ghasia na Sadiki wameamua kubariki kitu haramu wakijua fika msimamo wa serikali? Je wana maslahi binafsi UDA? Kwanini hawataji maslahi yao binafsi kabla ya kutoa matamko na pongezi kwa kampuni ambayo bado hajasafishwa na kanuni? Kwanini Sadiki analeta sera ya uzawa iliyokataliwa wazi wazi na serikali anayoitumikia? Je kigezo cha mtu kupata zabuni ni uzawa au sifa stahiki za kuendesha mradi husika? Je huu si ubaguzi? Inakuwaje ujenzi wa barabara tena unaotegemea pesa za nje uwanufaishe wazawa pekee hata kama hawafai? Nadhani namna hii tutaangukia pua hasa ikizingatiwa kuwa mataifa yaliyoendelea hayakuzingatia uzawa katika kutoa zabuni. Mfano mdogo ni wafanyabiashara matajiri wa Mashariki ya Kati kuruhusiwa kuwekeza kwenye nchi kama Marekani na Uingereza kwa vile wana mtaji na sifa za kuendesha miradi husika.
Kuonyesha UDA inavyohalalishwa kinyemela kwa joho la uzawa, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala mkoani humo (DARCOBOA), Sabri Mabrouk alikaririwa akikoleza moto wa uzawa akisema, “Hakuna sababu ya kumwachia mtu kutoka nje aje kuendesha mradi huu, tukikusanya mitaji tukaungana na UDA, tutaweza kuendesha mradi huu kwani hauhitaji fedha nyingi sana, tukiamua tunaweza.” Kumbe watu wenyewe hata mitaji hawana!
Wakati wa kufanya biashara kwa kanuni za biashara badala ya kujuana umefika. Japo ni haki yao kuunga mkono UDA au la, viongozi wa serikali inabidi watangaze maslahi yao kwanza huku wakiepuka kupingana. Watanzania, hasa wakazi wa Dar es Salaam wenye UDA yao, wangependa kujua ukweli kuhusu umilki wa UDA unaoendelea kuwa utata mtupu huku Kisena akiendelea kutambuliwa kinyume cha hali halisi. Wengi wangetaka kujua kama huyu Kisena amepata mtaji wake kihalali au anatumiwa na vigogo wa serikali hii hii kama alivyodai Mtemvu kuwa nyuma ya UDA kuna vigogo kama vile waziri wa zamani Prof Juma Kapuya ambaye hajawahi kukanusha vilivyo kwa hoja zinazoingia akilini.
Pia kuna fununu kuwa mtoto wa kigogo mmoja wa nchi ambaye ni rafiki mkubwa wa Kisena ndiye mwenye mradi mzima. Mtoto huyu ambaye ameingia bungeni hivi karibuni anakumbukwa kwa alivyofanya kila hila kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 kwa kulazimisha jina la kada maarufu wa CCM na mbunge wa wakati ule John Magale Shibuda kukatwa huku Kisena akigombea na kushindwa na Shibuda baada ya kuhamia CHADEMA. Je huu si ushahidi tosha kuwa UDA inahujumiwa na kutwaliwa kwa vile kuna vigogo nyuma yake? Je haiwezekani kuwa huyu mtoto wa kigogo wa serikali anasimamia mradi wa baba yake anayesifika kwa kigeugeu? Sijui tunamkomoa nani kwa kukwapua mali ya umma na ya wananchi kwa kisingizio cha uzawa na upuuzi mwingine? Kwanini leo wazawa waonekane wa maana iwapo ndiyo hao hao waliozamisha miradi ya umma kwa kuiibia na sasa kuiiba chini ya visingizio mbali mbali. Je waziri Malima anatwambia nini kuhusiana na hisa 49 za serikali? Je Malima atakuwa tayari kusimamia ukweli hata kama ni kwa kupoteza kitumbua chake au amenyamazishwa kwa vile wenye UDA ni mabosi wake?
Chanzo: Tanzania Daima Sept,.16, 2014,

No comments: