Tuesday, 9 September 2014

Kijiwe chataka wabunge wawe na PhD

Baaada ya Bonge la Mizengwe ya Kuchakachua Katiba (BMK) kuendelea na uovu wake, Kijiwe hakitaki kushiriki hii dhambi kwa kaya. Eti limependekeza waishiwa wajue kusoma na kuandika tu na hiyo iwe ndiyo sifa ya kugombea ulaji!  Hivyo, tumekaa kama kamati kujadili na kupitisha baadhi ya mambo ambayo yanakwenda ndivyo siyo. Hatuwezi kunyamazishwa wala kugeuzwa mabunge wote. Hivyo, Kijiwe cha leo kimekaa kama Umoja wa kutetea Katiba ya Wachovu (UKAWA) ili kuweka mambo sawa tayari kwa historia kukandikwa kuwa lau tulithubutu.
Mpemba ambaye leo anaonekana kuwa na bashasha analianzisha, “Yakhe mmesikia huu utwahuti wa kuendelea kutukuza ujinga na kudhalilisha na kuikana ilmu?”
Mgosi Machungi anajibu, “Mbona eimu iliuawa miaka mingi na kughushi kuhaaishwa. Unaongeea utwahuti gani wakati kaya imegeuka kuwa ya matwahuti na wababaishaji kisanii?”
Mpemba anajibu, “Naongelea huu upuuzi wa kupinga pendekezo la Tume ya Waryuba kuwa lazima wahishimiwa angalau wawe wamesoma na kuhitimu kidato cha nne bila kughushi.”
Kapende anaamua kupoka mic, “Kumbe unaongelea huu uchakachuaji wa Katiba uliolenga kunufaisha wasaka tonge kisiasa baada wengi wao kuogopa umande siyo?”
Mijjinga hangoji Mpemba ajibu. Anakwanyua mic, “Nimesoma hii habari kwenye gazeti la Mawenge la leo. Hata hivyo, nina mawazo tofauti. Napendekeza wahishimiwa wote wawe na PhD kama sisi wana kijiwe. Mnaonaje?”
Mipawa, leo kala bonge la kanzu na kofia ya tarabushi na kuonekana kama bonge la shehe, anaamua kutia daruga, “Nkwinga nakubaliana nawe mia kwa mia hasa ikizingatiwa kuwa kughushi ni rahisi na kumehalalishwa na wanaofanya hivyo hawashughulikiwi zaidi ya kufumbiwa macho na kuongezewa vyeo.”
Msomi Mkatatamaa akamua mic, “Japo msemayo yanaweza kuchukuliwa kama utani, tunapaswa kuzingatia kuwa bila kuwa na wawakilishi wasomi wataburuzwa kirahisi. Hivyo, nakubaliana na pendekezo kuwa wawe na PhD.”
Mzee Maneno anaamua kumpinga Msomi akisema, “Wasomi wamefanya nini zaidi ya kueneza ufisadi na rushwa hata za ngono? Je wao hawaburuzwi pamoja na usomi wao au wote ni vihiyo walioghushi?”
Mbwa Mwitu aliyekuwa akifunga kamba ya kiatu chake vizuri anachomekea, “Kama mbaya mbaya. Mie napendekeza wasijue kusoma wala kuandika bali wawe na uwezo wa kusema, yaani kutoa ahadi lukuki kwa wapiga kura, kuuchapa usingizi mjengoni na kuunga mkono hoja hata kama ni mfu za chama.”
Kijiwe hakina mbavu kwa pendekezo hili la aina yake.
Kapende anarejea huku akimtazama Sofi Lion aka Kanungaembe ambaye siku zote ni mbaya wake. Anasema, “Mie napendekeza wanaogombea uishiwa wawe na nyumba ndogo nyingi. Kama ni mama ambaye hajaolewa, ajue kuwawowa vijana kama yule aliyedaiwa kumuwowa kijana na ndoa ikafungwa na kaunungaembe fulani kaitwako Gettie Rwakatarehe ambako huwahadaa akina mama kuwa kanaweza kuwapatia mume wakati kenyewe hakana huyo mrume.”
Kijiwe kinaangua kicheko kwa jinsi Kapende anavyorusha vimondo.
Sofi kashikwa pabaya! Anaamua kula mic, “Mambo ya kuolewa kuoa au kutooa yanahusiana nini na uhishimiwa jamani? Mbona mnaleta mambo ya kihuni kwenye mambo ya maana hivi?”
Mijjinga anaamua naye kumchapa mbaya wake Sofi kwa kusema, “Ndoa lazima ati. Kwanza, kwa kuwa wameoa au kuolewa, wataepusha kuchukuana huko mjengoni kama alivyowahi kusema muishiwa mmoja kuwa kila mmoja ana wake mjengoni. Pili, kama mtu ameshindwa kuwa na familia yenye kuheshimika, atawezaje kuwakilisha wachovu? Lazima ajue uchungu na umuhimu wa familia na ndoa au vipi washirika?”
“Da unaonea kama mtume Paulo wa Wadanganyika wa Kikolito!” Anazoa Mchunguliaji.
Mpemba anarejea kwa chati na kusema, “Mie naona lazima wajue lau Kiswahili na kimombo vilivo. Nani anataka mijitu iniyochanganya lugha hadi inaongea kishwangilish?”
Kanji aliyekuwa akitetea chini chini jambo na Sofi anaamua kutia timu, “Mimi ona yote sema hapana shiko. Kama vatu nachagua mtu napenda yeye basi tosha. Kama soma au hapana soma yote sava.”
 Mheshimiwa Bwege aliyekuwa kimya kitambo anaamua kuvaa jezi na kupeta, “Kwa vile wanachaguliwa kwenda kutunga sheria, basi napendekeza angalau wawe wamesoma sheria ili aweze kubaini wizi kwenye mikataba ya kijambazi inayoendelea kufilisi kaya yetu kipumbavu.”
Hata kabla ya Mheshimwa Bwege kuendelea, Mzee Ndomo anakula mic, “Kwani hao wanaowasaidia wezi wanaoitwa wawekezaji wakati ni wachukuaji si wamesoma sheria wakaamua kuitumia vibaya sawa na wanaotumia madaraka vibaya?”
Mbwamwitu anachomekea haraka, “Mmesahau sifa nyingine adhimu. Wawe ni watoto au wake wa vigogo au wanaotoka kwenye koo tawala.”
Msomi ambaye alikuwa kimya kitambo anaamua kumwaga pwenti, “Tuache utani. Hata kutaka wawe na PhD unaweza kuwa utani, lazima wawe wameelimika vilivyo na si kughushi wala kuokoteza kama ilivyo. Wakiwa wasomi, licha ya kufufua uchumi, watathamini elimu na kuhakikisha haibakwi na akina Kawadog. Nadhani kinachofanya watu wapende kuwa na wawakilishi vihiyo au walioghushi ni mfumo uliopo. Hapa lazima tubadili mfumo mzima kuanzia kuzuia uchakachuliwaji wa Katiba na kuandika Katiba safi wenyewe tukisema wazi kuwa ufisadi uwe wa kughushi, kiuchumi na kimaadili ni makosa ya jinai yenye kupewa adhabu ya kifungo cha maisha.”
Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si tukasikia sauti ya mwizi!
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 19, 2014.

No comments: