Wednesday, 3 September 2014

Katiba mpya: Sitta amepewa kitanzi ajimalize?

          Alipoenguliwa kwenye kugombea tena nafasi ya spika wa Bunge, Spika wa zamani, Samuel Sitta, (Mkiti wa Bunge Maalum la Katiba (BMK), alitikisika sana. Wengi waliona kama alikuwa amekwisha hasa baada ya kuibuliwa kwa mtu ambaye hana sifa wala uwezo wa kuendesha bunge, Anna Makinda spika wa sasa wa bunge. Taratibu, fununu zilianza kusambaa kuwa alikuwa akipanga kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama kipya Cha Jamii (CCJ) ambacho bahati mbaya au nzuri kilikufa kabla ya kuzaliwa baada ya Sitta na vigogo wenzake walioamuru kianzishwe kutojiunga nacho. Kwa mujibu wa mwanzilishi wa chama hiki, Fredrick Mpendazoe aliyetoa kafara ubunge wake na kuachwa Solemba, Sitta, Harrison Mwakyembe na Stella Manyanya walikuwa nyuma ya kuanzishwa kwake. Hata hivyo, mambo hayakwenda kama yalivyokuwa yamepangwa. Hii ni baada ya Sitta na wenzake kupewa uwaziri na mwingine ukuu wa mkoa kiasi cha kurejesha angalau ulaji.
          Angalau Sitta alikuwa amepata nafuu kidogo. Nafuu kubwa ilikuja baada ya CCM kumkubalia agombea uspika wa BMK ambao bila shaka, kwake aliona ni karata ya kurejea kwenye ulaji na mipango yake ya kuutaka urais asijue ulikuwa ni mtego hata kitanzi vitakavyommaliza hasa baada ya kuwa nyenzo kwenye kuvurunda mchakato mzima. Kimsingi, kama alivyotumiwa na rais Jakaya Kikwete na CCM kuepusha balaa la kutupwa nje kwenye kashfa ya Richmond ambayo ilimwondoa swahiba na mshirika mkuu wa Kikwete, Edward Lowassa, Sitta aliona kama anarejea kileleni asijue bado utakuwa mtihani mgumu kwa majaliwa yake kisiasa. Tazama sasa anavyosakamwa kuliko hata Kikwete mwenyewe ambaye kumvizia kwake mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba jaji Joseph Warioba kuliwezeshwa na Sitta mwenyewe.
          Je ni kwanini Sitta amepewa kitanzi ajimalize kama siyo kummaliza?
Kwanza, CCM walijua fika kuwa ukitaka kumkomesha mchawi, mwachie mtoto. Kwa kupewa uspika wa BMK wakati Kikwete na CCM wakijua wazi kuwa kitakachoandikwa si katiba iliyokusudiwa, walijua fika kuwa Sitta atakuwa amejiongezea maadui kisiasa. Hili unaweza kuliona kwa jinsi anavyosakamwa kwa kuvuruga na kukwamisha mchakato mzima. Sitta, kwa sasa anabeba dhambi ya kuruhusu fedha ya umma iendelee kuibiwa kwa kuwalipa wajumbe wa bunge ambalo mwisho wa siku hatalitafanikiwa kuandika katiba mpya hasa baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuamua kujitoa na kufanya uwezekano wa kupatika akidi kutoweka. Hivyo, chuki toka kwa wananchi wanaoathiriwa na kuendelea kwa BMK ni pigo la kwanza kwa Sitta.
          Pili, Katiba mpya isipoandikwa, atakayeathirikia na kulaumiwa sana kisiasa ni Sitta hasa ikizigatiwa kuwa Kikwete haweza kugombea cheo chochote kisiasa kisheria.
          Tatu, kwa kuendelea kumsakama na kumdhalilisha jaji Warioba ambaye ametokea kuwa kipenzi cha watanzania kutokana na msimamo wake, kutamwongezea Sitta maadui.  Juzi juzi tu alimwita mpotoshaji hata aliposema ukweli mtupu baada ya kufanya mdahalo kwenye runinga ya ITV ambapo Sitta alikaririwa akisema, “Wajumbe wa tume kazi yao ilishamalizika, lakini sasa hivi kazi zao kila siku ni hili Bunge na kupotosha, ongeeni na wazee wenzenu muwaambie waache, waambieni muda wao umeisha.” Japo Warioba hashiriki tena siasa kama mchezaji, ana ufuasi na uungwaji mkono si haba. Hivyo, hali hii itazidi kumweka pabaya Sitta.
          Nne, baadaye maadui zake na washindani wake wa kisiasa ndani ya chama chake watatumia nafasi hii kumwosha Sitta kama mtu asiyefaa kuongoza nchi.  Watamgeuka ingawa kwa sasa wanajifanya kuwa naye katika kuendelea kuvurunda. Wanatumia ile falsafa kuwa adui yako akikosea usimkosoe ili akosee zaidi.Watahoji kwa nguvu zote: Iwapo ameshindwa kuongoza bunge tu na kulipatia taifa katiba mpya, atawezaje kuongoza nchi ambayo atakuwa ameiangusha kwa kuinyima katiba mpya? Na kweli, atawezaje kuongoza nchi wakati ameshindwa bunge la watu wachache tu?
          Tano, kitendo cha Sitta kuendelea kudanganywa na CCM kuendelea na vikao vya BMK kitamponza sana. Atabebeshwa kila lawama kwa vile ameshindwa kuona mtego aliyomo akidhani kuwa ni fursa ya kujijenga kisiasa asijue anajibomoa.  Sitta ameshindwa kuelewa kuwa suala la Katiba mpya si la CCM wala UKAWA bali la kitaifa.
          Sita, Sitta bila shaka hata kama atagundua alivyotegwa na kutoswa, atajaribu kufurukuta asifanikiwe. Laiti angesoma mawazo ya baadhi ya wabunge na vigogo wa CCM walioamua kutoa misimamo dhidi ya kuendelea kwa vikao vya BMK hasa baada ya kugundua kuwa wapiga kura wao hawakubaliani na kuendelea kwa bunge. Hivyo, ili kuepuka kwenda na maji kwenye uchaguzi ujao, baadhi ya wabunge tena wenye ushawishi chamani kama vile Mwigulu Nchemba, Ridhiwani Kikwete,Ali Kessy, James Lembeli, Ester Bulaya, Ignas Malocha na wengine ambao wanaogopa chama tu lakini hawakubaliani na kuendelea kwa BMK wamejaribu kujitenga na zoezi zima.
Je Sitta ni nani asiangushwe na ushiriki wake kwenye kuvuruga mchakato wa Katiba mpya huku akiendelea kubariki fedha za walipa kodi kupotea kwenye kulipa wajumbe ilhali wakijua hawataandika katiba mpya na kama wataiandika haitakuwa ya wananchi bali ya CCM? Hakika Sitta amepewa kitanzi ajimalize mwenyewe. Na kweli, atajimaliza. Kwa vile, sikio la kufa halisikii dawa.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 3, 2014.

No comments: