Wednesday, 24 September 2014

Kijiwe kufanya matamasha ya akili

Baada ya wanakijiwe kupiga kele bila kueleweka wala kusikika, wamegundua kuwa kumbe tatizo pamoja na kuwa na utawala msonge na mchafu,ni wachovu wenyewe yaani wanakaya.  Hivyo wamekuja na mbinu ya kupamban an hali iliyopo hasa kuweza kuokoa kaya kwa kuzuia utwahuti unaoendelea kufanywa na akina Njaa Kaya, Mura Were-ma, Saada Mkuyati, Sam Sixx na manyang’au wengine.
          Mgosi Machungi baada ya kuamkua anasema, “Timechoka kugeuzwa kaya vibua tukiiwa na kila wasaka tonge. Baada ya kusukuti ni kwanini kaya yetu has gone to dogs, nimegundua kuwa tatizo ni wana kaya wenyewe.”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa ametoka kumwonyesha Mijjinga jinsi gunia lilivyomchubua, anakatua mic na kusema akimtazama Mgosi, “Umegundua nini?”
 “Nimegundua kuwa kumbe akii za watu wetu zimevia kutokana na kuchezewa mahepe. Kama utachunguza utagundua kuwa kia kuna mwaka matamasha ya kutafuta vipaji vya kunengua, mibaba kukuna nazi, kuchoma nyama, kukimbiza kuku, kunywa bia na upuuzi mwingine. Je timeidhika kuwa kaya ya wanangeuaji?
“Da Mgosi kweli wewe ni daktari nimeamini!” Anachomekea Mbwamwitu.
“Kwani siku zote uikuwa hujui! Mimi ni daktai wa kwei kuiko akina Merry Nyagu, Makoongo Muhanga, Emmy Nchimbi na wengine wengi waioghushi.”
Mbwamwitu anachomekea kwa utani, “Hebu muuza mmwagie Mgosi hadi azimie.”
Mgosi hakubali. Anakatua mic, “Kijana chunga tabia yako. Unawezaje kusema eti animwagie hadi nizimie?”
“Mgosi usinielewe vibaya. Namaanisha akuwekee kahawa hadi uchoke mwenyewe.” Anajitete Mbwamwitu.
Msomi kuona utani unaanza kuharibu hoja anakwanyua mic, “Kusema ukweli uchambuzi na utafiti wako umefumbua mcho. Japo najua vyanzo vingi vya matatizo ya watu wetu, sikujua hili kusema ule ukweli pamoja na utaalamu wangu.
Mgosi anatabasamu huku akibwia kahawa yake na kashata. Meno yote nje akifurahi kumwagiwa ujiko.
Msomi anaendelea, “Hivi ukichunguza baina ya vijana na wazee nani anaathirika na upuuzi unaoendelea? Wazee wengi tena hawa wanaotuburuza kama wataishi sana hawawezi kuzidi miaka 20. Je, kwa mfano, wanapochakachua ambayo itakuwapo miaka 100 ijayo anayeathirika vibaya ni nani?”
Wanakijiwe wanajibu, “Vijana.”
Anaendelea, “Je kwa sasa ni nani wanakula utamu wa kaya hasa wenye ajira zao binafsi na watu wao?”
Wanakijiwe wanajibu tena, “Wazee.”
Je ni nani waliasisi matatizo hasa ya ufisadi tunaoshuhudia?”
Wanakijiwe wanajibu kwa pamoja isipokuwa Sofia Lion aka Kanunga embe na Kanji, “Wazee.”
Je ni nani wanaoonyesha kuishiwa mawazo, kupitwa wakati na kukataa kukua,?”
Kama kwa wanakijiwe wanajibu kwa pamoja isipokuwa wale mahabithi wawili, “Wazee.”
“Je ni nani atalipa zigo la madeni wanalosababisha kwa kukopa kuiba na kutanua?”
Wanajibu, “Vijana.”
Msomi anaendelea bila kuulizwa swali, “Ukilinganisha majibu mliyotoa, utagundua kuwa kuna pande mbili kuu yaani walaji ambao wengi ni wazee na watakaolipa wasichokula ambao ni vijana. Kwa taarifa yenu vijana, watoto na akina mama ndiyo wengi kayani na ndiyo wenye kuteseka kwa makosa yaw engine. Je ni kitu gani kimewafanya waridhike na jinai hii?”
Kila mmoja anatafuta jibu. Mijjinga anakuwa wa kwanza kujibu, “Nadhani kama alivyobainisha mtaalamu Mgosi, tatizo ni la makundi haya kuchezewa kiakili kwa kupewa fursa za kufanya upuuzi badala ya mambo ya maana kama alivyoyaorodhesha kitaalam Mgosi.”
Mpemba aliyekuwa ameshika tama muda mrefu anachangia, “Yakhe mmemfumbua macho wallahi. Kumbe hawa waungwanaa watutumia ili tuangamie baadaye! Naelewa sasa ni kwanini wakiambwa waache kukopa na kutanua hawasikii wala kujali.”
Mipawa ambaye alikuwa naye hajasema kitu anaamua kula mic, “Kumbe hapa lazima tufanye mapinduzi ya kifikra. Lazima tuanzishe utamaduni mpya kwa kuanza kuangalia mambo kwa jicho la uasi na ukali badala ya kuwaamini wapuuzi wachache waliotuangusha. Hapa lazima kifanyike kitu haraka kuokoa kaya yetu ili kupambana na huu upuuzi wa kugeuzwa vikaragosi.”
Kabla ya Mipawa kuendelea Mgosi anauma mic na kusema, “Tinahitaji kutafuta vipaji vya akili na kufikiri ili kuokoa kaya yetu toka kwenye mikono michafu ya majambazi na wabangaizaji. Hapa azima vipaji vitakavyotafutwa viwe si vya kuhoji tu bali kutenda mambo kwa kuangaia mbai na si usawa wa tumbo kama iivyo sasa.”
Kapende naye anadakia kwa vile hajasema kutokana na kuwa akiandika ujumbe kwenye simu yake, “Hapa lazima tukubaliane kuwa Mgosi ametangaza mapinduzi na vita dhidi ya hawa nuda wala watu. Jeshi la kufanya haya mapinduzi na makamanda wa kuliongoza tupo. Kwanini tushindwe huku tukiendelea kulalamikia wahuni waliotajwa hapo juu wakati tuna kila sababu na uwezo wa kuwapiga chini? Lazima tutangaze mapinduzi leo.”
Kabla ya kuendelea kila mmoja anampigia makofi kutokana na jazba, ngoa na usongo anavyoonyesha.
Sofi ambaye alikuwa amenuna muda wote anaamua kula mic. “Hakuna cha mapinduzi wala nini bali uchochezi mtupu. Nadhani nyinyi mmechoka na amani.”
Mijjinga hamkawizi, “Amani ya kuliwa yamfaa kuku si mwanadamu dada yangu.”
Kanji anachomekea haraka haraka, “Sasa nyinyi taka shida kwa dugu na toto yenu. Kama nafanya pinduzi mimi kwenda Bombay au hamia Kenya hadi yote tulia.”
Mzee Maneno anamjibu, “Ni kweli Kanji. Kwani una uchungu gani na hapa wakati hapajawahi kuwa kwenu isipokuwa kwenye kuchuma?”
Kijiwe kikiwa kinaanza kunoga tuliona gari la Po Chagonjwa tukaamua tumkabili kumpa displine aache unazi wa kipuuzi.
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 24, 2014.

No comments: