Tuesday, 16 September 2014

Sitta na UKAWA nani msanii tena anayetapatapa?


          Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba lililopoteza maana, Samuel Sitta anaonekana kuchanganyikiwa, kuguswa na kuweweseka. Pia ni mtu asiyeishiwa vituko ambavyo mara nyingi humuumbua na kufichua Sitta wa kweli ambaye mara nyingi hujificha kwenye madaraka. Hivi karibuni alidhihirisha kutokuwa na mawasiliano na uhalisia pale alipokaririwa akiwaita Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wasanii ambayo maana yake halisi kwa siasa za Tanzania ni ubabaishaji. Sitta alisema, “Kwa hiyo natoa ushauri tu kwamba, mwakani watakaposhindwa vibaya wakati wa uchaguzi kutokana na tabia zao hizo, basi warejee katika fani ya uigizaji ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia.” Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu, nani msanii baina ya wawili hawa. Je Sitta amejuaje kuwa watashindwa au anafahamu mipango ya kuchakachua hata matokeo ya uchaguzi kama ilivyozoeleka kutekelezwa na chama chake? Je wenye matendo ya kuweza kushindwa baina ya UKAWA na akina Sitta ni nani hasa ikizingatiwa kuwa wameidhinisha kupotea pesa ya umma maskini ipatayo shilingi bilioni 200 ambazo zingepunguza adha ya umaskini waliomo watu wetu?
          Ili kutoa hukumu nzuri, tutajaribu kuonyesha wawili hawa kupitia mambo waliyofanya kwa taifa. Tuanze na Sitta. Akiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano alijipachika jina la mzee wa Viwango. Kwa muda alifanikiwa kuonyesha lau viwango hasa pale alipomsulubu waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyeachia ngazi baada ya kukumbwa na kashfa ya Richmond. Hata hivyo, ima Sitta alidhihirisha viwango au la inategemea unamtathmini vipi.
          Kwa kufanikiwa kuishikisha adabu serikali na chama chake kwa kumfukuza waziri mkuu, Sitta alijijengea umaarufu kabla ya kuubomoa. Tunasema alibomoa umaarufu wake pale mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk Harrison Mwakyembe, akijibishana na Lowassa aliyelalamika kuonewa, kusema kuwa kama wasingeficha baadhi ya mambo huenda serikali nzima ingeng’oka. Hapo ndipo wachambuzi wa mambo walianza kuhoji usafi na viwango vya Sitta.
Mungu hamfichi mnafiki. Punde tu baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiridhisha kuwa kada wake huyu hakuwakingia kifua, kiliamua kumtosa toka kwenye uspika. CCM walingoja amalize lau ngwe ya kwanza kabla ya kumchomoa Spika wa sasa Anna Makinda ambaye hupenda aitwe Anne ingawa sisi tuliokuwa wakati wa awamu ya kwanza Makinda akiwa madarakani alijulikana kama Anna. Hayo tuyaache.
          Makinda, pamoja na udhaifu wake, aliweza kupitishwa kwa kuhakikisha Sitta hagombei. Kwa lugha rahisi ni kwamba CCM waliamua kumuengua Sitta kama onyo kwa kichwa ngumu yake. Hivyo, kwa mara ya kwanza, Sitta alipata pigo ambalo hakulitarajia pamoja na kuficha baadhi ya mambo muhimu ambayo yangeing’oa serikali akidhani angeweza kuwaridhisha wote.
          Baada ya Sitta kupigwa teke toka kwenye uspika, alianza kuhaha huku tetesi zikitoka kuwa aliamuru kianzishwe Chama Cha Jamii (CCJ) kama ilivyodaiwa na mshirika wake mkuu Fredrick Mpendazoe baadaye. Sitta alijitahidi kujitenga na CCJ ingawa bado watanzania wanajua kuwa kweli alikuwa nyuma ya kuanzishwa kwa chama hiki ambacho alikisaliti pale alipopewa uwaziri lau kutuliza hasira na kupunguza nguvu ya makundi ndani ya CCM. Pamoja na kumpiga teke kwenye uspika, CCM hawakutaka Sitta aondoke na kudhoofisha chama. Hivyo, hivi karibuni, katika harakati ya kumwekea spidi gavana kwenye mbio za urais ambao ameishatangaza atagombea na kumtuliza, CCM walimruhusu agombee uenyekiti wa BMK ambao alipata.
          Bila kujua mtego na kitanzi alichokabidhiwa, Sitta alikaririwa akijitapa baada ya kutangazwa mshindi kuwa samaki alikuwa amerejeshwa majini asijue maji yenyewe ni ya moto na machafu kama inavyoanza kujidhihirisha baada ya rais Jakaya Kikwete kukubaliana na UKAWA kusitisha BMK.  Pamoja na Kikwete kunawa mikono akisema wazi asitwishwe zigo na lawama za kuhujumu Katiba Mpya, Sitta anaonekana kutoelewa somo na kama amelielewa anajifanya haelewi kwa kusimamia kitu kishichowezekana. Pamoja na makubaliano ya kusitisha BMK, Sitta ameshupaa na kuhakikisha inaendelea kinyume cha sheria huku ikipoteza muda na fedha za umma jambo ambalo baadaye litamuandaman Sitta.
          Katika kufanikisha hili, Sitta amepata maadui wa kudumu ambao ni UKAWA anaowapa majina ambayo mara nyingi kimepewa chama chake na bosi wake. Nani hajui kuwa watanzania wanafahamu fika Kikwete ambavyo amekuwa akiitwa bonge la msanii kutokana na kufanya mambo kinyume na anavyoyaahidi? Hata tunapoandika, wana CCM wengi walioaminishwa kuwa Kikwete angeingia kwenye vitabu vya historia kama rais aliyeandika Katiba Mpya akashindwa mwenywe, wanamuona msanii tu wa kawaida.
          Tuje kwa UKAWA. Hawa jamaa walipaza sauti na kusema kuwa CCM na serikali yake walipanga njama za kuhujumu rasimu ya Jaji Joseph Warioba, mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni (CRC). Mwanzoni umma haukuwaamini. Walipopaza sauti na kutoa ushahidi umma ulianza kushawishika na kuwaamini kiasi cha CCM kutishika na kuanza kuwaandama kwa kutumia akina Sitta isifanikiwe. Baada ya kuona hakieleweki, UKAWA walijitoa kwenye Bunge jambo ambalo Sitta alilikejeli asijue ataramba matapishi yake hasa pale baada ya bosi wake kukubali kukutana na UKAWA na kuja na sitisho la BMK linaloendelea kuleta utata hasa pale wapambe kama Sitta kushupaa kuwa lazima waendelee kukamilisha kitu kilichokwisha kataliwa.  Nafasi haitoshi. Tungeweza kudurusu mengi juu ya wawili hawa ili wasomaji watoe hukumu ya haki. Je hapa msanii ni nani kati ya Sitta na UKAWA? Sitta, Kikwete, CCM hata watanzania wanajua fika nani wasanii ambao wamebanwa kwenye kona kiasi cha kuramba matapishi yao na kutoa matamko yanayokinzana. Anachofanya Sitta ni kuzidi kuwapa shime UKAWA waende kwa wananchi kupinga kujwa kwa shilingi bilioni 200. Je ukweli utakapofichuka Sitta ataweka wapi sura yake katika umri huu anapopaswa kujijengea heshima lakini akaibomoa kwa kushikilia vitu visivyowezekana?
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 17, 2014.

No comments: