Saturday, 6 September 2014

Mlevi kulishtaki BMK, ataka katiba mpya yenye mapya

Japo wanasheria wamesema hakuna jinsi ya kulishtaki au kulisitisha Bunge Maalum la Kitabu (BMK), wanaoliheshimu sana huliita Bonge la Mazingaombwe na Kuhomolea, mie nitalishtaki ili kuleta suluhu na kuonyesha njia.
Tatizo la watu wengi ni kudhani kuwa mahakama lazima liwe jengo. Kwangu mimi mahakama ni taasisi yoyote inayoweza kutatua migogoro.Hakuna mahakama kuu kayani kama walevi wenyewe.
Ukiona kesi imeshindikana kwenye mijengo, mahakama we wapelekee walevi.Watatoa hukumu tena isiyopendelea wala kugharimu njuluku kibao. Kwenye mahakama ya walevi ambayo ni tukufu kuliko zote, hakuna rushwa wala ucheleweshaji wala misongamano ya kesi.
Wanaingia mitaani siku moja kila kitu kinakuwa shwari, au vipi? Kwa vile siku hizi naona kama nimesahaulika kwenye medani za kisiasa na ujiko, lazima nitafute gea ya kurejea ugani.
Hata hivyo, lazima nirejee kwa kufanya kweli kwa ajili ya walevi badala ya kusaka umaarufu uchwara.Mchovu Saidia Kubenua upo? Vipi lile gazeti lako la udaku liliishia wapi? Nimesoma vitu vyako ukitaka kun-time huu ujiko wa bure.
Imekuwaje upate mshipa wa kushitaki BMK ushindwe kuwashitaki walioua chata lako?Je! yawezekana kuwa na uchungu na wanakaya kabla ya kuwa na uchungu kwako binafsi na familia yako?  Hayo tuyaache. Hata wale wanaobuna laki tatu kwa siku wanajidai wanatetea walevi wakati ukweli ni kwamba wanawauza kukidhi njaa ya matumbo yao.
Watawezaje kuwakombo walevi kwa kuwabambikia katiba ya mtibuo isiyoangalia maslahi yao?Japo mlevi si mwanachama wa chama chochote, lazima awapongeze jamaa wa Umoja wa Katiba ya Walevi (Ukawa) kwa kugomea mizengwe japo wameogopa kuingia mitaani ili kieleweke.  Hata hivyo hakuna sehemu wanakoniacha hoi kama kujiruhusu kutumiwa.
Kukutana na jamaa wasio na uwezo wa kuelewa wala kubadilika ni kupoteza muda.Mtastuka na kukumbuka blanketi kumekucha muanze kulia.Njoo mjiunge na walevi muingie mitaani na kuondoa kadhia.
Kwa vile najua wazi kuwa kushitaki BMK mahakamani hakuna nguvu wala matokeo mazuri, nitashitaki kwa walevi ili wachague la kufanya kuhakikisha uchache wao uibiwe na kutumika kuwahongea wasaka tonge watakaopitisha kila aina ya upuuzi bila kujali maslahi na mustakabali wa walevi.
Walevi ndiyo watakaoamua kama tuingie viwanja na kuhakikisha kaya haitawaliki wala kuibiwa kama BMK inavyofanya kwa kulipana laki nt’atu kwa kutofanya lolote kwa siku.
Haiwezekani kaya kapuku tena inayoishi kwa kuombaomba na kukopakopa iwe na jeuri ya kulipa madafu laki tatu kwa siku kwa walaji wasiofanya lolote zaidi ya kile mzee mmoja aliita utoto.Mie nasema: Huu si utoto bali wizi wa kitoto.
Kwa hiyo, ifahamike wazi, hata hawa wanaokimbilia mahakamani kutafuta ujiko uchwara badala ya kuwekeza kwenye kama mbaya mbaya, wanafanya utoto.
Kwani wanajua fika, kisheria, BMK haishitakiwi kutokana na kuundwa kilevi kwa kuangalia na kuamini kuwa upande mmoja ungeacha utoto na uridhie na kujadili rasimu ya Waryuba.
Unakuwa utoto zaidi hasa pale wahusika wanapokuwa ni wale wale waliowahi kukwamishwa na utawala huu kidhabu wakashindwa kushitaki na kujikwamua.Iweje sasa hao hao walioshindwa kujitetea binafsi eti wawe na mshipa wa kutetea umma kwa kukwepa kuuhamasisha kuondoa kadhia ya kuibiwa na kuburuzwa?
Kwa kujua jinsi wasanii wanavyoweza kuuvuruga na kuutumia mchakato kutafuta ujiko, fedha, vyeo na upuuzi mwingine, Mlevi naamua kuishitaki BMK kwa kufuata utaratibu wa kuhakikisha anahamasisha walevi ili waandamane na kuhakikisha inafungwa kama siyo kuwafunga wale wote wanaoendekeza kuiba njuluku za walevi tena makapuku.
Kama ningetaka ujiko kama wasaka ujiko wanaokimbilia mahakamani wakijua hakuna kitu, kwa vile mimi ni mwanasheria, basi ningekwenda huko na kujiwakilisha mwenyewe na kupata huo ujiko uchwara.
Hata hivyo, mimi sitaki wala sishtaki kutafuta ujiko zaidi ya katiba mpya ya walevi.Nataka katiba mpya iliyo mpya na yenye mapya.
Katiba itakayokomesha wizi wa mali za walevi na ulafi wa ngurumbili wenye madaraka kula kwa mikono na miguu bila kunawa tena watakavyo.
Nataka katiba mpya iliyotungwa na kuandikwa na walevi wenyewe bila mizengwe wala shinikizo wala wizi wa njuluku zao kama ilivyo sasa ambapo genge moja limeteka mchakato mzima.
Kwa vile nawajua wanaokwamisha kila kitu, nina mpango wa kumshitaki Sammmy Sixxx kwanza kwa kukubali kutumiwa na Njaa Kaya kuhujumu mchakato.
Huyu ndiye anapaswa kuadhibiwa kwanza kabla ya yoyote kwa vile ndiye aliyejirahisi na kujiruhusu kutumika kuibia na kuhujumu walevi.  Ajabu nasikia eti anausaka urahisi asijue amepewa kitanzi ajimalize!  Kama ameshindwa kuendesha BMK anaweza kweli kuendesha kaya huyu mdugu?
Amechemsha. Hafai kuwa hata mjumbe wa nyumba kumi sawa na aliyemtumia ambaye amegeuka kuwa ajali na balaa la kihistoria kwa kaya ya walevi, bahati yake hausaki ulaji tena angekoma na kukomaa.
Wiki ijayo naweza kuanza kufunga ili kupata maoni ya kumpata mtu atakayewekeza kwenye ikulu baada ya walevi kuibinafsisha.Tuonane wiki ijayo. Leo namkumbuka mshirika wangu Coltide aliyerejesha namba wiki jana.
  CHANZO: NIPASHE 

No comments: