Wednesday, 26 November 2014

IPTL: Nani awajibishwe kati ya Pinda na Kikwete?


Mengi yameishaandikwa na kusemwa kuhusiana na kashfa ya wizi wa fedha za umma toka Benki Kuu (BoT) chini ya mfuko wa Escrow. Kashfa hii licha ya kunakera, inachefua, ni aghali, imegharimu taifa heshima, uaminifu, uwajibikaji, muda na fedha hata maendeleo. Imetuacha uchi na wa hovyo ukiachia mbali umaskini. Hivyo, katika kuishughulikia, wenye dhamana ya kufanya hivyo waende mbali kwa kuangalia historia nzima ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na jinsi ilivyoingizwa nchini kwa makusudi mazima ya kuliibia na kulihujumu taifa. Ifahamike, kashfa hii ni zaidi ya Escrow na watuhumiwa ambao wengi wamekamiwa kudondoshwa.
Kashfa ya Escrow, licha ya kufichua uchafu, uroho, ufisi, ufisadi, upogo, upofu, roho mbaya na jinai ya baadhi ya wakubwa zetu, imefichua utegemezi na uhovyo wetu na mfumo fisadi na zandiki. Licha ya kuhujumu na kudhalilisha taifa, kashfa hii, imelifedhesha hasa ikizingatiwa, kuna njama za kuizima wakitaka kutumia majaji, tuseme majanki, yaliyoteuliwa na wanaopaswa kubebeshwa zigo zima. Hapa ndipo uhovyo wetu kama taifa unagundulika. Kitendo hiki cha kutaka kuiua kashfa ya Escrow kimefanya wafadhili watudharau na kuamua kuingilia kati baada ya kuona hatufanyi mambo sawa sawa. Hii ni aibu na kilio kwa taifa. Je tufanyeje zaidi ya kujifunza kubadilika na kufanya mambo kama watu wenye akili timamu na uzalendo? Changamoto sasa iko mikononi mwa bunge letu tukufu ambalo si mara ya kwanza kukumbana na mtihani kama huu. Tunawaamini na kuwategemea wabunge wetu bila kujali itikadi, vyama au mafungamano. Taifa ni zaidi ya vyama na itikadi. Mtashinda tu mkidhamiria.
Wakati vichwa vikiuma juu ya namna ya kushughulikia kashfa hii, tunapaswa kujua chanzo cha sakata zima. Kwa mujibu wa historia ya kampuni nyonyaji na kidhabi ya IPTL, kampuni hii ilipata tenda ya kuzalisha umeme kwa taifa kwenye mazingira ya kutatanisha chini ya utawala wa Ali Hassan Mwinyi mwaka 1994 wakati rais wa sasa Jakaya Kikwete akiwa waziri wa Maji, Nishati na Madini kabla ya kuhamishiwa wizara ya fedha mwaka huo huo. Hivyo, unapoongelea IPTL huwezi kumaliza bila kuwataja Mwinyi na Kikwete. Mwingine aliyesaidia sana kuingizwa kwa IPTL nchini ni katibu mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) marehemu Horace Kolimba.
Hivyo, kushughulikia kashfa ya Escrow bila kuwagusa Mwinyi, Kikwete na wengine waliohusika kwa kiwango kikubwa kuhalalisha wizi kwa taifa jambo ambalo licha ya kusababisha ulanguzi na mgao wa umeme, sasa linatumika kuliibia taifa kijingajinga ni kupoteza muda na kukubali kafara.
Inashangaza kuona tunaposhughulikia wizi huu wa mabilioni kwa taifa maskini, anayeonekana kujua undani wa IPTL na mwenye serikali yake, yaani Kikwete, haguswi wala kuhusishwa. Wengi, kwa sasa, wamehanikiza kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anaweza “kwenda na maji” kama Edward Lowassa aliyeenguliwa na kashfa nyingine kama hii ya Richmond. Je ni halali kuongelea au kushughulikia IPTL bila kumshughulikia walioiingiza na wenye kuonekana kujua mengi kuliko Pinda? Je hao watuhumiwa waliteuliwa na nani na walifanya kazi kwa niaba ya nani zaidi ya rais?
Wapo wanaoona kama historia itarejea na tabia ya kujirudia. Kama wenye dhamana ya kushughulikia kashfa hii, yaani wabunge, hawatakuwa makini, kuna uwezekano kilichotokea Februari 7, 2008 kujirudia ndani ya muda mfupi. Na ikitokea hivyo, tutakuwa tumepoteza fursa muhimu ya kutatua tatizo.Na kama ikitokea hivi, tutakuwa tumeshughulikia kafara badala ya mwenye dhambi anayetoa hiyo kafara. Tutakuwa tumekata matawi na kuacha mzizi wa tatizo ambao ni Kikwete, CCM na serikali nzima. Hivyo, kumaliza kadhia hii ni kushughulikia kiini kizima cha gonjwa badala ya matokeo.
 Kwa wanaokumbuka malalamiko ya Lowassa kuwa rais Jakaya Kikwete alijua kila kitu kuhusiana na Richmond, hawana shaka kuwa Waziri Mkuu wa sasa Mizengo Pinda, kama atatolewa kafara na bunge likaingia mkenge na kukubali, atarudia maneno yale yale. Je tutakuwa tumetatua tatizo au kumuacha wahusika wakuu kuendelee kucheza ngoma ile ile, kulihujumu taifa na kufanya kile waingereza huita, to get away with murder?
Tusingetegemea wabunge wapoteze muda kushughulikia vijidagaa na makuwadi wakati wenye mradi mzima wapo wakiendelea kufikiria jinsi ya kutenda madudu mengine. Hivi ni woga au ujinga? Bunge linaogopa nini kufumua mfumo mzima hasa baada ya kumtaka rais ajitetee hasa ikizingatiwa kuwa jinai hii imetendeka chini ya uangalizi wake ukiachia mbali kuwa sehemu ya historia ya tatizo? Muda wenyewe uliobaki kwenda kwa wananchi ni mdogo tu.
 Wakati wabunge wakitafakari haya wanapaswa kujiuliza swali moja: Je nchi hii ni mali ya nani zaidi ya watanzania bila kujali ukubwa wa nyadhifa zao? Je nani yuko juu ya sheria akaruhusiwa kutenda jinai atakavyo asishughulikiwe? Je imekuwaje serikali izembee na kukaa kimya hadi wafadhili waingilie kati kwa kuondoa fedha zao zipatazo shilingi zaidi ya trilioni moja wanazochangia kwenye bajeti ya taifa letu ombaomba na tegemezi lakini bado likawa na mshipa wa kuvumilia ujambazi kama huu wa Escrow na jinai ambayo imefanyika kwa muongo mzima ya IPTL na ulanguzi na mgao wa umeme ukiachia mbali uchafuzi wa mazingira tokana na kutumia teknolojia ya zamani kuzalisha nishati? Wakati haya yakiendelea, tunaambiwa deni la taifa linaumka bila maelezo ya msingi na bado tuna mshipa wa kuwavumilia wanaotenda jinai hii wakiongezea na ya Escrow na nyingine nyingi! Basi tu viumbe wa hovyo na wa ajabu kidogo.
          Tumalizie kwa kuwataka wabunge waende mbali bila kuangalia maslahi binafsi au kuogopa cheo cha mtu ambacho kimsingi ni dhamana toka kwa watanzania hawa hawa wanaohujumiwa na kufanyiwa ujambazi mchana kweupe.
Chanzo: Tanzania Daima leo.

2 comments:

Anonymous said...

Wote wawili na wengine ili kuondoa status quo!

NN Mhango said...

Anon usemayo kweli. Tufyeke shamba zima la mibuyu badala ya kukubali kafara ya waziri kuu wakati mhusika mkuu ni rais na wengine.