Friday, 14 November 2014

Zinjanthropus Makamba, dijitali na ndoto za ufalme


 
Katibu mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuf Makamba alitoa mpya baada ya kuwakandia watu wanaotaka kugombea urais kwa kumpigia debe mwanae asijue anajikandia pia. Makamba alikaririwa akisema, “Makamba ni msomi, kijana na Tanzania ya sasa inahitaji rais wa kisasa atakayekwenda na kasi ya dunia na Junuary ni kizazi cha digitali, siyo kizazi cha BBC yaani Born Before Computer ambao hawana uwezo wa kukabiliana na kasi ya dunia ya leo.” Je hawezi kuwa Born and Bred Corruptly?   
Kwa wanaojua uzuri na ubora wa elimu, wanashangaa usomi wa January ambaye historia yake inaonyesha kuwa aliingia kidato cha tano kwa mizengwe ukiachia mbali kuwa shahada yake ya MSc in Conflict Analysis and Resolution si kubwa kiasi hicho kwa kizazi hiki cha kisomi. Je angekuwa na PhD kama mbili au tatu au masters kama mbili au tatu ingekuwaje? Je hiyo elimu yake kubwa alishaifanyia nini iwapo amefika hapo alipo kwa kubebwa na jina la baba yake na si elimu yake? Mtu asiyeweza kujitengeneza hadi atumie mgongo wa baba hawezi kuwa msomi kitu. Nani anataka rais atakeamriwa na baba yake aliyemtengeneza? Japo ni haki ya Makamba kugombea cheo chochote, afanye hivyo kwa sifa zinazoingia kichwani na si kubebwa na jina kubwa la baba yake. Je Makamba ameifanyia nini nchi hadi afae kuwa rais? 
Je January kweli ni msomi wa kidijitali kama anavyodai baba yake au ni kamba za kawaida?  January, sawa na watu wa umri wake wa kitanzania, alianza kuitumia hiyo kompyuta anayosifiwa alipokwenda kusoma Marekani akiwa tayari ni mtu mzima wa zaidi ya miaka 18. Isitoshe, kwa mtu mwenye umri zaidi ya miaka 20 aliyezaliwa na kukulia Afrika hawezi kujiita mtu wa dijitali sehemu ambako kompyuta bado ni kitu cha watu wachache tena wateule kwa nchi maskini yenye mipango ya hovyo kama hiyo. Leo bado kuna watu wanazaliwa hadi wanakufa bila kuigusa hiyo kompyuta. Watu hawana maji wala umeme unawaletea nyimbo na tambo za kompyuta! Je kwa vile Makamba aliyetumia nafasi na fedha za wananchi walalahoi kusomesha mtoto wake nje sasa anawaringishia asijue bila hao anaowaona ni analogue, huyo Makamba na huyo mtoto wake wasingefika hapa wanapojivuna na kukufuru? Watanzania hawataki geek (Gwiji la kompyuta) bali mtu anayeweza kufanana nao na kujua matatizo yao na anayetokana nao. Tunao watanzania wa namna hii tena wengi wako kwenye upinzani. Wapo akina Dk Wilbrod Slaa, profesa Ibrahim Lipumba na wengine wenye elimu zao za haja na bado hawawakejeli watanzania. Huu ndiyo usomi. Si ulimbukeni tena unaofanywa na watu wanaoonekana kuwa wakubwa kiumri lakini wakatenda kitoto. 
Usomi wa January uko wapi kama anategemea kubebwa na baba yake asiyejua hata anachosema hasa ikizingatiwa kuwa anasifika kwa kujikanganya kama anavyoonekana mara nyingi akibeba Biblia badala ya msahafu wake. Inakuwaje cha wengine kiwe bora lakini chako ukifiche kusiwe na tatizo? Hata hivyo, leo hii si hoja japo kinachotaka kuonyeshwa hapa ni tabia ya Makamba kujikanganya na kukanganya wengine. Sikutegemea Makamba aongelee mambo ya kidijitali hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni BLBT yaani Born Long Before Typewrite. Ongelee sifa zinazotakiwa na watanzania kama vile kupambana na ufisadi na ufisi vilivyotamalaki.  Hata hivyo, simlaumu tokana na kuwa na kiwango kidogo cha elimu na welewa kiasi cha mawazo yake mgando kuyaona ni hekima wakati siyo. 
Hivi kila kigogo akibeba mwanae hao wasio na wazazi vigogo watakuwa wageni wa nani? Kama wote wangetumia vigezo vya kiroho na kibinafsi kama anavyotumia Makamba, je yeye angekuwa hapo? Kama ni usomi mbona Makamba alifika alikofika bila usomi? Kama si mfumo wa kujuana na kufadhiliana Makamba angekuwa hapo alipo akikufuru?  Kama si mfumo wa kulindana usioangalia mchango wa mtu, watu kama Makamba kweli wangeweza kufika hata nusu ya hapo walipo? Je wote wangekuja na lugha za nyodo kama anazokuja nazo Makamba baada ya kutumia fursa ya umma kumsomesha mwanae yeye angekuwa wapi kama si kuishia kuwa mcheza ngoma za kienyeji? Na kama ni usomi mbona kuwa vijana wenye elimu kubwa na nzuri kuliko ya huyo January? 
Hatuwezi kuendekeza majina makubwa na kurithishana ulaji kumpata rais wa nchi. Hivi baba wa taifa mwl. Julius Nyerere angekuwa mroho wa madaraka na kipofu namna hii Makamba na January wake wangekuwa hapo wakimwaga makufuru wanayofanya wakiutaka urais ambao, bila shaka, ungekuwa mikononi mwa watoto wa Nyerere? Hatutaki ufalme wa akina Makamba na wote wenye majina makubwa wanaotaka kutupenyezea watoto wao warithi madaraka yao. Mwalimu aliacha mfano unaong’ara. Hakuwahi kuruhusu mkewe wala mwanae kugombea uongozi kwenye chama au serikali yake. Alijua kutakuwa na mgongano wa maslahi jambo ambalo linaondoa dhana nzima ya uongozi bora na utawala wa sheria. Kimsingi, wanachotetea akina Makamba si uongozi bali uroho wa madaraka na upogo tu. Wanasahau hata historia zao zenye kutia kila shaka kuwa wasingeshikwa mikono na kupendelea wasingefika hapo walipo wanapotambia elimu walizopata kwa kuwatumia wengine. Ni kituko Zinjathropus Yusuf Makamba anapoongelea dijitali wakati kidijitali alishakufa miaka mingi iliyopita!
Chanzo: Dira ya Mtanzania

3 comments:

Anonymous said...

Katika wasomi naye msomi huyu
Kafanya nini kikubwa kwa watanzania kama si kubebwa na baba yake ambaye inashangaza kupata madaraka licha ya kumpa mimba mtoto wa shule ya msingi akiwa mwalimu wa shule ya msingi
Inashangaza usalama wa taifa wanafanya nini Watu kupewa madaraka wakati Hawana maadili kwa jamii

Anonymous said...

Sidhani kama usomi(Ma-degree lukuki) unamahusiano ya moja kwa moja na sifa kiongozi bora. Ingekuwa hivyo basi Afriak leo(Tanzania) ingekuwa mbali sana.

Nachoelewa mimi kiongozi mzuri anatakiwa pia atoke familia bora kimaadili. Kimsingi tabia na uasili wa kiongozi unaanzia tangu makuzi. Ukitoka familia ovyo ovyo kitabia kama umalaya, chuki miongoni mwa wwanafamilia, visasi, lugha chafu uhuni, misingi ya rushwa na ukandamizaji itatakukuza katika misingi hiyo hiyo.

Hata baadae ikatokea ukwa kiongozi utafanya hayo hayo mambo yaliyokukuza sababu hautaona tofauti. Kuhusu taratibu za kiserikali kuchagua au kupendekeza kiongozi nadhani huo ni mlolongo mrefu sana kwa taasisi kuwa imara inatokana taratibu zote zilizotumika hata kupata hao wafanyakazi iwapo ilitokana na sifa au kujuana. Basi tegemea pia utendaji wa kazi katika kiwango duni pia.

NN Mhango said...

Anon hapo juu mmemaliza kila kitu. Sitaki niongeze na kuvuruga mawazo yenu mwanana na yenye siha. Nasahukuruni sana.