Friday, 21 November 2014

Mlevi afanya utafiti kuhusu uchaguzi ujao

Baada ya kuona wengine wakija na matokeo ya utafiti wao ambao wapinzani wao wameyaita mazingaombwe waliyopachika jina la utafiti wakati ni utafutaji mlo toka kwa mafisadi wanaotaka kugombea urais kayani, Mlevi ameamua kuja na utafiti wa kisayansi bila kujali kama ataitwa kihiyo anayejidai msomi. Wala sitajali kuitwa mchumia tumbo ingawa kweli kuna wachumia tumbo wanaoweza kutumia utafiti kusaka njuluku.
Hivyo, ufuatao ni utafiti uliofanywa na Mlevi usiolenga kusaka mlo wala kumpromoti yeyote. Kwa vile Mlevi ana shahada ya uzamivu Takwimu (PhD in Statics) aliyoipata kwenye chuo cha Hazard, huko kwa Joji Kichaka ameamua kuja na namna bora na ya kisayansi ya kufanya utafiti bila kubeba ngurumbili wala fisadi yeyote.
TWENDE KAZINI
Kupima kiwango cha uungwaji mkono kwa baadhi ya vyama vya siasa kayani hasa kulingana na usafi au uchafu na uwezo wao kuikwamua kaya toka kwenye mikono ya mafisi na mafisadi wanaokula kwa miguu na mikono bila kunawa huku wakipasiana.
Katika utafiti huu tulitafiti vyama kama taasisi zinazotoa wagombea badala ya watu binafsi. Maana, wahenga wanasema akili zenye rutuba hujadili masuala wakati zile zenye utapiamlo hujadili watu.
ZANA ZA UTAFITI
Yalitumika mahojiano yasiyo rasmi kwa njia ya simu za kiganjani ambapo waliopiga simu walikuwa na hiari ya kushiriki au kutoshiriki hasa baada ya kuambiwa haki zao kitafiti na kimaadili na si kimadili kama wale ambao wameficha hata waliogharimia utafutaji ulaji wao.
Mantiki ya utafiti ilikuwa ni kuangalia ni chama gani kingeweza kuchaguliwa kama uchaguzi ungefanyika sasa ili kuweza kuwajuza walevi anayefaa au wanaoafaa kuchaguliwa kwenye uchaguzi ujao.
HISTORIA YA KAYA NA UTAMADUNI
Tokana na kukithiri kwa uchakachuaji,wizi wa kura na hila mbali mbali za kutaka kuwapitisha mafisadi wagombee, nimeamua kufanya utafiti wa kisomi utakaowawezesha walevi kukataa kubambikiwa mafisadi wala kuibiwa kura  kwenye uchaguzi ujao. Hivyo, utafiti huu si ule utafutaji mlo toka kwa yeyote awe safi au fisadi. Ni utafiti wa kisomi na kisayansi kweli kweli.
KANUNI YA UTAFITI
Kuchanganua takwimu kuonyesha ukubwa wa tatizo la kuchakachua na kuiba kura ni mkubwa kayani ambapo mamlaka zinazosimamia uchaguzi ni zile zilitoteuliwa na wezi wa kura wenyewe huku ndata wakitumia kubeba chama twawala ili kiendelee kuwala walevi.
SAMPLI
Katika utafiti huu tumetumia aina ya mahojiano yajulikanyo kitaalamu kama snowball kwa kuhoji walevi 100 wanaume 50 wanawake 50 ambao walikuwa wa umri kati ya miaka 18 hadi 70 ambapo 70% walikuwa ni umri kati ya miaka 18-50 na 30% wa umri kati ya miaka 51 hadi 70.
Waliohojiwa walikuwa na kiwango cha elimu kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu ambapo 52% walikuwa na elimu ya kati ya shule ya msingi na sekondari wakati 30% ni kiwango cha High school hadi Diploma na 10% walikuwa na shahada ya kwanza na waliobaki yaani 8% walikuwa na shahada ya uzamili hadi uzamivu.
Utafiti umefanyika kwa miezi sita mfululizo ukihusisha mikoa yote ya kaya ya walevi.Uchambuzi wa takwimu Baada ya kufanya utafiti, tulichambua na kuainisha takwimu zilizoandikwa na zile zilizorekodiwa na kufanya mlinganisho na kuja matokeo ambayo nadhani kila mmoja analidhika nayo.
MASWALI YALIYOULIZWA
Kipaumbele cha uchaguzi ujao kiwe kurejesha rasmu ya katiba mpyai? Ndiyo au Hapana Vyama vyenye kashfa kubwa kama vile HEPA, Screw boozers, Richmonduli unadhani vizuiwe kushiriki uchaguzi? Ndiyo au hapana.
Kushindwa kushughulikia mafisadi hasa walioficha njuluku nje kutaangusha wale waliokuwa madarakani? Ndiyo au Hapana.Katika swali la kwanza waliojibu Ndiyo walikuwa watu 79 sawa na asilimia 79 ikilinganisha nwa waliosema hapana ambao walikuwa 21 sawa na asilimia 21.  Katika swali la pili waliojibu Ndiyo ni asilimia tisa ikilinganishwa na 10 waliojibu hapana.
Na katika swali la mwisho waliojibu ndiyo ni 95 ikilinganishwa na asilimia tano ambao bila shaka ni mafisi mafisadi au watu au watoto wao.Kwa ujumla walioonyesha uwezekano wa kushindwa chama twawala ni asilimia 88 ikilinganishwa na 12 ambao nao wanaonyesha hima kuwa mafisadi wenyewe au watu wao.Katika utafiti huu hapakuwa na rushwa wala hongo wala hatukuwa na mtu wetu kama wale wengine.
Utafiti huu uligharimiwa na walevi ili kupata taarifa safi zisizo za kupika wala kununua au kulenga kuvutia mafisadi fulani wakate pochi kama wale.Kwa ufupi ni kwamba utafiti huu umefuta uongo na hila vinavyoweza kufichwa kwenye utafiti kiasi cha kutoa matokeo yasiyowezekana kiakili.
Muhimu ni kuelewa kuwa hatukununuliwa, kushawishiwa wala kusaidiwa na yeyote katika utafiti huu adhimu. Ifahamike wazi. Wapiga kura hasa walevi na wavuta bangi wanapanga kuwapatiliza vidhabi na mafisadi wanaodhani wanaweza kutuungiza mkenge mwingine kwa kufanikiwa kujipenyeza au kupenyeza watu wao kwenye ikulu.
Walevi wanaonyesha kupenda vyama vyenye ajenda ya kupambana na ufisadi huku vikiamuru rasimu ya jaji Joseph Warioba irejeshwe ugani ili mawazo ya wananchi yajadiliwe na kuandika katiba safi.
By the way, tumegundua kuwa hali ya mambo kama uchaguzi utafanyika leo ni tofauti na tafiti nyingine zilizotangulia ambazo hata hivyo hazikutaja jinsi zilivyofanyika na nani walizifadhili. Hivyo, tunawashauri walevi wote kuupa utafiti huu umuhimu na kipaumbele. Kwa vile umekidhi viwango vyote vya kitafiti na kitaaluma, uwazi na ukweli. Tunatoa onyo hili hasa ikizingatiwa kuwa siku hizi uganganjaa imegeuka enterprise kubwa ambapo majambazi na mafisadi hutumia utafiti kupenyeza hoja zao.
Tukipata fursa tutafanya utafiti kuhusiana na mabilionea wa kweli.
Dondoo: Huwezi kuwa mhishimiwa aliyeko mjengoni kulinda maslahi ya baba yako na jamii yenu au kuwa mwizi wa Kagodamn ukawa bilionea. Utakuwaje bilionea atokanaye na kuibia umma, kukwepa kodi, kupunja waajiri wako mishahara na kufanya biashara haramu?
Tukutune wiki ijayo kwa mambo mengine yajayo. Onyo, watu wa Uwanja wa Ndege tafadhali acha mchezo wa kuruhusu miunga na vipusa kupitishwa hapo. Pia punguzeni rushwa. Maana wengi ni matajiri wa kutupwa tokana na kuendekeza njaa na rushwa. 
CHANZO: NIPASHE 

No comments: