Thursday, 6 November 2014

Kuepuka rushwa Miss Tanzania iandaliwe na wanawake


 
Japo huwa si mpenzi wa michezo, leo nitadurusu mashindano ya kutafuta miss Tanzania ingawa kinadharia ni hivyo na kivitendo ni miss mzungu. Baada ya kumalizika kwa kinyang'anyiro cha kumtafuta miss Tanzania, mara nyingi kama si zote hufumka tuhuma mbali mbali kama vile upendeleo hata rushwa ya ngono. Wengi hufikia hitimisho kutokana na wanavyomuona aliyetwaa taji. Kuna hoja ya msingi katika hili. Maana, mara nyingi, ukilinganisha washindi na kile ulichotegemea unapata vitu viwili tofauti. Kuondoa hili, hasa la rushwa ya ngono, mashindano husika yangeandaliwa na kuratibiwa na wanawake wenyewe.
Si uzushi kuwa kila baada ya kutangazwa kwa mwakilishi na mwenye kushikilia taji la miss Tanzania ama kumekuwa madai ya rushwa hasa ya ngono, upendeleo hata miss kutofanana na anaowawakilisha.
Kwa anayejua vionjo vya kiafrika, atakubaliana nasi kuwa miss Tanzania inabidi afanane na watanzania kwa kila fani. Sikumbuki ni lini waafrika hasa wanaume waliwahi kupenda hata kushabikia mtu aliyekonda ukiachia mbali kasumba za ulimbukeni wa kuiga na kutawaliwa na wanaowatumia binti zetu kujaza mifuko yao.
Leo tutatoa changamoto kwa wanawake tukiwatake waandae mashindano yao badala ya kutegemea wanaume kiasi cha kutoa mwanya wa shutuma za rushwa ya ngono. Kuna umuhimu wa aina yake kwa wanawake kumiliki, kusimamia na kuendesha mashindano ya urembo.
Kwanza, kama ni vigezo vya urembo, wanawake wanavifahamu sana kuliko wanaume. Maana linapokuja suala la urembo ni nini, wanaume ni sawa na watazamaji wa mechi ya mpira wakati wanawake ni wachezaji. Kitanda usicholala huwezi kujua kunguni wake.
Twende mbele zaidi, wanawake mbali na kujua urembo ni nini, ushiriki na umilki wao wa mashindano haya, licha ya kuwa kwenye mikono safi na salama utaondoa malalamiko ya rushwa ya ngono. Na siyo malalamiko tu bali hata uwepo wa mdudu huyu ambaye tafitishi nyingi zimeonyesha kuwa yupo. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya mashirika mengi yanayojihusisha na kupambana na rushwa na kutetea maslahi ya wanawake.
Huwa tunajiuliza: Kama kutoa kazi tu kunakuwa kishawishi cha kuomba rushwa ya ngono, hali inakuwaje pale wahusika wanapokuwa ni vimwana moto wanaowania taji la urembo lenye kumuingizia mshindi mamilioni ya fedha ukiachia mbali kupata umaarufu? Japo hii haimaanishi kuthibitisha shutuma za kutembezwa ngono, tunataka kuonyesha jinsi kishawishi na uwezekano wa ngono kutembezwa ulivyo mkubwa hapa.
Kwa nchi ambayo imepata uhuru miaka nusu karne iliyopita, lazima kutakuwa na kada ya wanawake wenye uwezo kielimu kulhali wa kuweza kusimamia zoezi hili vyema. Leo tuna wanawake mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na idara mbali mbali, wamiliki wa makampuni yenye.
Leo tuna wanawake marubani, wandishi wa habari tena mahiri, madaktari tena bingwa, wanasheria,wanajeshi hata washauri wa kitaaluma (Consultants) ndani na nje ya nchi. Kwanini tushindwe kuwa na wanawake wenye kuweza kutuepusha na malalamiko, aibu na jinai hii inayowadhalilisha wanwake wote?
Tunao wanawake mamilionea waliofikia pale kihalali siyo kubebwa na waume zao au wenye madaraka wanaojulikana na wengine wengi ambao wanaweza kuratibu na kuendesha mashindano ya kumtafuta miss Tanzania. Kwanini hawa wasijitokeze kunusuru heshima ya mwanamke inayoendelea kumomonyolewa na matapeli na wafanyabiashara wahuni wachache? Nani hajasikia matukio ya kitapeli ya promoters matapeli wanaowatapeli mamiss? Tutenganishe mashindano ya miss Tanzania na uganga wa kienyeji na utapeli mwingine.
Hakuna haja ya kina mama kuendelea kupigania haki ndogo ndogo wakati heshima na utu wao vinazidi kutumiwa na kumomonyolewa. Imefikia mahali wasichana wenye heshima zao na stahiki wanaogopa kushiriki mashindano haya ambayo kutokana na kuzungukwa na tuhuma za vitendo vya rushwa yanaonekana kama ya kimalaya na uchafu mwingine.
Hakuna haja ya kuogopa kuukabili huu ukweli hata kama unauma. Pitisha kura ya maoni uone wananchi wa kawaida wanayachukuliaje haya mashindano ambayo kimsingi hulitangaza taifa letu kiasi fulani.
Mashindano ya umiss yangetungiwa sheria kuwa sharti la kwanza lazima mwenye kuyaendesha na kuyamilki awe ni mwanamke. Ndiyo. Kitendo cha wanaume kuendelea kuyatumia na kuyamiliki mashindano haya ni sawa na ukeketaji. Huu ni ukeketaji wa kiakili.
Ni mwendawazimu gani atawatuhumu warembo kutoa rushwa ya ngono iwapo wanaoyasimamia wangekuwa wanawake wenyewe? Kutokana na mashindano haya kuendelea kuwa mikononi mwa wanaume, licha ya matapeli wa kiume na wakware kuyavamia na kuyatumia, yataendelea kuandamwa na tuhuma za ngono na kuonekana kama chaka la umalaya.     Wananchi wengi wanayaponda sana mashindano ya urembo na kuyaona kama kichaka cha aibu na kutukuza mila za kigeni kwa kudhalilisha zetu. Wanawake wakishiriki kuyasimamia na kuyaendesha wana uwezo wa kulishughulikia hili kuliko wasaka ngawira wanaowatumia wanawake kutengeneza utajiri bila kutoa jasho.
Ingawa hili laweza kuchukuliwa kama ubaguzi, safu hii ilishangaa kuona msichana wa kihindi akishinda taji la urembo barani Afrika! Je hii ni kutokana na wafanyabiashara wa kihindi kuwa na nguvu juu ya mashindano haya?
Kwa mtu anayeijua jamii ya kihindi vizuri hasa nchini mwao, si rahisi mtu mweusi kuwa mwakilishi wa taifa hili linaloongoza kwa kuwa na unyonyaji na ubaguzi wa kimfumo. Maana nchini India kila mtu huishi kwenye caste yake.
Hivyo dawa ya ubaguzi kuna kipindi ni ubaguzi wenyewe. Watu wenye akili bila shaka watauliza ni kwanini jamii ya kihindi inakuwa karibu nasi kwenye ulaji tu ilhali kwenye mambo mengine inatutenga. Watu wengi wamekuwa wanafiki kuogopa kulisemea hili kana kwamba halipo.
Bahati mbaya hata serikali zetu zimekuwa zikilipuuzia ili zisionekana kama wabaguzi wakati ubaguzi uko wazi kuwa wahindi wamekuwa matajiri kutokana na kuwatumia watawala wetu wachafu na waroho wanaoishirikiana nao kutuibia. Rejea ujambazi wa rada hata kununua ndege ya rais.
Pia hili la mamiss kutaka kufanana na wazungu linaweza kushughulikiwa hasa ikizingatiwa ujinga na ulimbukeni wa watu wetu. Tungeshauri, kuwa kuna haja ya kuyafanyia mabadiliko. Maana nchi za ulaya kwa sasa zimeamua kuwasaidia warembo kwa kupiga marufuku wale waliokonda ambao kimsingi wanahatarisha afya zao.
Tunalitumbukiza hili la kujikondesha kutokana na kuona karibu washiriki hadi washindi wengi wa shindano hili wamekuwa ni mifupa mitupu huku ukweli ukiwekwa pembeni kuwa kwa mswahili mwafrika mwanamke mrembo ni pamoja na mwili uliokamili siyo mifupa tunayoshuhudia kwenye majukwaa yetu.
Hapa wahusika inabidi waweke nukta na kuanza kujiandaa kubadilika.

Tuhitimishe kwa kusisitiza kuwa kama mashindano ya urembo yataendelea kuwa mikononi mwa wanaume, rushwa ya ngono haitakwisha na isitoshe hata kubambikiziwa warembo wasiofanana nasi kutaongezeka maana kama siasa zetu mwenye dau kubwa ndiye atainunua haki.
Chanzo: Dira

2 comments:

Anonymous said...

Kugushi Tanzania kitu cha kawaida
Kama mawaziri wamegushi vyeti Na bado wapo kwenye uwaziri, na wanatujua hata rais wetu mwenye PhD Kila kona eti na u profesa
Mungu tubariki UKAWA ingine madarakani

NN Mhango said...

Anon usemayo ni kweli. Kughushi kumehalalishwa Tanzania. Nimefurahi kuona kuwa mashinikizo yetu yamemfanya binti Mtemvu aliteme taji kwa kuogopa kufichua mengi.