The Chant of Savant

Wednesday 5 November 2014

Wanakijiwe waukwaa uprofesa

BAADA ya udaktari na uprofesa kugawiwa kama njugu hasa kwa matepeli na wasaka sifa wanaotapeliana na kugeuzana mabunga, wana kijiwe kwa vile wana sifa kuliko wengi wa wanaopewa vitu hivi, nao wameamua kujipa uprofesa. Baada ya kusukuti na kukubaliana, uprofesa utagawiwa kama ifuatavyo:
Profesa Emeritus wamepewa Alhaj, Mtukufu, Luteni Kanali, ndugu, Mheshimiwa, Field Marshal Dk. Mpayukaji Msemahovyo na Dk. Msomi Mkata Tamaa. Full Profesa imekwanda kwa Dk. Mijjinga wa Shedi, Dk. Kapende wa na Dk. Mgosi Machungi.
Associate profesa ni Dk. Mpemba Ami, Dk. Maneno, Dk. Mchunguliaji na Dk. Mbwa Mwitu Dk. Mheshimiwa Bwege.Wakati Kanji na bi Sofi Lion aka Kanungaembe wamepewa vyeti vya ushiriki wa kijiwe.
Yote haya yameanza baada ya Mchunguliaji kuingia na kulianzisha akisema, “Wazee mmesikia uprofesa wa kugawiwa kama njugu?”
Kapende anajibu huku akibeua midomo, “Unaongelea huu utapeli wa mchana kwa wapenda sifa wanaochuuza watu wao kwa zawadi za kipuuzi siyo?”
Mijjinga hangoji Kapende aendelee. Anakula mic, “Mie nimesikia. Nangoja waramba makalio yake kwenye mitandao waanze kujikomba kwa kumuita jamaa yangu mchunga mbuzi profesa Njaa Kaya Kiwewe.”
“Pilipili usokula yakuhusu nini kama si wivu na umbea? Hata wakimuita mtume wewe yakuhusu nini? Mwenye wivu si ajinyonge? Mtake msitake mkuu ni Profesa hata mkimuita mchunga mbuzi hata mchuna ngozi. Halo halo!” Bi Sofi Lion aka Kunungaembe anaamua kuwapa vipande vyao wanaomkejeli muungu wake.
Msomi Mkata Tamaa kutaka kumkatisha tamaa Sofi anang’aka kwa umombo, “When professorship is offered to wank instead of wonk there is a problem.”
“Mie hili la waramba viatu wala halinipi taabu. Najiuliza hawa walotoa huu uprofea alopewa atatoa nini? Maana maisha ya kisasa kula na kulipa ati.” Mpemba anaamua kukamua mic.
Mbwa Mwitu anajibu haraka, “Vya kuwapa anavyo vingi. Wametoa vya ubongoni kwanini asitoe vya mwilini?”
“Mbwa mitu acha tusi hovyo. Hiyo ya mwili nini? Kwanini tukana vatu bure bwana?” Anachomekea Kanji huku akicheka.
Msomi anarejea, “Mie wapeane vyovyote wapeanavyo mradi viwe vyao hainihusu. Kasheshe ni pale tutakapoona hawa watoa upuuzi kama uprofesa kwa wachunga mbuzi na wauza karanga kuja hapa na kuanza kupewa upendeleo kwenye mambo ya biashara. Hapa patakuwa hapatoshi.”
Mgosi Machungi anatia timu huku akibwia kahawa yake, “Usemayo kwei. Mambo ya kuhongana upuuzi kama shahada suti au michango kwenye kampuni ya bi mkubwa yanapaswa kukomeshwa.”
Mzee Maneno anakwanyua mic, “Mtayakomeshaje wakati mmeruhusu katiba mpya kuchakachuliwa?”
Kapende anachomekea,“Nadhani kuchakachua katiba si jibu. Ndiyo maana kijiwe tulipanga kususia hii kiini macho tunayoambiwa eti ni kura ya kupitisha au kutopitisha katiba feki.”
Mheshimiwa Bwege anatia timu, “Uprofesa mwingine choo kweli kweli. Tangu lini mchunga mbuzi na muuza mananasi tena aliyeshirikiana na fisi kuwararua kondoo anaowachunga akapewa uprofesa?”
Msomi anaongezea,“Kila nikiwaambiwa kuwa shule si kitu ya kuchezea huwa mnadhani najipa ujiko. Angalia vihiyo wanavyouzimikia hadi wengine kuwa tayari hata kuwatoa sadaka watu wao ili waonekane wasomi hata kama ni vihiyo? Anabwia kahawa yake na kuendelea.“Ubaya ni kwamba imefikia mahali hata watu waliohujumu na kuzika elimu kwenye kaya zao wanapewa uprofesa. Hii haikubaliki.”
Mzee Kidevu ambaye siku nyingi hakuhudhuria kijiwe anatia timu, “Hebu tuwe wakweli. Unategemea nini kutoka China.  Huoni visimu vyao vinavyozimika. Nasikia hata vitoto vinavyozaliwa na dada zetu wanaozaa na wachina vinazimia hovyo hovyo kama vijisimu vya mchina.”
Mpemba anauliza, “Hivi huyo rais wa Uchina akija hapa aweza pewa ujinga kama huu akaukubali au wapewa hawa wanaodhaniwa hamnazo?”
Mgosi Machungi anapoka mic huku akicheka, “Umetikumbusha kisa cha juzi pale Kaiakoo nilipoona mchina akichoma mahindi. Eti huyu naye ni mwekezaji wakati ni mchukuaji na mganga njaa. Hivi mswahili anaweza kuuza mahindi china wakati wachina hawana ajira wasimnyotoe roho na walivyo wabaguzi!”
Mheshimiwa Bwege anaamua kurejea tena, “Washangaa wachina kufanya umachinga kama kuuza mahindi na kusukuma mikokoteni? Kwanini wasifanye hivo iwapo wachunga mbuzi wanakwenda kule na kufanywa wasomi hata kama utapeli? Hapa nadhani wahusika wanatapeliana. Huyu anampa mwenzie dhahabu feki na yule analipa kwa fedha feki. Ngoma droo. Tangulini uprofesa ukatolewa kama njugu?”
Mpemba ananyaka mic,“Yakhe naona kama uprofesa waanzagawiwa kama njugu basi nasi wana kijiwe tutambue usomi wetu kwa kuwa maprofesa tokana na nchango wetu kwenye kupambana na utwahuti kayani mwetu. Mnaonaje hili?”
Mgosi anapokea ngoma na kuweka kifuani na kusema,“Ami tinakubaiana nawe. Kama wachunga mbuzi wanapewa upoofesa kwanini sisi mapoofesa wa kwei tisiotambuika tikatambuika japo kidogo?”
“Unashangaa hili? Hukusikia juzi nchini Zimba za Mabwe ambapo bi mkubwa yaani mke wa jongwe Bob Mugabie alitunukiwa shahada ya uzamizi baada ya kufanyiwa mtihani na wengine wakati hata shahda ya kwanza hana? Unadhani kulala kitanda kimoja na bwana mkubwa mchezo? Wengine wanaondoka na NGO na wengine wanataka warithi hata urais!”
Kijiwe kikiwa kinanoga si msafara wa Prof mchunga goat ukapita. Acha tumzomee kwa kututia aibu kwa kuhongwa upuuzi mtupu. Muhimu muelewe kuwa tangia sasa wanakijiwe wote ni maprofesa isipokuwa wale vibaraka na vidhabi.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 5, 2014.

No comments: