The Chant of Savant

Saturday 1 November 2014

Mlevi ampongeza Kikwete kumuokoa

          Baada ya rais Jakaya Kikwete kueleza “ugumu” wa “kazi” ya urais japo urais si kazi kwa vile hakuna aliyeisomea, Mlevi ameamua kuachana na ndoto za kugombea urais kama alivyokuwa ameahidi hapo awali.
Kwanza, Mlvei hakupenda kugombea sema bi mkubwa ndiye aliyekuwa akimuandama na kumataka agombee ili awe first lady, aweze kuunda NGO ya kutengenezea mshiko, watoto wake nao waweze kupata ubunge hata ulaji kwenye biashara zao binafsi. Hapa ndipo utaona ugumu wa urais. Kuapishwa uapishwe wewe wafaidi wengine mgongoni mwako wakitanua kama marais wakati hawakuapishwa. Huu kweli si ugumu. Unawezaje kumwambia bi mkubwa wako aache kutanua wakati ukifanya hivyo naye anaamua kukugomea ustanue naye sehemu sehemu. Wanaojua yanayotolewa na kupokelewa bedroom wanajua ninachomaanisha. Ukifanya hivyo unakosa mlo wa usiku bure. Je tutumikie mlo wa usiku na kuwatelekeza walevi au tuamue moja? Hayo tuyaache.
Pia bi mkubwa alitaka akiwa first lady atumie urais wangu kuizunguka dunia akiandamana na mlevi na kuondoa tongo tongo yeye na mashoga zake. Kwa vile sasa rais mwenyewe amesema kuwa kazi yenyewe ni ngumu, sina haja ya kuendelea na dhamira yangu ya kugombea hata kama bi mkubwa mpenda matanuzi atanisonga vipi. Itabidi ima tuachane akaolewa na Wasaka urais au atulize boli tuishi na kuachana na ndoto za kutanua kwa kutumia mshiko wa walevi makapuku. Mwenzenu hata kama napiga sana mma na bangi sina roho mbaya kama hawa wanaowatumia walevi kumaliza ushamba na ulimbukeni wao. Ndiyo maana imekuwa rahisi kwangu kuachana na ndoto za urais.
Najua wengi wataona kama bangi na gongo vinasumbua. Ukweli ni kwamba urais si kazi rahisi japo si kazi bali cheo. Ungekuwa rahisi unadhani wengi wangeugombea huku wakipigana vikumbo kuusaka? Unadhani urais ungekuwa rahisi watu wangehonga waupate hata kwa kuibia walevi na mabenki yao? Unadhani urais ungekuwa kazi, tena rahisi, wengi wangenunua magazeti na waandishi nyemelezi na fisi kuwapigia debe tena kwa kuwapakazia na kuwachafua washindani wao? Au mmesahau ilivyokuwa mwaka 2005. Kama umesahau kawaulize akina Salva na Mihingus Rweyependekeza waliowachafua watu hadi wakaishia kupewa ulaji kwenye afisi ya dingi na ukuu wa wilakaya. Hayo tuyaache, kwani wanadhani walevi ni wasahaulifu hadi kuwafunga kamba kijinga jinga hivi? Urais ni rahisi, sorry, ni mgumu kama keki.
Urais ni kazi ngumu inayohitaji watu wasio na woga na wasiojali. Maana kuwatumia watu kwa faida yako na familia na marafiki inataka moyo. Nadhani ndiyo maana mijitu vihiyo kama Idd Amin, Joseph Mobutu, Sani Abacha na mingine haikupenda kuachia kazi ngumu kama hii inayohitaji wagumu na si watu wa kuchekacheka hovyo. Unadhani walevi wanafurahi wanaposhuhudia kwa mfano mkeo akiwa tajiri au mwanao mheshimiwa kwa vile wewe ni rais? Unadhani ni kazi ndogo kuendelea kujifanya kama husikii makelele ya walevi kutokana na dhuluma kama hii inayofanyika kwa jina lako?
Urais si kazi nyepesi bwana. We fikiria mtu unalindwa utadhani kuna mtu mwenye mpango wa kukuiba. Lakini usipolindwa unadhani wale unaokula njuluku zao watakupenda hasa ikizingatia kuwa kuupata lazima utoe ahadi za urongo na ukweli? Urais ni kazi rahisi hasa usawa huu ambapo kila mtu anajua ukiwa rais basi familia yako, marafiki zako hata waramba viatu wako wataukata ingawa umma utaumia tu.
Urais ni kazi ngumu inayohitaji kuweka walevi sawa kuwa unatawala kwa faida yao wakati ukweli ni kwamba unatawala kwa faida yako. Inahitaji roho ya mwendawazimu kuwa mfalme lakini ukawafunga kamba watu kuwa u mdemokrasia.
Kama alivyosema rais, kuwa anatamani kwenda kuchunga mbuzi na ng’ombe hata kuuza mananasi Msata. Mlevi sasa yuko anasukuti kuanza biashara ya kufunga kuku, mbuzi na ng’ombe hata kuuza manansi. Biashara ya bingi na gongo sasa itanisahau kwa muda kama kweli sitaruka ahadi yangu. Maana kusema ni rahisi kuliko kutenda. Hivyo siku nikikwama mkaniona jijini msianze kuulizia juu ya ahadi ya kufunga minyama wala kuuza mananasi. Hata kama ni kamba inabidi tuvumiliane.
Turejee kwenye urais. Ni kazi ngumu inayohitaji moyo. Maana ukiangalia watu wanavyouhenyekea lazima uwe mgumu. Na unahitaji roho ngumu zaidi baada ya kuupata na jinsi ya kuutumia kutengeneza ufalme na himaya za utajiri haraka sana bila kujali kuwa walevi ni makapuku au la. Nikikumbuka zama za mzee Mchonga alivyokuwa akigombea na kivuli na kuanzisha siasa za chama kimoja, naona ugumu wa urais. Urais ni mgumu hasa kwenye kaya ya madili ambapo kila mwenye kutaka dili lake lazima aje kwako au kwa watu wako ili kuwachuuza walevi.

Walevi wasiojua kinachoendelea kwenye moyo na kichwa cha rais wanamuona kama mtu anayefaidi wasijue kumbe naye ana yake. Unadhani ni kazi rahisi kuishi kwa kuwapa walevi matumaini yasiyokuwepo? Hapa bado walevi hawajaja na malalamiko kuhusiana na maamuzi yako kama vile kuwakingia kifua wauza miunga, walioghushi, majambazi, mafisadi na wengine wengi wanaowahujumu walevi kwa vile ni swahiba zako. Hali hii imenikumbusha sakata la Ditto Mzuzue alivyomnyotoa roho dereva wa ngwala ngwala akakingiwa kifua na dingi akaponyola Lupango asijue Wadudu hahongwi wala si Mlevi wala Athumani.  Dhambi zote kama hizi utaziweka wapi na kwanini usione urais mgumu hata kama siyo? Hapa ndipo unamkuta mtu akicheka au akitabasamu huku akilia moyoni japo hakwambii. Hali hii inahitaji uwe bonge la msanii vinginevyo utakufa wakati si wako au vipi. Hayo tuyache.
CHANZO: Nipashe.

No comments: