The Chant of Savant

Saturday 8 November 2014

Mevi atia timu Burkina kumung'oa dikteta

Kutokana na  urafiki na udugu wa Mlevi na marehemu Thomas Isidore Sankara, Rais wa zamani wa Burkina Faso  wiki iliyopita Mlevi aliamuru kwenda kutia timu kule Burkina ili kutia shime mapinduzi matakatifu ambapo ‘muimla’ wa muda mrefu wa kaya hii Blaise Compaore aka ‘Ebola’ aliangushwa.

Mbuyu huu ulipigwa chini fasta kwa nguvu ya walevi kayani humo.Walevi wa Burkina hawana mchezo na mafisi na mafisadi. Walimtimua Compaore na kuwagomea ndata kuchukua ulaji wao.
Hivyo, ninapoandika nafanya hivyo toka Ouaga kama wanavyopenda kuita mji wao mkuu Ouagadougou ukikosekana Wagadugu.
Nimefikia mitaa ya Avenue de Capitaine Thomas Sankara karibu na Lycee Phillipe Zinda Kabore kwenye mtaa maarufu wa Rue Nongremasson yaliko makutano na Ave de la Liberte kwenye hoteli ya Le Pavillon Vert. Naona yule anacheka akidhani hizi ni kamba.
 Si kamba hata kama sitanui na bi mkubwa wangu kwa kodi za walevi, bado ninao uchache wa kusafiria kwenda kufanya mapinduzi ili liwe somo kwa walevi wa kaya yetu.
 Kwa vile kilichokuwa kikiwakumba walevi wa taifa hili wanaoitwa “Burkinabe” kama ambavyo sisi tunaitwa Watanzania ni kile kile kinachowasibu walevi wa kayani mwetu.
 Mlevi amekwenda kule kupiga shule na siyo kupewa uprofesa wa kuchunga mbuzi kama wale wengine walioogopa umande wakaua elimu na kutukuza ufisadi. Mlevi licha ya kuwa msomi wa kweli, husaka elimu kila inapopatikana huku akichangia kwa kutoa elimu aliyo nayo kuhusiana na suala zima la ukombozi.
Pili mlevi alikwenda kwa Wa-Burkinabe kuwafariji ndugu wa marehemu Sankara na kuwapongeza kwa kuishinda Ebola ya kisiasa iliyokuwa ikiwatafuna kwa miaka 27.
Nina mpango wa kuonana na Mariam Sankara (mjane wa marehemu) vitegemezi vyake Phillipe na Auguste kule Ufaransa baada ya kuzuru makaburi ya Thomas mwenyewe hapa Ouaga na baadaye makaburi ya Margueriete Sankara na Sambo Joseph Sankara huko Yako kijiji alikozaliwa Sankara.
Katika ziara yangu ya Burkina niligundua yafuatayo:
Mosi, ukweli kuwa madaraka siku zote ni mali ya walevi sema walevi wenyewe huwa hawalitambui hili na kama wakilitambua wanajificha kwenye woga. Jamani, msiogope tena.  Kwani kiboko ya wakandamizaji na wauawaji wa waandamanaji kwa sasa yaani International Criminal Court (ICC) hailali ikiwatazama na kuwasaka wanaojaribu kuwaua waandamanaji.
Mnadhani Compaore alivyokuwa na roho mbaya alishindwa kuamrisha mbwa wake kuwasagasaga waandamanaji? Alitaka sana. Ila alipokumbuka hili dude liitwalo ICC alinywea na kuamua kutoka baruti kama mbwa aliyeiba mafuta.
Pili niligudua kuwa watawala hasa vidhabi wezi na mafisadi, licha ya kuwa wababaishaji na wenye kutishatisha hawajiamini.  Ni woga kuliko hata kichanga. Rejea Compaore na genge lake la majambazi walivyotoka nduki wasijue hata waendako bado wanaweza kunyofolewa na kuishia lupango kule the Hague.
Baada ya kuongea na upinzani nchini Burkina, niliwashauri wamshitaki kwa mauaji ya Sankara na wengine wengi  aliowaua kama vile mwandishi na rafiki yangu Norbet Zongo aliyefichua mauaji na utoaji wa kafara wa mazeruzeru aliofanya akimtumia ndugu yake Fancois Compaore aliyekuwa mshauri wake wa uchumi wakati ni kihiyo. Tatu, niligundua kuwa walevi wakichoka husema, “Sasa imetosha na liwalo na liwe.” Wakifikia hapa, hakuna risasi, mabomu ya machozi wala vipigo vinaweza kuwanyamazisha.
Nne, niligundua kuwa hata Bongolalaland aka Danganyika wana haja ya kulianzisha hasa wakati huu ambapo wamepokwa katiba yao na manyang’au yanayotetea uoza na ufisadi. Hivyo, jamani nasisitiza msiogope njia iko wazi kujiletea mabadiliko na mapinduzi ya kweli.
Saa ya ukombozi ni sasa. Tano, niligundua kuwa watawala siku zote wanatumia hila, longolongo na gilba, ukiwashupalia wanatoka nduki na kuacha kitu kwa walevi. Ila hapa kuna tahadhari. Mnapoamua kuwapiga chini wezi na watesi wenu, msiruhusu ndata kudandia na kupora ulaji kama ilivyotokea Masri ambapo ndata walichukua ulaji na kuandaa uchaguzi feki na kutwaa maulaji. Burkina walilikataa hili wazi wazi. Nanyi msikubali hili litokee.
Power is for boozers not ndatas or ndutus. Tumeelewana?
Katika uchunguzi upembuzi wangu wa kilevi, niligundua kuwa Compaore alifanya makosa yafuatayo:
Kwanza, kama wasaliti wetu walivyomsaliti mzee Mchonga, alisaliti mapinduzi matakatifu yaliyoongozwa na kamanda Thomas Sankara (Mungu aiweke mahali pema peponi roho yake).
Pili, alimuua Sankara mkombozi na nabii aliyekuwa ameahidiwa kuwakomboa Wabukinabe.Tatu, alikaa madarakani muda mrefu akiifuja kaya ya Burkina bila kujua kuwa mwisho wake ungefika.
Nne, hakusoma alama za nyakati sawa na wezi na mafisi na mafisadi wetu ambao hutumia madaraka kama kijiko kikubwa cha kuchotea utajiri wa walevi maskini asijue siku wakikengeuka wataipatapata fresh.
Tano, Compaore alijisahau na kujiona muungu mtu sawa na miungu wetu wanaofuja ulaji wetu wakigawana na kula kwa miguu na mikono bila kuomba wala kunawa.
Hata kama Compaore alibahatika kupewa upenyo na waramba makalio yake na kutimkia Cote d’ Ivoire, kuna siku watamtia nguvuni ili alipie madhambi yake hapa hapa duniani.
Wengi tulitamani yamkute yaliyomkuta Muamar Gaddafi ila aliponea chupu chupu. Kutokana na nilichoshuhudia Burkina, naweza kutabiti kwa kinywa kipana kuwa akina Compaore aka Ebola waliosalia barani kwetu watie maji baada ya mwenzao kunyolewa.
Wale ving’ang’anizi wawe wetu au magenge yaitwayo vyama waliong’ang’ania ulaji huku wakiwaibia na kuwahujumu walevi wakae mkao wa kuliwa na si kula. Hatuwezi kuendelea kutenzwa kama mataahira na  hayawani.
Tuna akili na nguvu ya kujitambua na kuwatambua na kuwafurusha wezi wetu wanaotutapeli kwa kujionyesha wana nguvu wakati si chochote si lolote. Akina EPA, Kagodam, Richmonduli, Escrew na majambazi wengine wakae mkao wa kuliwa tu watake wasitake.
Mwisho, kwa uchambuzi huu mfupi wa safari yangu ya Burkina naamini walevi watatia akilini na kuona mwanga kuwa wakiamua wanaweza hata leo kuondoa wale wanaowaibia na kuwatenza kama mabunga na mataahira. Kwa ufupi hiyo ndiyo ilikuwa safari yangu ya kujifunza na kufundisha ukombozi kwa walevi. SAA YA UKOMBOZI NI SASA. Haya shime walevi amkeni mjikomboe kweli kweli. Bye bye from Ouaga Burkina.

CHANZO: NIPASHE

No comments: